OGP yaigharimu serikali. Yashutumiwa kuvuruga  bajeti ya maendeleo

Jamii Africa

Serikali imeshauriwa kuongeza uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa kuandaa na utekelezaji wa bajeti kuu ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa muhimu za vipaombele, miradi na maendeleo katika jamii.

Akizungumza katika mdahalo wa bajeti ulioandaliwa na taasisi ya Policy Forum, Afisa Programu kutoka  HakiElimu, Godfrey Boniventura alisema uundaaji wa bajeti tangu ngazi ya kata hadi taifa sio shirikishi jambo linalokwamisha utekelezaji wa vipaumbele vya wananchi.

Alisema kuwa ushirikishwaji mdogo wa wananchi unatokana na serikali kushindwa kuweka wazi bajeti kuu kwenye tovuti ya wizara ya Fedha na Mipango na kutoa vitabu vya bajeti kama sheria ya Bajeti (2014) inavyoagiza ili viwafikie wananchi katika maeneo yao.

Boniventura ambaye alishiriki kwenye utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Ubia wa Bajeti (IBP) juu ya uwazi wa bajeti za nchi mbalimbali duniani mwaka 2017 ulibaini kuwa taarifa muhimu za bajeti ya Tanzania haziwafikii wananchi kwa wakati ambapo ni changamoto katika kukuza uwazi na uwajibikaji serikalini.

“Changamoto ni kwamba vitabu vya bajeti havitolewi kwenye website (tovuti) ya wizara, ukienda sasa hivi mara ya mwisho kilitolewa mwaka wa fedha 2015/2016. Mwaka wa fedha 2016/2017, 2017/2018 havipo kwahiyo ni changamoto kidogo”.

Kulingana na ripoti ya utafiti huo inaeleza kuwa mwaka 2017, Tanzania ilipata alama 10 kati ya 100 ambapo iko chini ya wastani unaotakiwa wa 42 na kujumuishwa kwenye nchi ambazo hazina uwazi kwenye bajeti ya taifa inayotakiwa kuwa wazi kwa wananchi wa kada zote.

Tanzania imeshuka kwa alama 36 ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo ilipata alama 46. Alama za Tanzania zimeshuka kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na utafiti huo ambayo yanazitaka nchi ziweke bajeti zao kwenye mtandao (tovuti) kama kigezo muhimu cha uchapishaji wa taarifa za bajeti.

“Matokeo ya uwazi wa mfumo wa bajeti ni mabaya sana kwasababu Tanzania imepata alama 10 kati ya 100 kwa mwaka 2017 sasa kuna tofauti kubwa sana na matokeo ya 2015 ambapo ilikuwa alama 46, hii ni ishara kwamba kuna taarifa nyingi hazikuweza kutolewa”, alisema Boniventura na kuongeza kuwa,

“Taarifa ya msingi ambayo ilitakiwa itolewe kwenye tovuti au kwenye mtandao ni taarifa ya bajeti ya awali lazima kwa viwango vya utafiti ilitakiwa kutolewa mwezi mmoja kabla sasa haikuweza kutolewa”.

Alama hizo zinaiweka Tanzania miongoni mwa nchi zenye fursa chache kwa wananchi kutengeneza bajeti inayoakisi vipaumbele na matakwa yao katika jamii.

Ripoti ya utafiti huo inaeleza kuwa Bunge la Tanzania kupitia kamati za kudumu zimefanya kazi nzuri ya kusimamia mchakato wa kutengeneza bajeti lakini imeonyesha udhaifu wa usimamizi wakati wa utekelezaji wa bajeti.

Ikumbukwe kuwa mwaka 2017, serikali ya Tanzania ilijitoa kwenye Mpango wa Uendeshaji serikali kwa Uwazi (OGP) kwa madai kuwa inafungamana na kanda nyingine ambazo zinatekeleza uwazi na uwajibikaji.

Kauli ya utafiti huo inaungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ambaye alisema nguvu ya Bunge kusimamia bajeti imepungua ukilinganisha na Bunge la awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwasababu Serikali imeingilia mamlaka ya Bunge na kuzuia wabunge kujadili kwa uwazi vipaumbele za wananchi.

“Nyingine ambayo tumeiona ni Bunge kutopata taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mara kwa mara. Kwa mujibu wa sheria ya Bajeti ya mwaka 2014 ilikuwa inatakiwa Serikali kila baada ya miezi mitatu kwa maana mara nne kwa mwaka iwe inapeleka taarifa Bungeni juu ya utekelezaji wa bajeti” alisema Zitto na kufafanua kuwa,

“Baadaye kifungu hicho kilibadilishwa mpaka ikawa ni mara mbili kwa mwaka lakini Serikali haifanyi hivyo kwasababu inatakiwa taarifa ipelekwe kwenye kamati ya Bunge ya Bajeti ambayo kwa sasa hivi inaongozwa na mama Hawa Ghasia lakini Serikali haifanyi hivyo. Kwahiyo hivi ni baadhi ya vitu ambavyo vinasababisha vigezo vyetu kushuka kimataifa na sasa hivi katika nchi za Afrika Mashariki sisi ni wa pili kutoka chini tumezidiwa na Burundi tu”

Zitto amesema kama hakuna uwazi katika bajeti ni rahisi kutumia matumizi nje ya bajeti. “Kuna haja kama watanzania na kupitia Bunge na Asasi zisizo za kiserikali kuangalia uwezekano wa kuhakikisha kwamba tunarudi katika mstari na vigezo tulivyokuwa navyo”

Ameongeza kuwa ripoti ya utafiti huo ni muhimu ipelekwe mbele ya kamati ya Bunge ya bajeti ili kuiamsha Serikali kutekeleza wajibu wake katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji unakuwepo kwenye uandaji na utekelezaji wa bajeti.

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka taasisi ya kilimo ya wanawake Tanzania (TAWLAE), Mary Liwa alisema wananchi wanapaswa kuelimishwa na kujengewa uwezo wa kufuatilia mchakato wa bajeti inapoandaliwa na mpaka utekelezaji wake ili kuhakikisha inakidhi matakwa yao na sio maslahi ya wanasiasa.

Naye, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Richard Mbunda alishauri kuwa serikali inatakiwa itathimini na kutengeneza mipango na mikakati itakayosaidia matumizi yote kujumuishwa kwenye bajeti kuu ili kuepusha ufisadi kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *