Ili kukuza pato la ndani la Taifa (GDP), Serikali imeshauriwa kutengeneza mfumo wa kulinda viwanda vya ndani kwa kudhibiti bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi ili kuboresha huduma za kijamii na kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati ifikapo 2025.
Inaelezwa kuwa bidhaa za viwanda kutoka nje ya nchi zinaingia kwa wingi nchini, lakini hakuna mfumo thabiti wa kusimamia uingizaji wa bidhaa hizo hali ambayo inadhoofisha nguvu ya viwanda vya ndani kushindana kibiashara.
Bidhaa kutoka nje huuzwa kwa bei rahisi ikilinganishwa na bidhaa za ndani ambazo huuzwa kwa bei kubwa ili kufidia gharama za uzalishaji na ongezeko la kodi ambalo limejitokeza katika serikali ya awamu ya tano.
Kulingana na taarifa ya Idara ya Forodha ya China (2016) inaeleza kuwa katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka 2016, Tanzania iliagiza Betri zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 36.5 kutoka China. Lakini takwimu za Idara ya Forodha za Tanzania kwa kipindi hicho zinaonyesha kuwa betri zilizoingia nchini kupitia ukaguzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) zilikuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 5.3 tu.
Tafsiri yake ni kuwa betri nyingi zinaingia nchini kupitia njia zisizo halali ambapo zinaikosesha serikali mapato ya kodi na kuathiri ushindani wa kibiashara ya viwanda vya ndani. Kwa muda mrefu sasa Tanzania imekuwa na viwanda vinavyotengeneza betri kikiwemo kiwanda cha Sony lakini ukuaji wake ni mdogo na kwa sehemu kubwa vinajiendesha kwa hasara kutokana na gharama kubwa za uzalishaji.
Shirika la The Observatory of Economic Complexity (OEC) linaloangazia usafirishaji wa bidhaa duniani katika ripoti yake ya mwaka 2016 inaonyesha kuwa China iliingiza bidha za viwandani zenye thamani Dola bilioni 3.49 nchini Tanzania ambapo ni mara mbili ya bidhaa za Tanzania zilizosafirishwa nje ya nchi.
Bidhaa zilizoingia kwa wingi kutoka China ni viatu kwa asilimia 5.8, Simu za mkononi (4.9%), nguo (4.1%), betri (1.8%). Bidhaa zingine ni vifaa vya ujenzi, magari, vifaa vya muziki na vitanda vya wagonjwa.
Hali hiyo imeathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji na soko la bidhaa za Tanzania zinazosafirishwa nje ya nchi ikizingatiwa kuwa bidhaa nyingi zinaingia nchini kwa njia zisizo halali. Udhibiti wa serikali ni mdogo kutokana na teknolojia duni inayotumika kupima ubora wa bidhaa zinazoingia nchini.
Hata hivyo, ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (Machi 2016) zinaonyesha kuwa mauzo ya bidhaa za viwandani nje ya nchi yamepungua kutoka Dola bilioni 1.4 mwezi Machi 2016 hadi kufikia Dola milioni 0.9 mwezi Machi 2017. Anguko hilo la bidhaa ni zaidi ya Dola milioni 500 ambazo nchi imepoteza ndani ya mwaka mmoja.
Tafsiri rahisi ya kiuchumi ni kuwa viwanda vya ndani havijaimarika katika udhalishaji na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi, hali ambayo inatishia anguko la uchumi na ajira za wananchi ambao wameajiriwa katika sekta ya viwanda. Ripoti hiyo ya BOT inaeleza kuwa mauzo ya bidhaa za viwandani nje ya nchi yanashika nafasi ya pili kuliingizia taifa mapato (GDP) baada ya sekta ya utalii ambayo inachangia asilimia 17 ya pato lote la taifa, Mauzo hayo yako mbele ya mauzo ya dhahabu ambayo yanashika nafasi ya tatu.
Kutokana na kupungua kwa uzalishaji na ongezeko la kodi, kampuni mbalimbali zinalazimika kupunguza idadi ya wafanyakazi ili kuepuka hasara za kiuchumi. Mwazoni mwa mwaka huu Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambayo ni mlipa kodi mkubwa iliwaondoa wafanyakazi 100 wa idara ya masoko kutokana na kushuka kwa uzalishaji na soko la bia ndani na nje ya nchi.
Maoni ya Wataalamu wa Uchumi
Mbunge wa Kigoma Mjini na Mtaalamu wa Uchumi, Zitto Kabwe akiongea katika bunge mwaka huu alisema, “kwasababu bidhaa za viwanda zinazouzwa nje zinapopungua maana yake ni kwamba viwanda vyetu vya ndani vimepunguza uzalishaji, kuna watu wamepoteza kazi, kuna mapato ya serikali ambayo yamepotea”, ameongeza kuwa hali hiyo inasababishwa na udhaifu wa serikali kushindwa kulinda viwanda vya ndani na kuruhusu bidhaa za nje kuingia nchi bila kudhibitiwa.
“Uwezo wetu wa kulinda viwanda vyetu umekuwa ni mdogo sana, watu wanaingiza nguo, mafuta ya kula, betri kinyemela katika nchi yetu zinakuwa na bei ndogo matokeo yake ni kwamba viwanda vya ndani vinashindwa kushindana nao katika soko na tunapoteza ajira”, alisema Zitto.
Hata hivyo, ameitaka serikali kutumia rasilimali za ndani na kuacha kuagiza kutoka nje ili kuchochea ukuaji wa viwanda vya ndani. Pia kuimarisha miundombinu ya usafiri wa reli na bandari kwa kurekebisha mfumo wa ukusanyaji kodi ili kuwapa nafuu wawekezaji katika sekta ya viwanda kuzalisha bidhaa nyingi.