Macho ni taa ya mwili ambayo humsaidia mwanadamu kuona vitu na kuhakikisha anakuwa salama wakati wote. Lakini macho kama viungo vingine hupata hitilafu na kushindwa kutimiza wajibu wake kwa ukamilifu.
Leo tunazungumzia ugonjwa wa macho mekundu ambao husababishwa na tabaka la juu la jicho ambalo kwa kawaida ni jeupe lakini mara kadhaa watu wanashuhudia tabaka hilo hubadilika rangi na kuwa nyekundu.
Hali hiyo ikitokea jicho huvimba na mtu hushindwa kuona vizuri na wakati mwingine husikia maumivu yanayoambatana na machozi. Hata hivyo, ukubwa wa tatizo hutofautiana kutoka mtu mmoja kwenda mwingine kutokana na kisababishi kinachoyafanya macho yawe mekundu.
“Mara nyingi macho hubadilika na kuwa mekundu kwasababu mishipa ya damu iliyopo tabaka la macho inatanuka au kuvimba”, amefafanua Dk. Jessica Lee, Daktari wa macho katika hospitali ya New York Eye and Ear Infirmary iliyopo karibu na Mlima Sinai nchini Marekani. “Na kuna sababu nyingi ambazo zinaweza kusababisha”.
Sio rahisi kutambua sababu zinazosababisha macho yawe mekundu na nini unatakiwa kufanya ili urejee katika hali ya kawaida. Baadhi ya watafiti wanabainisha baadhi ya tabia na mambo ambayo mtu akiyafanya yanaweza kuwa chanzo cha mtu kuwa na macho mekundu.
Unywaji pombe kupita kawaida
Ikiwa kuna siku umewahi kunywa pombe kupita kawaida utakuwa shahidi kwamba muda mfupi au siku iliyofuata baada ya pombe kuisha mwilini ulijikuta macho yako yakiwa mekundu na yamevimba.
Dr. Lee anasema pombe inasababisha mishipa midogo midogo iliyopo kwenye macho kutanuka na damu nyingi inapita katika mishipa hiyo, “Kadri unavyo kunywa sana pombe, ndivyo wekundu unatokea kwenye macho yako na kuondoa rangi nyeupe”.
Anasema dawa ya maji (eye drops) inaweza kukusaidia kupunguza wekundu kwenye macho na kurejea katika hali ya kawaida. Muhimu usinywe pombe kupita kawaida zinaweza kuleta madhara makubwa zaidi kwenye macho.
Kutopata usingi wa kutosha na uhakika
Macho yaliyochoka yana tabia ya kubadilika na kuwa mekundu. Na hiyo ndio sababu kuwa ukikosa usingizi unapunguza hewa ya oksijeni kwenye macho, jambo linalosababisha mishipa ya damu kutanuka zaidi ili kuruhusu hewa ipite kwenye macho.
“Ikiwa macho yako yatakuwa wazi kwa muda mrefu kwasababu ya kukosa usingizi inazuia tabaka la jicho lako (cornea) lisilainishwe na hii inaweza kusababisha ukavu na wekundu kwenye macho”, amesema Dk. Lee. “Njia nzuri ni kupata usingizi wa kutosha na kutumia dawa ya maji (eye drops) kulainisha macho”.
Matumizi ya lensi
Wapo baadhi ya watu wanatumia lensi za bandia kwa ajili kuongeza uoni. Lensi hizi zinaweza kuzuia hewa ya oksijeni kufika kwenye macho, na kusababisha wekundu na kutanuka mishipa ya damu, amesema Dk. Lee. “Ikiwa lensi hizi zitavaliwa muda mrefu au wakati umelala zinaweza kusababisha wekundu, maambukizi na vidonda kwenye tabaka la jicho”.
Muhimu zingatia matumizi mazuri ya lensi, safisha kwa wakati, zingatia usafi wa macho na zitoe kabla ya kulala. Lakini unaweza kutumia dawa ya maji kulainisha macho yako.
Kupasuka kwa mishipa ya damu
Kupasuka kwa mishipa ya damu kitaalamu kunajulikana kama ‘subconjunctival hemorrhage’ ambapo hutokea pale ambapo mishipa ya damu iliyopo kwenye tabaka la jicho kupasuka. Damu inaganda na kutengeneza michiri kwenye sehemu nyeupe ya jicho.
Ni jeraha la kawaida ingawa linaweza kuogopesha lakini haliwezi kuathiri uoni au maumivu na kuvimba. Hali hiyo hutokea kama umetumia nguvu nyingi, labda ukiwa kwenye mazoezi au kunyanyua kitu kizito hata kupiga chafya na kukohoa kwa nguvu. Rangi hiyo nyekundu hutanda kwenye jicho na inaweza kuondoka yenyewe ndani ya wiki moja.
Glaucoma/Glakoma
Glaucoma husababishwa na kutanuka kwa lensi ya jicho ambapo huathiri mishipa inayounganisha jicho na ubongo, na mara nyingi hutengeneza ukungu kwenye macho. Dalili ya kwanza inayojitokeza ni wekundu kwenye macho ikufuatia na kushindwa kuona vizuri, kuvimba na maumivu kwenye macho.
Glaucoma inaweza kusababisha upofu, ni muhimu kumuona mtaalamu wa macho ili akufanyie uchunguzi. Kwa kawaida glaucoma huanza kidogo kidogo, na ikiwa utapata wekundu, matatizo ya kuona vizuri na maumivu ya kichwa, inaweza kuwa tatizo kubwa linalohitaji kutatuliwa haraka.
Hata hivyo, ni muhimu kufanya uchunguzi ikiwa unahisi hali isiyo ya kawaida kwenye macho ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuyakinga macho yako dhidi ya hatari yoyote inayoweza kutokea.
Macho kama yanawasha na kuona umawingu tiba yake naomba msaada