Serikali ya Tanzania inakusudia kuingia makubaliano na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kufadhili mradi wa kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya chakula ili kuinua kipato cha wakulima na ukuaji wa viwanda nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Shaaban, ameyasema hayo katika mazungumzo na Meneja wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Maendeleo ya Miundombinu Vijijiji, Bw. Olagoke Oladapa, kwenye Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika- AfDB unaoendelea Jijini Busan- Jamhuri ya Korea Kusini.
Amesema kuwa mwanzoni mwa mwezi Mei, 2018, AfDB ilituma timu ya wataalam nchini Tanzania kufanya mazungumzo ya awali na Serikali kuhusu utekelezaji wa mradi huo ambao utawaunganisha wakulima na teknolojia ya kisasa na soko la uhakika la mazao yao.
“Serikali imefurahishwa na utayari wa AfDB kufadhili mradi huo kwani utachangia ukuaji wa uchumi na kuleta maendeleo katika sekta ya viwanda na kilimo nchini Tanzania” amesema Shaaban
Utekelezwaji wa mradi wa kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya chakula utanufaisha watu wa kipato cha chini kwa kuwa sekta ya kilimo Tanzania inachukua nafasi kubwa katika kuinua uchumi wa nchi.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu, aliahidi kuwa Serikali itaharakisha ukamilishaji wa taratibu za maandalizi ya awali ya mradi huo ili kuwaondolewa wakulima changamoto za kifedha.
Kwa upande wake, Rais wa AfDB, Dkt. Akinumwi Adesina, akizungumza katika jukwaa la uchumi nchini Korea ya Kusini, amesema ili wakulima wafaidike ni lazima uwekezaji huo uunganishwe na sera ya viwanda inayoweza kutumia mazao ya wakulima kutengeneza bidhaa mbalimbali zitakazouzwa nje ya nchi.
Pia amewataka Magavana wa nchi za Afrika kuzisaidia nchi zao kutatua changamoto za kiuchumi ili kuendana na mapinduzi makubwa yanayotokea kote Duniani kwa kuhamasisha ukuaji wa viwanda.
Mkutano wa 6 wa jukwaa la ushirikiano kati ya Jamhuri ya Korea Kusini na Nchi za Afrika unalenga kujadili namna bora ya kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda katika Nchi za Afrika.
Wadau wa Mkutano huo uliofunguliwa na Makamu wa Waziri Mkuu wa Korea Kusini, Kim Dog – Yeon, wamezitaka nchi za Afrika kuhakikisha zinafanya mapinduzi ya kiuchumi kwa kuwekeza kwenye miundombinu na kilimo ili kuchochea ukuaji wa viwanda vya ndani.
Minyororo ya thamani inavyofanya kazi
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Thomas Samkyi amesema kukosekana kwa masoko ya mazao ya kilimo ni changamoto nyingine inayorudisha nyuma maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Katika kutekeleza majukumu ya Benki hiyo, serikali imeanza kutoa huduma kwa kulenga minyororo michache ya ongezeko la thamani katika kilimo cha mahindi kwa kutoa mikopo ya ununuzi wa pembejeo, vifaa na vifungashio vya kisasa vya kuhifadhia mahindi na teknolojia ya uhifadhi wa mahindi ili kukidhi mahitaji ya soko la kimataifa.
“Kwa sasa tumejikita katika mnyororo mzima wa uongezaji wa thamani kuanzia uandaaji wa shambani hadi kwa upatikanaji wa masoko, ikiwemo mahitaji ya uzalishaji wenye tija kwenye sekta nzima ya kilimo kuanzia hatua za awali za utayarishaji wa mashamba.
“Kupima ubora wa udongo na virutubisho vinavyohitajika kwenye uzalishaji wa mahindi, upatikanaji wa pembejeo za kilimo zikiwemo mbegu bora, mbolea, madawa na vifaa na teknolojia mbali mbali za umwagiliaji na fedha kwa ajili ya kulipia gharama mbalimbali za uzalishaji wa mahindi,” amesema.
Samky amesema usaidizi utakaotolewa kwa wakulima itakuwa kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu katika kuimarisha minyororo ya thamani katika kilimo
“Inajumuisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na mitambo ya umwagiliaji, uchimbaji wa visima vya maji ya umwagiliaji, ujenzi wa mabawa ya uvunaji maji ya mvua, ujenzi wa maghala bora ya kuhifadhia mahindi na ujenzi wa miundombinu ya masoko,” amesema.