Moja ya suala ambalo limeleta changamoto katika malezi ni ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano hasa matumizi ya simu za kisasa/janja (smart kisasa). Mjadala uliopo katika jamii ni umri gani ambao mtoto anaweza kuruhusiwa kutumia simu? Na kwa nini?
Kutokana na umuhimu wa malezi, wazazi zaidi ya 1,000 kutoka katika majimbo 42 ya Marekani wameanzisha kampeni ijulikanayo ‘Wait Until 8th Movement’ inayokusudia kuwashawishi wazazi nchini humo kutokuwaruhusu watoto wadogo kutumia simu mpaka wafike darasa la 8.
Kampeni hiyo inasambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii, ilianzishwa na Brooke Shannon, mama wa watoto watatu miezi michache iliyopita ili kuungana na wazazi wengine duniani kuhakikisha watoto hawazuliki na mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano na matumizi ya simu.
“Wakati mtoto wangu mkubwa Grace akiwa darasa la awali (kindergarten), watoto kama 5 (katika darasa lao) walikuwa na simu,” ameeleza Shannon. “Tangu wakati huo imeshuka zaidi hadi kwa watoto wadogo, sasa naona watoto wengi wa madarasa ya awali wana simu za kisasa! Sasa imeenea kote.”
Mzazi mwingine, Shelly Gerson ambaye ameungana na Shannon katika kampeni hiyo amesema kuna madhara mengi ya kiafya na saikolojia yanayoweza kutokea kwa mtoto akianza kutumia simu katika umri mdogo.
“Nina hofu sana kuhusu madhara ya simu kwa maendeleo ya mtoto”, amesema Shelly na kuongeza kuwa, “Sitaki kumuweka mtoto wangu kwenye hatari zaidi za utotoni”.
Shannon anaeleza kuwa kuna kila sababu ya kuwalinda watoto na kuwawekea mipaka katika baadhi ya vitu ikiwemo kutumia simu ambazo zimeunganishwa na intaneti mpaka pale watapokuwa na ufahamu mzuri wa kupambanua mema na mabaya yanayotokea katika ulimwengu wa dijitali.
Kwanini umzuie mtoto kutumia simu?
Kuna orodha ndefu ya sababu ambazo wazazi wanatakiwa wazifahamu ili kuwakinga watoto dhidi ya matumizi ya simu katika umri mdogo:
Simu zinabadilisha dhana ya ‘utoto’
Asili ya mtoto ni utoto yaani kufanya mambo yanayoendana na umri wake ikiwemo kucheza na wenzake, kusoma vitabu, kutumia muda mwingi na familia ili kuhakikisha anajengwa katika mfumo mzuri wa malezi. Lakini simu zilizounganishwa na intaneti zina mchanganyiko wa mambo mbalimbali ambayo mtoto hatakiwi kuyaona au kuyasikia mpaka ifike umri fulani.
Simu zinasababisha urahibu (addiction)
Utafiti mpya unaonyesha kuwa utegemezi kwenye simu yako unatengeneza urahibu wa ubongo kama ule unaotokea kwa watu ambao wameathirika na ulevi, uvutaji sigara au kucheza kamali ambapo hawawezi tena kuacha tabia hizo.
Simu ni kama mashine ya bahati nasibu katika akili ya mtoto wako ambayo wakati wote inamshawishi kupekua zaidi kwasababu programu za simu na mitandao ya kijamii zimetengenezwa ili watu watumie muda mrefu ili kampuni zinazosimamia kazi hiyo zipate faida.
Simu ni kikwazo katika ujifunzaji wa mtoto
Elimu ya awali na msingi ndio msingi wa mafanikio ya kitaalama; mtoto anajifunza jinsi ya kuzalisha, kutunza muda, miradi na kazi za nyumbani. Kumpa simu kunatoa mwanya wa kuzorotesha taalama na maendeleo yake (academic mediocrity).
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa mtoto akianza kutumia simu, matokeo yake darasani yanashuka; Utafiti mwingine ulibaini kuwa watoto ambao hawaruhusiwi kuwa na simu shuleni wanafanya vizuri kwenye majaribio ya darasani.
Inasababisha matatizo ya usingizi
Tafiti zaidi zinaonyesha matumizi ya simu za kisasa na vifaa vingine vyenye mwanga wa kioo zinaathiri ubora wa usingizi kwa watoto wadogo. Watoto hawapumziki kwasababu wanashawishika kupokea ujumbe wa maneno kutoka kwa marafiki jambo linalovuruga mpangilio wa kulala wakati wa usiku.
Baadhi ya watoto huamka usiku kuangalia ujumbe au mitandao ya kijamii. Ukosefu wa usingizi kwa watoto unatajwa kuathiri afya ikiwemo ulaji mbaya, unene uliopitiliza, kudhoofisha kinga za mwili, udumavu na magonjwa ya akili.
Inaharibu mahusiano ya mzazi na mtoto
Wazazi wengi wanajuta kuwapa watoto wao simu kwasababu ukaribu kati yao umepungua. Ni jambo la kawaida kwa mzazi kuonana mara kwa mara na watoto wake ili kufahamu maendeleo yake na kumuongoza katika njia na mtazamo sahihi wa maisha.
Lakini akipewa simu mahusiano au ukaribu unapungua na mtoto anajikita zaidi kufuatilia mambo yanayoendelea ulimwenguni kupitia mtandao.
Inaongeza hatari ya kupata msongo wa mawazo na mkazo
Kwa asili watoto hawana uwezo mkubwa wa kukabiliana na udanganyifu na uhalifu wa kimtandao, ni rahisi kukutana na mambo ambayo yanaweza kumsononesha na kuathiri hisia zake.
Kuangalia maudhui ya ngono
Simu za kisasa zimewawezesha watoto kuangalia picha za ngono mahali popote. Soko la picha za ngono linawalenga vijana wanaotumia intaneti na kuwalaghai kwa picha mnato na video za utupu. Utafiti mwingine unaonyesha kuwa asilimia 42 ya vijana wanaotumia mitandao wamewahai kukutana na picha za ngono ambapo 66% ya hao walilazimishwa kuangalia kupitia matangazo ya mtandaoni.
Inaelezwa kuwa watoto hawaishii tu kuangalia picha za ngono bali hutengeneza za kwao na kuzisambaza, jambo linalohatarisha mustakabali wa maisha yao.
Kulingana na ripoti moja iliyochapishwa kwenye gazeti la New York Times, imeeleza kuwa wazazi wengi ambao wana ujuzi wa teknolojia huwazuia watoto wao kushika simu mpaka wafikishe miaka 14. Lakini wanaweza kupiga na kutuma ujumbe mfupi wa maneno, na wakifika miaka 16 wanaanzishiwa mpango wa kutumia intaneti.
Hata hivyo, maamuzi ya mzazi kumpa au kumnyima mtoto ruhusa ya kutumia simu yanabaki katika uwezo wake kwasababu ana jukumu la kumlea mtoto wake katika malezi ya bora.