Mwanza: Mkuu wa Mkoa amtunishia misuli Waziri Magufuli

Sitta Tumma

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa mkoa huo, Injinia Evarist Welle Ndikilo, ametofautiana na maagizo ya Wizara ya Uchukuzi kuhusu amri ya kusimamishwa mara moja kivuko cha Mv. Sammar III, kinachofanyakazi za kusafirisha abiria kati ya jiji la Mwanza na Sengerema ndani ya Ziwa Victoria.

Utofauti huo umejidhihirisha leo hii (muda mfupi uliopita), baada ya RC Ndikilo kufuatwa ofisini kwake kisha kutakiwa kuzungumzia amri ya Wizara ya Uchukuzi chini ya Waziri wake, Dk. Harrison Mwakyembe iliyotolewa jana Januari 29 kwa barua kumb MN/2/3/04 kupitia Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Mkoa wa Mwanza, kukisimamisha kivuko hicho, na wakati wananchi bado wanakabiliwa na adha kubwa ya usafiri majini.

"Mimi kama Mkuu wa Mkoa na mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama wa mkoa huu, agizo la Wizara ya Uchukuzi silijui. Kamati yangu ya Ulinzi na Usalama ilishaagiza hiki kivuko kiendelee kufanyakazi eneo hilo, maana bila hivyo kuna hatari yaweza kutokea wanapojazana kwenye kivuko kimoja mamia ya watu. Muulizeni Mwakyembe kwa nini ameamuru hivyo?", alihoji Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza, Ndikilo kwa mshangao mkubwa!.

Uchunguzi uliofanywa na FikraPevu umebaini kwamba, Wizara ya Uchukuzi imetoa agizo hilo kwa makao makuu ya TPA Jijini Dar es Salaam, kisha amri hiyo ikaelekezwa kwa uongozi wa TPA Mkoa wa Mwanza, ambapo Kaimu Mkuu wa TPA Mwanza, Richard Msechu, ambaye pia ni Mkaguzi Mkuu wa Mamlaka hiyo ya Bandari Kanda ya Ziwa, amekiri kupokea maagizo hayo na kumwamuru mmiliki wa kivuko hicho cha Mv. Sammar III, Salum Ali atekeleze mara moja agizo hilo, ikiwa ni pamoja na kuhamishia huduma hizo eneo la Bandari, ili kupisha njia ya Reli, lakini eneo hilo kivuko kinapotakiwa kuhamia bado halijaandaliwa vizuri.

Mkurugenzi wa kampuni ya Sammar III, Salum ameeleza kushangazwa na kitendo cha Wizara ya Uchukuzi kukisimamisha kivuko chake kutoa huduma kwa wananchi, bila kupewa muda wa maandalizi ya kuhamia eneo jingine, na kusisitiza kwamba: "Nitaondoa kabisa huduma hii ya kusafirisha abiria kutoka jijini Mwanza kwenda Sengerema, iwapo nitaona shughuli hii imekuwa na migogoro mingi na kuathiri biashara zangu".

3 Comments
  • hiyo ni ishara ya wazi kuwa utawala wa CCM umefikia mwisho. Kama ilivyokuwa babeli ukiona kila 'fundi' anazungumza lugha yake,ujenzi wa mnara (Taifa) hauwezi kuendelea. TAFAKARI….

  • Ah, mbona hii habari haijakaa sawa aliyetunishiwa misuli ni nani Magufuli au Mwakyembe, maana kichwa cha habari kinasema hivi na habari yenyewe inaeleza vingine.

  • Chukua Chako Mapema(CCM) hawana jipya.
    ‘Kisha kutakuwako kundi moja(Tanzania)na mchungaji mmoja(CHADEMA)’-Yohana 10

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *