SERIKALI imeanza kuushughulikia mgogoro wa ardhi kati ya mwekezaji wa lililokuwa Shamba la Mpunga la NAFCO na wananchi wa kijiji cha Kapunga wilayani Mbarali, imefahamika.
Hatua hiyo imekuja baada ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kumtuma mmoja wa wakurugenzi wake kutoka makao makuu, Paulo Tarimo, aliyekwenda kufuatilia mgogoro huo uliodumu kwa miaka sita sasa.
Mgogoro huo ulioanza mwaka 2006 baada ya Tume ya Taifa ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) kumkabidhi mwekezaji – Kampuni ya Export Trading Limited – lililokuwa shamba la NAFCO, umeaacha majeraha mengi kwa wananchi wa maeneo hayo baada ya kubainika kwamba hata kijiji cha Kapunga kimo kwenye eneo la mwekezaji.
Mbali ya kijiji hicho kudaiwa kuwa kwenye eneo la mwekezaji, lakini huduma nyingine za kijamii kama shule na zahanati nazo ziko kwenye eneo hilo ambapo mwekezaji huyo anadaiwa kuwafukuza walimu kwenye nyumba zilizokuwa za NAFCO, hivyo kuwafanya watembee umbali wa kilometa 52 kila siku kwenda na kurudi shule.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Kapunga, mwenyekiti wa kijiji hicho Ramadhan Nyoni, alisema kwamba Tarimo, aliyekwenda kumwakilisha waziri, alikutana na mwekezaji na wanakijiji kwa nyakati tofauti na kuzungumzia jinsi serikali inavyotaka kulimaliza tatizo hilo.
“Katika kikao chetu (Tarimo) amekiri kwamba taarifa za mgogoro huo zimeichanganya serikali kwani imebainika kwamba eneo lililotangazwa kuuzwa ni tofauti na lile ambalo mwekezaji alikabidhiwa, na ameahidi kuwa suala hilo litashughulikiwa,” alisema Nyoni.
Ujio wa mkurugenzi huyo wa wizara unafuatia vikao viwili vilivyofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Cosmas Kayombo, pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, kati ya Desemba Mosi na 3, 2011 ambao waliahidi kulipeleka suala hilo ngazi za juu ili lipatiwe utatuzi.
Taarifa kutoka Kapunga zinaeleza kwamba, tangu kuwasili kwa viongozi wa serikali, walau hali imetulia kidogo baada ya mwekezaji – kampuni ya ubia inayoendesha shamba hilo ya Kapunga Rice Project Limited – kufungua njia za wananchi kupita na kwenda mashambani baada ya kuzifunga kwa miezi minne.
“Sasa tunaweza kwenda shambani japokuwa mwekezaji amegoma kuruhusu kupita na magari. Hali ingekuwa mbaya kama tungelazimishwa kuzunguka umbali wa kilometa 28 kwenda na kurudi kama mwekezaji alivyotaka,” anasema Emmanuel Kasekwa, abaye shamba lake eneo la Mpunga Mmoja, upande wa pili wa shamba la mwekezaji.
Shamba hilo la Mpunga Kapunga lenye ukubwa wa hekta 5,500 liliuzwa kwa Export Trading Company Limited bought kwa Shs. 2.311 bilioni mwaka 2006, lakini kampuni hiyo ikadai kwamba eneo ililokabidhiwa ni hekta 7,370 kwa mujibu wa hati ya ardhi namba 6249-MBYLR.
Hata hivyo, hati hiyo iliyokuwa ya Mradi wa Mpunga Kapunga (KRIP) inahusisha shamba la wakulima wadogo lenye ukubwa wa hekta 800, shamba la NAFCO la hekta 5,500 zilizotangazwa kuuzwa pamoja na eneo la kijiji lenye ukubwa wa hekta 1,070, jambo lililowashtua wananchi wa eneo hilo ambao ndio walioipatia NAFCO shamba mwaka 1985.
Wachunguzi wa masuala ya haki za ardhi wanasema kulikuwa na ufisadi katika uuzwaji wa shamba hilo kwani tangazo la Serikali lililotolewa na PSRC na kuchapishwa na gazeti la The Guardian Julai 12, 2004 lilieleza kuwa eneo lililokuwa linauzwa na hekta 5,500 ambalo ndilo mwekezaji alilojitokeza kununua.
“Lakini nyaraka za uuzaji zinaeleza kwamba eneo lililouzwa ni hekta 7,370. Hizi zilizoongezeka zilitoka wapi na zilitangazwa lini?” anahoji William Mwamalanga, mkurugenzi wa Taasisi ya Mazingira na Haki za Binadamu mkoani Mbeya (MRECA).
Mwekezaji anatakiwa kufukuzwa awaachie wananchi ardhi yao. Tangu aingie ameonyesha hana nia ya kuwekeza ila kutwaa ardhi ya wananchi. Wananchi hawashindwi kulima mpunga, kinachotakiwa ni sera nzuri ya kilimo na sio kuwarudisha wananchi kwenye ukuloni. Ikiwa serikali haitamwondoa mwekezaji huyu anayetaka kuwageuza wananchi manamba basi wananchi wamwondoe wao wenyeshe. Hayo ndiyo mapinduzi, sio kuimba tu “Nambari wani eeeeh’