Ongezeko la bajeti isiyoendana na mahitaji ya lishe kuathiri afya za watoto nchini

Jamii Africa

Licha ya kuongezeka kwa bajeti inayoelekezwa katika sekta ya lishe nchini, bado haijafanikiwa kutokomeza tatizo la udumavu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 5, jambo ambalo linaathiri maendeleo ya kiafya kwa watoto hao.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mapitio ya bajeti ya Lishe inayotolewa na Shirika la Watoto duniani (UNICEF-2015/2016) nchini Tanzania inaeleza kuwa bajeti iliyotengwa kwenye shughuli za lishe ya taifa imeongezeka hali iliyochochea ongezeko la matumizi mara mbili zaidi katika sekta hiyo ya mwaka wa fedha wa 2011/2012 na 2014/2015.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa matumizi halisi katika sekta hiyo kwa mwaka 2011/2012 yalikuwa bilioni 10.5 na bajeti hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka na hadi kufikia 2014/2015 ilikuwa bilioni 22.5. Licha ya ongezeko hilo bado bajeti hiyo haikidhi mahitaji yote ya lishe inayoelekezwa katika sekta mbalimbali ambazo zinahusika kuboresha afya za watoto.

Matumizi ya bajeti ya lishe yanaelekezwa katika maeneo matatu makuu ambayo ni kuhimiza ulaji wa chakula bora kwa watoto wachanga na watoto wadogo; kuzuia na kupambana na utapiamlo na kuboresha mazingira kuiwezesha serikali kutoa huduma bora za lishe nchini. Shughuli zote hizo zinaratibiwa na sekta za afya na ustawi wa jamii, maendeleo ya jamii, jinsia na watoto; elimu; kilimo, usalama wa chakula; maji na usafi; mifugo na uvuvi; biashara na viwanda na taasisi za fedha.

 Mathalani, mwaka 2011/2012 sekta ya lishe ilitenga bajeti ya bilioni 121 kutekeleza miradi mbalimbali lakini zilizopatikana ni bilioni 10.5 na makisio hayo ya bajeti yamekuwa yakiongezeka kila mwaka kutokana  na ongezeko la watoto walio chini ya miaka 5. Na ilipofika mwaka 2014/2015 makisio yalikuwa bilioni 183 lakini matumizi halisi yalikuwa 22.5 pekee. Hii ni kwa mujibu wa mapitio ya Takwimu za lishe.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya bajeti hiyo inategemea fedha za wafadhili. Katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 ufadhili wa washirika wa maendeleo kutoka nje kwenye lishe ulikuwa asilimia 55.8 ya matumizi yote ya sekta hiyo. Na utegemezi huo uliongezeka kutoka asilimia 44.5 mwaka 2013/2014 ambapo asilimia 44.2 ilikuwa ni mapato ya ndani.

 

Bajeti ya lishe inavyotumika

Ripoti ya UNICEF  inaeleza kuwa utekelezaji wa bajeti ya lishe umekuwa ukitofautiana kila mwaka kutokana na mabadiliko yanayojitokeza katika ofisi ya hazina. Tangu mwaka 2011/2012 hadi 2014/2015 wizara ya Afya imetumia chini ya nusu ya bajeti yake iliyoelekezwa katika sekta ya lishe.

Inaelezwa kuwa tangu 2011/2012 hadi 2014/2015 zilitengwa bilioni 15.5 kwenda sekta ya lishe lakini ni bilioni 6.7 tu ndio zilipokelewa na kutumika katika sekta hiyo.  Hii inashiria kuwa juhudi za kuboresha lishe kwa watoto bado zinahitaji utashi wa kisiasa na uwekezaji mkubwa ikizingatiwa kuwa fedha zinazoelekezwa katika sekta husika hazitimizi mipango iliyowekwa na kuathiri watoto walio chini ya miaka mitano.

Watoto wanahitaji viini lishe na mlo kamili ili wakue vizuri lakini kutokana na changamoto ya bajeti na umaskini wa kaya, hujikuta wakipata utapiamlo na kudumaa jambo linaloathiri afya na uelewa masomo darasani.

 

Hali ya Udumavu nchini

Emmanuel John (2) ngozi yake imekunjamana, tumbo kubwa na anaonekana mwenye huzuni, akiashiria ana matatizo ya kiafya.

Akiwa karibu na mama yake, Janeth Elias, ambaye  anauza chakula eneo la Kijitonyama, Wilaya ya Kinondoni, Emmanuel anaonekana kuwa na tumbo kubwa na urefu wake hauendani na umri alionao. Mtoto huyo amekumbwa na udumavu  tangu akiwa mdogo.

Emmanuel ni miongoni mwa asilimia 24 ya watoto wote duniani waliodumaa, ambapo kati ya watoto wanne walio chini ya umri wa miaka mitano, mmoja amedumaa na inakadiriwa zaidi ya watoto milioni 165 duniani wana udumavu.

Shirika la Afya Duniani (WHO), linaeleza kuwa matatizo ya kudumaa ni miongoni mwa majanga makubwa yanayokwamisha maendeleo ya binadamu.

Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu vya udumavu, ikiungana na nchi nyingine za Afrika ambazo zinakumbwa na ukame, ukosefu wa chakula na huduma mbovu za afya ya mama na mtoto.

FikraPevu imepata Ripoti ya Uchunguzi  ya Taifa ya Lishe (2014) ambayo inabainisha kuwa asilimia 34.7 ya watoto wenye umri wa mwezi 0 hadi miezi 59 (0-59) wamedumaa au wana Utapiamlo wa kiwango cha juu.

Kwa Tanzania Bara, matokeo ya uchunguzi yanaonesha kiwango cha utapiamlo kiko juu zaidi ya asilimia 40 kwa mikoa 9 (Iringa, Njombe, Kagera, Dodoma, Ruvuma, Rukwa, Kigoma, Katavi na Geita) na katika mikoa hiyo iko yenye kiwango cha juu ya asilimia 50, Iringa (51.3%), Njombe (51.5%) na Kagera (51.9%).

Zanzibar ina viwango vya udumavu ambavyo vinatofautiana kati ya eneo na eneo, Mjini Magharibi ni asilimia 20 na Unguja Kusini ni asilimia 30.4.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, zadi ya watoto milioni 2.7 walio chini ya umri wa miaka mitano wamedumaa nchini Tanzania ripoti hiyo inaeleza na kushauri hatua za haraka zichukuliwe katika mikoa ya Kigoma, Kagera, Mwanza, Iringa na Mbeya ambayo tatizo ni kubwa.

FikraPevu imeelezwa kuwa utapiamlo unatajwa kuwa sababu kubwa inayofanya watoto wengi kutokuwa na maendeleo mazuri ya ukuaji. Lishe duni isiyo na virutubisho muhimu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano humfanya mtoto kupungua uzito na urefu kutoendana na umri alionao.

 

Suluhisho

Kwa kutambua changamoto za lishe, serikali iliamua kusogeza huduma za lishe karibu na wananchi wa kawaida kwa kuajiri wataalamu wa lishe ambao wako kila Halmashauri kutoa miongozo ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa lishe (NNS) na kuhakikisha kunakuwa na matumizi mazuri ya rasilimali za afya

Hata hivyo, mpango huo umetekelezwa kwa sehemu na jambo linalohitajika ni kuongeza bajeti ya lishe ili kuwanusuru watoto dhidi ya utapiamlo na udumavu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *