RAAWU: Serikali imehusika kumdhuru Dk. Ulimboka

Jamii Africa

CHAMA cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti nchini (RAAWU), Kanda ya Ziwa kimelaani vikali kitendo cha kinyama cha kupigwa na kuumizwa vibaya, alichofanyiwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka, na kudai kwamba, unyama huo umefanywa na Serikali yenyewe.

Katibu wa RAAWU Kanda ya Ziwa, Ramadhani Mwendwa, akisisitiza jambo huku akionesha vitabu vya sheria na utumishi. (Picha na Sitta Tumma).

RAAWU imesema, ushahidi wa mazingira unaonesha dhahiri shahiri kwamba Serikali imehusika kwa namna moja au nyingine kumdhuru kiongozi huyo wa madaktari nchini, ikiwa ni lengo la kutaka kuzima mgomo wa madaktari unaoendelea katika kudai maslahi na huduma bora ya matibabu kwa Watanzania.

Kauli hiyo imetolewa mchana wa leo Jijini Mwanza na Katibu wa RAAWU Kanda ya Ziwa, Ramadhani Mwendwa, wakati alipozungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake kuhusiana na tukio hilo la kinyama, lililotokea majira ya saa 6 usiku wa kumkia juzi, ambapo watu watatu wanaodaiwa kuwa na silaha aina ya Short gun na bastola walimteka Dk. Ulimboka eneo la barabara ya Tunisia, Kinondoni jijini Da re Salaam.

“RAAWU tunalaani vikali sana unyama huu. Na hapa mimi ninadhani Serikali imehusika kumdhuru kiongozi huyu wa Madaktari nchini. Huu ni unyama usiovumilika wala kufumbiwa macho.

“Serikali badala ya kutatua matatizo inaanza kutumia mabavu kuwapiga viongozi wanaotetea maslahi ya Watanzania. Isijidanganye kwamba kutumia mabavu ndiyo itakuwa suluhu ya matatizo. Kwa unyama aliofanyiwa Dk. Ulimboka iwe chemichemi ya wafanyakazi wote kuungana na viongozi wao kudai kwa nguvu zote haki zao”, alisema Katibu Mwendwa.

Mwendwa ambaye pia ni Katibu wa Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), Mkoa wa Mwanza, alikwenda mbali zaidi kwa kusema kwamba, manyanyaso na ukandamizwaji mkubwa unaofanywa na Serikali inaonesha wazi kwamba viongozi wa Tanzania wanawapeleka wananchi wao katika machafuko aliyoyaita ya udiktetaship.

“Ninavyoona mimi, hivi sasa nchi inaelekea kwenye machafuko yanayotokana na udiktetaship. Tusifike huko kama nchi nyingine zinavyopigana. Viongozi wa wafanyakazi tuweni wamoja na wafanyakazi wote katika kutetea maslahi ya taifa. Tusirudi nyuma”, alisema Mwendwa.

Alisema, iwapo Serikali itaendelea kuonesha ‘udhaifu’ wake katika kusimamia maisha ya Watanzania, machafuko yanayotokea katika nchi mbali mbali hapa duniani yanaweza kuikumba pia Tanzania, na kwamba lazima viongozi na Serikali wakae pamoja na wafanyakazi wao kisha kuzungumza na kutatua kero zilizopo, na si vinginevyo.

Akizungumzia kuhusu kodi kubwa wanazotozwa wafanyakazi, Mwendwa ambaye amekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya wafanyakazi na Watanzania kwa ujumla, aliwaonya wabunge wa CCM na wengine kuacha kushabikia bajeti mbovu isiyokuwa na tija kwa taifa, kwani ushabiki huo unalididimiza taifa hili.

Alisema, hivi sasa Serikali imekuwa ikiwatoza kodi kubwa wafanyakazi, wakati kipato chao ni kidogo cha sh. 170,000, na kwamba lazima Serikali ibuni njia mbadala ya kukusanya mapato kutoka katika vyanzo vingine vingi, na si kuwakandamiza kwa mzigo mzito wafanyakazi wake.

“Ifike kipindi wafanyakazi waigomee Serikali ndiyo itasikia. Vyanzo vya mapato vipo vingi sana, lakini mzigo wa kodi anatupiwa mfanyakazi, na wabunge wa CCM wanatetea na kuungana na uozo wa Serikali hii”, alisema Katibu huyo wa RAAWU Kanda ya Ziwa, Mwendwa.

Aidha, Katibu huyo wa RAAWU aliionya Serikali kuacha tabia yake ya kuwafukuza kazi watumishi wake wakiwemo madaktari pale wanapogoma kudai maslahi yao ya msingi, na kwamba badaya yake ikae nao pamoja na kuweka makubaliano ya kumaliza adha zinazowatatiza, kwa maslahi ya taifa na Watanzania wote kwa ujumla.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Mwanza

15 Comments
  • Kaka yangu mwendwa unachokisema kina mantiki hapa! Serikali ikae chini na madaktari ili kumaliza tatizo hilo kwani wanaoumia ni sisi.

  • Lazima mkae mfikili kwani madactol wamesoma wanaelewa wanacho fanya.Serikali jalibuni kuelewa hili na sioninyi ndio muwe wasemaji wamwisho

  • Hotuba ya mheshimiwa rais yawezekana kuna watu imewapa matumaini lkn zile mashine na vitanda wagonjwa kulala wawili wawili inakuwaje??

  • Tatizo ni kwamba Watanzania wengi ni waoga wa mabadiliko. Tutavumilia uozo huu mpaka lini?

  • Iko siku viongozi wetu watajutia maamzi yao. Badala ya kuacha kazi kama JK alivyosema, watumishi wataendelea na kazi lakini badala ya kufanya “kazi bora” wao watafanya “bora kazi” na matokeo yake yatakuwa kama ya wanafunzi 5000 sekondari hali hawajui kusoma na kuandika! Tunajenga taifa gani?

  • Sitegemei kuwa RAAWU ina uchungu na maelfu waliokufa kutokana na mgomo badala ya kushauri kwa hekima ili hili lisawazike vema na daktari ajitambue kuwa anayemsababishia kifo ni nduguye awe na huruma leo RAAWU inachochea chuki ya kuwa serikali inahusika mbona kuhusika kwa Ulimboka kwa vifo wa watanzania maskini nchi nzima hamuongelei ambapo ni suala halihitaji uchunguzi hii inaonesha jinsi maslahi yalivyo mbele na utu nyuma. Tutambue uwepo wa Mwenyezi Mungu tutende mapenzi yake tupone salama na balaa ya kizazi hiki.

  • Pole sana Dr Steven Ulimboka kwa yaliyokukuta, lakini Mungu ni mwema kwako bado anakupenda utapona na baadaye utakuja kuwaambia watanzania ilivyokuwa.
    Napenda kutoa maoni yangu kuhusu hali hii ya mgomo wa madaktari inayoendelea au mgomo uliokuwepo nchini.
    Nikikumbuka enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere tulikuwa na chama kimoja tu cha kutetea wafanyakazi “Juwata”. Chini ya uongozi wa chama hiki wafanyakazi wote walikuwa wanapitishia malalamiko yao na serikali ilikuwa inayafanyia kazi na wakati mwingine kila kwenye siku kuu ya wafanyakazi mei mosi Mheshimiwa Raisi alikuwa anaongeza mishahara na marupurupu mengine kulingana na pato la Taifa na wafanyakazi wanafurahi ingawa kwa kunungunika.
    Lakini hali imeendelea kubadilika jumuia za wafanyakazi zikawa nyingi, viwandani, madaktari walimu nk kila jumuiya inatetea wafanyakazi wake wakasahau umoja ni nguvu. Zikaanza taaluma , nyingine zikaitwa rare profession mishahara yao ikaanza kuwa mikubwa, taaluma kama za kukusanya mapato zikapata upendeleo ili kukusanya mapato mengi zaidi na kupunguza wizi lakini kinyume chake wizi ukaongezeka.
    Idara nyeti za serikali kama benki kuu zikapewa mifumo tofauti ya mishahara lakini matatizo ndiyo yakaanza kama ya EPA .Madaktari na walimu nao wakajiona ni wa muhimu zaidi wakaanzisha migomo ya mara kwa mara na kusahau wajibu wao wa kuhudumia jamii kwanza. Serikali ikasahau kuwa ni kama baba na hizi rare profession ni kama watoto je baba anaweza kumbagua mtoto wake. Mfagizi asipo fagia ofisi kwa wiki moja /au mzoa taka za jiji jiji litanuka je nao wagome, wahasibu wakikataa kulipa mishahara ya watumishi kilio kitakuwaje nao wagome, mkulima akikataa kulima njaa itakuwepo hata huyo mkubwa atathirika naye agome,nk Kwa maoni yangu Serikali ijipange upya kuangalia pato halisi la Taifa na mgawanyo wake.
    Naweza kusema yote haya yamesababishwa na ufisadi unaoendelea nchini , kwani watu wachache wana maisha mazuri wanaishi kama wapo peponi kwa fedha za walipa kodi. Tumesikia baadhi ya watu wachache wanalimbikiza fedha mabilioni ya dola kwenye benki za nje ya nchi kwa miradi ya mafuta na gesi ambayo ingekuwa ndiyo mkombozi wa watanzania ,lakini wachache hawa wanataka kunufaika wenyewe,
    Tumesikia baadhi ya wabunge waliokuwa mawaziri wamekutwa na mabilioni ya fedha lakini wanapohojiwa wanasema ni visenti. Hali hii ndiyo inayochangia kwa kiwango kikubwa baadhi ya wafanyakazi wetu kugoma kwani wanaona uchumi wetu haugawanywi ipasavyo na wakiangalia wafanyakazi katika nchi jirani wanalipwa vizuri na labda uchumi wao ni mbaya kuliko wetu
    Kwa mtazamo wangu hebu viongozi kuanzia ngazi za juu wajisafishe tukumbuke usemi wa marehemu Julius Kambarage kuwa kwa nini watu tunakimbilia Ikulu. Viongozi wote Mungu aliopenda kuongoza Taifa hili wawe waadilifu waone kama wamepewa dhamana tu ya kuongoza Taifa hili, Utajiri uliopo kwenye nchi hii uwe wa watanzania wote kama nilivyosoma kwenye vyombo vya habari kuhusu utajiri wa Gesi tulionao kutoka kwa waziri wa Nishati na madini
    Tumeona waheshimiwa kwa mfano waziri Mkuu mstaafu Lowasa anataka Gesi hii iweze kutumika vyema kwa kuanzisha viwanda vya pamba kuleta ajira kwa vijana hili ni jambo jema kabisa kupunguza watu wasio na kazi na kuongeza kipato
    Kwa maoni yangu naomba gesi hiyo pia itumiwe majumbani kwenye viwanda mashuleni kwenye makambi ya jeshi ili kupunguza ukataji miti na kuleta mvua nyingi kwa ajili ya kilimo kama inavyotumika kwenye nchi zilizoendelea kama Marekani na Ulaya
    Mbona Tanzania kuna maeneo mengi kama madini , mali asili , milima bahari , utalii na ambayo yakitumiwa vizuri na fedha zake zikijulikana vyema pato la Taifa litaongezeka uchumi utakuwa mishahara itakuwa mizuri na migomo itapungua.
    Namwomba Mheshimiwa Raisi Kikwete na baraza lake la mawaziri waliangalie tena swala hili linalosababisha migomo ili hali ya utulivu uliokuwepo wakati wa Uongozi wa mwalimu Nyerere urudi
    Mungu ibariki Tanzania na watu wake

  • mgomo huwa haukuwekwa kwa baadhi ya watu au taasisi,bali ni hali isiyokuwa nzuri lakini inabidi. Ukiwa unataka gari lako lisikupe shida ya matengenezo ya gharama kubwa ni kujali utunzaji wake na kulicheki kila unapotaka kuliendesha. ukililazimisha kuna siku litakugomea na huenda ikawa ndo mwisho,au likugharimu sana.

    Madaktari si malaika,ni watu ambao pamoja na huduma yao nyeti,huwa wanalipwa mishahara,kama ingekuwa ni kufuata kigezo cha wito,basi ina maana hata wakinyimwa mishahara lazima ,,wafanye kazi,je ni kweli hiyo? sasa basi kila kazi ni ya wito,hakuna kazi isyohitaji wito,kama kuna mjinga anafikiri hivyo basi anajidanganya mwenyewe na matokeo ni kuwa omba omba kama serikali yetu.Rasiliali tunazo za kutosha tuishi kama nusu ya paradiso.

    Huko vigogo wanapokimbilia kutibiwa wenzao walitumia kila rasilimali walizo nazo,na zingine wakapora za kwetu,wakasimamia vyema matumizi ya serikali,sasa wanapeta. Sielewi viongozi wetu wanapokuwa ughaibuni hawavutiwi kuiga maendeleo ya wenzetu na kufanya kama wao?hata kama utamlipa dkt. mmoja milioni 10 kwa mwezi,je tunao wangapi,je shangingi ngapi zinatosha kuwalipa madokta?

    Hebu tufanye hesabu ya kutoa na kujumlsha; tuchukulie tuna madaktari 4000, ukiwalipa 10m/- kwa mwezi klia mtu tunapata 40000000000.sawa na 40bil.au 480bil kwa mwaka.shangingi moja ni 200m/-,tuna mawaziri 56,sawa na 11.2bil/-,bado makatibu wakuu,wakuu wa mikoa,wakurugenzi,idadi yao ikijumlishwa utapata jibu,bado matengenezo yake[services].hayana bima,yanakunywa mafuta kisawasawa,kigogo akitaka kwenda nje ya mkoa,anapanda ndege,shsngingi linapita aridhini likampokee huko aendako,dereva atalipwa posho,mafuta ndo usipime,je si kodi yote inaishia kwenye mashangingi,nani anajali -wacha wagonjwa walale watatu kitanda kimoja wapumzike manake wakishapata nguvu wanaambiwa dawa hakuna,siku zikipita wanaambiwa dawa bohari kuu zimeharibika,uchaguzi ukifika – tudumishe amani na msikamano- kwa wagonjwa wanafanya hivyo kivitendo si wanashirikiana vitanda.

    IKO SIKU MUNGU ATASIKIA KILIO CHA WATU WAKE,HAPO HAO WANAOWATESHA WATATAMANI ARDHI IWAMEZE.

  • serikali iache ubabe ya kweli wayakubali ndipo uongo unaweza kujitenga,basi wabunge wasipelekwe kutibiwa nje kama hospitali zetu zina vifaa vyote,nao waje walale kwenye kitanda wagonjwa 4.

  • Anachokisema ndugu Mwendwa ni cha kweli kabisa nami naungana nae kwani huo ndio uongozi halisi wa kutokuegemea upande wowote hasa katika maslahi ya taifa hili. Serikali inahusika kwa asilimia 100 kumteka Dr. Ulimboka na ilivyo na jeuri na ukandamizaji wanathubutu hata kutunga uwongo wa kusema wamemkamata mtekaji wa Dr. Ulimboka ili tu watanzania wasizungumzie habari ya uchafu wa serikali kwa kisingizio cha kusema kesi iko mahakamani.

    Lakini kwa upande mwingine sisi raia wa Tanzania tuna matatizo makubwa sana sijui nani katuroga, mara nyingi tunaposikia habari za dhuruma zinazofanywa na watu waliobeba dhamana ya kuliongoza taifa hili huwa tunapiga kelele siku mbili tu baada ya hapo kimya tunahamia kwenye kushabikia Taifa stara na likitokea lingine hivyo hivyo tunalisahau la jana tunashabikia la leo lakini kwa hili la Ulimboka nawaomba watanzania tusinyamaze kamwe kwa serikali hii yenye uozo na ufirauni wa kila aina.

    Tusiogope maneno ya kijinga ya kina Job ndugai waliogeuka kuwa wapiga debe wa shetani na uovu wake wala ya akina Jenister mhagama walioligeuka taifa hili na kuwa malaika wa vitendo viovu vinavyofanywa na serikali yao wala tusiwaogope kina Willium Lukuvi mawakili wa wa serikali yenye kujaa kila aina ya ukandamizaji na wala tusiwaogope kina Werema waliogeuka kuwa wanasheria wakuu wa chama cha mafisadi badala ya kuwa wanasheria wa serikali na wengine wengi wenye kujaa mikono yenye damu ya watanzania na msiogope matusi ya akina Nchemba wenyue uwezo finyu wa kufikiri na kuona mbali huku wakitumiwa na mabwana zao kutetea uozo wa chama cha kishetani, Akina Mwendwa itisheni maandamano ya nchi zima ambayo hayatakoma hata kwa mwaka mzima hata akina Kova watuteke wote mpaka watuambie kwanini wanafanya unyama wa namna hii katika nchi wanayoiita nchi ya amani.

    Wenu mlopokaji

  • Ni kweli watu wamekufa kutokana na hii migomo inaaumiza sana coz most ni wale wananchi maskini walioshindwa kumudu gharama za matibabu ktk hospitali binafsi. Wakubwa wakiigua wataenda popote watakapo kupata matibabu so inahuuuuuuu……………………….. hawaangalii we choka mbaya as they said mwenye shibe hukumbuki mwenye nja……………….. this is ugly truth

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *