RAIS John Magufuli ametishia kufunga migodi yote inayomilikiwa na wawekezaji kutoka nje ikiwa wawekezaji hao watashindwa kuanzisha mazungumzo haraka juu ya umiliki wao pamoja na kodi wanazopaswa kulipa.
Amesema kuliko kuwaachia wageni waendelee kuchimba madini huku wakikwepa kodi, ni bora awanyang’anye na kuwapatia Watanzania ambao watalipa kodi kwa manufaa ya taifa.
Rais Dkt. John Magufuli
Rais Magufuli ameyasema hayo leo Ijumaa, Julai 21, 2017 mbele ya wakazi wa Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Nyakanazi – Kibondo yenye urefu wa kilometa 50.
“Kuna haja gani ya kuwa na wawekezaji wanaochukua rasilimali zetu bila kulipa kodi? Ni heri nifunge migodi niwapatie Watanzania ambao najua watalipa kodi kwa maendeleo ya taifa letu,” alisema huku akisisitiza kwamba lengo lake ni kutetea maslahi ya Watanzania wote bila kujali itikadi zao.
Aidha, amesema haiwezekani makampuni hayo yanaendelea kuwa kimya wakati wameshakubaliana kuanzisha mazungumzo haraka.
"Makampuni ya madini yaliyoahidi kukaa na serikali kuzungumza, wafanye haraka, wakiendelea kuchelewa nitafunga migodi yote wanayomiliki… wapo wengine tutakutana nao hivi karibuni, lakini wengine hawajaonyesha dalili," alisema Rais Magufuli.
Kauli ya Rais Magufuli imekuja wakati tayari Serikali imesimamisha utoaji wa leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini hadi Tume ya Madini itakapoundwa na kuanza kazi na kwa sasa baadhi ya shughuli za tume hiyo zitafanywa chini ya usimamizi wa Kamishna wa Madini.
Hatua ya kusitisha leseni inatokana na uwepo wa Sheria mpya iliyoanza kutumika Julai 7, mwaka huu ambayo pia imeufuta Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA).
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, James Mdoe, ameyasema hayo leo Ijumaa, Julai 21, 2017 katika mkutano na waandishi wa habari ambapo amesema mbali na kufutwa kwa wakala huo pia sheria hiyo imeelekeza kuanzishwa kwa Tume ya Madini, na kuongeza malipo ya mrabaha kutoka asilimia nne kwa madini ya Metali (dhahabu, shaba, fedha) hadi asilimia sita.
Pia imeelekeza kuongezeka kwa malipo ya mrabaha kutoka asilimia 5 kwa madini ya almasi na vito hadi asilimia sita.
Kero ya kodi
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa ataendelea kupambana na kodi zenye kuwakera wananchi hasa wananchi wa hali ya chini.
Wananchi wakimsikiliza Rais Magufuli akihutubia Kakonko mkoani Kigoma
Amesema mpaka sasa serikali imeondoa kodi katika kilimo na mazao takribani 80 ambazo zilikuwa kero kwa wakulima na itaendelea kuzipunguza mpaka wakulima wafaidike na kilimo hicho.
“Tumefuta tozo 80 katika kilimo na mazao. Tushikamane wakulima wote ili kuendeleza nchi yetu, na tumefuta tozo zaidi ya 50 katika mifugo na bado tutaendelea kuzifuta tozo kwa wananchi wanyonge ili wafaidike na kilimo pamoja na ufugaji” amesema Rais Magufuli.
FikraPevu inafahamu kwamba, kwa muda mrefu wakulima vijijini wamekuwa wakisumbuliwa pindi wanaposafirisha na kuuza mazao yao kwa kubambikiwa kodi nyingi, hali ambayo ilikuwa inaendelea kuwadidimiza kiuchumi badala ya kuwakwamua.
Rais Magufuli amesema ilifikia wakati wafugaji walikuwa wanalipa kodi ya kwato, kwa maana ya kila kwato ilikuwa ikilipiwa kodi.
Wakwepa kodi
Rais Magufuli amesema kwamba, anachukia watu wanaokwepa kodi huku akisisitiza kwamba, wanaokwepa kodi siyo wananchi wa kawaidia bali ni matajiri wakubwa wakubwa.
“Wamiliki wa vituo vya mafuta wanabaki na kodi za wananchi wale wanaolipa kodi wanunuapo mafuta. Hao nitalala nao mbele, nimeshawaagiza ndani ya siku 14 wafunge mashine ( za kielekitroniki – EFD).
“Serikali ikikusanya kodi, hizo kodi zitarudi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wote,” amesema.
Amesema wakati serikali yake inaingia madarakani walikuwa wanakusanya mabilioni ya shilingi, lakini walipobana wakakusanya kati ya Shs. 1.2 hadi 1.3 trilioni. “Nina uhakika tukibana zaidi tutakusanya Shs. 3 trilioni.”
Amesema, fedha nyingi zimekuwa zikivuja serikali kutokana na matumizi mabaya ndani ya serikali kama semina, posho na safari, “…sasa hivi safari mpaka nikupe ruhusa. Hivi ndivyo fedha za wananchi zilivyokuwa zikichezewa.”
Amesema kwamba, hivi sasa fedha za kununulia dawa zimeongezeka ambapo serikali imeongeza fedha za kununulia vitanda hospitalini pamoja na vifaa vya maabara kwenye shule za serikali.