Taarifa za Umma bado ni siri, vyombo vya habari kitanzini

Jamii Africa
Serikali kupitia Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe imesema kuwa mchakato wa vazi la taifa ulisitishwa na ikaamuliwa Watanzania waachwe waamue wenyewe wanataka kuvaa nini. - Aidha, Waziri Mwakyembe akihojiwa na kipindi cha #NjooTuongee kinachoandaliwa na @twaweza.nisisi kwa kushirikiana na @jamiiforums alisema Wananchi wanayo fursa ya kuomba mchakato uanze upya kama wataona inafaa. - Waziri Mwakyembe akatolea mfano wa vazi la Kaunda Suti kwa Wanaume kuwa kwa sasa linapendelewa zaidi hivyo Wanawake na wao wanaweza kuamua wachague mtindo upi wa vazi lenye staha watakalokuwa wanavaa. #Informed | #Engaged | #Entertained | #JFLeo | #NjooTuongee

Kupata taarifa ni haki ya kila raia wa Tanzania lakini haki hiyo bado haitekelezwi ipasavyo katika baadhi ya taasisi za kiserikali kutokana na urasimu wa upatikanaji wa taarifa hizo. Kimsingi Haki ya kupata taarifa inatambulika na Katiba ya nchi pamoja mikataba ya kimataifa ambayo nchi yetu imeridhia.

Licha ya ofisi za Umma kuwa sehemu muhimu kupata taarifa, lakini vyombo vya habari ndio njia rahisi nay a haraka ambayo mwananchi anaweza kupata taarifa muhimu za taifa. Ili taarifa imfikie mwananchi lazima uhuru wa vyombo vya habari uzingatiwe na kupewa nafasi ya kutosha katika jamii.

Pia ulinzi wa waandishi ambao wanahusika kutafuta na kutoa taarifa nao ni muhimu, lakini katika siku za hivi karibuni ulinzi na vyombo vya habari unatishiwa na baadhi ya watu katika jamii ambao hawapendi taarifa muhimu ziwafikie wananchi.

 

Kauli ya Waziri wa Habari

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza katika kipindi cha runinga ambacho huandaliwa na Twaweza kwa kushirikiana na JamiiForums, amesema ili kulinda Uhuru wa Vyombo Vya Habari nchini wataendelea kushirikiana na vyombo hivyo ili kujadili mambo ya msingi yanayohusu maslahi yao. Pia amesema jukumu la kuwalinda waandishi wa habari wakati wanatekeleza majukumu yao sio la serikali.

Tutakuwa Wizara yenye uwezo mkubwa kama tutakuwa tunajua waandishi kila asubuhi wako wapi, kwanza watashangaa kwa nini tunawafuatilia. Ni wajibu wao kujichunga na kutoa taarifa”

Amewataka waandishi wa habari kushirikiana na serikali ili kukuza uhuru wa kujieleza na kutoa maoni nchini ambapo amesema, “Wanahabari wajifunze kuwasiliana kwa karibu na Wizara yao. Wizara yangu iko wazi saa 24”,

Akizungumzia kufungiwa magazeti amesema hatua hiyo ni kulinda maadili ya vyombo vya habari na kuiepusha jamii na upotoshaji wa habari, “Watanzania wanachanganya maji na mafuta, hakuna gazeti lililofungiwa bila ya kuonywa mara nyingi”.

Kuhusu suala la kurusha matangazo ya Bunge moja kwa moja bado amesema linaendelea kwa baadhi ya vipindi maalumu vya maswali na majibu na hasa kama kuna jambo muhimu la kuwajulisha wananchi. Serikali ya awamu ya tano imekuja na sera mpya ya kubana matumizi ili fedha zielekezwe katika maeneo muhimu ya maendeleo.

Matangazo ya Bunge yako live haswa kipindi cha maswali na majibu. Serikali ya awamu ya tano imekuja na mkakati wa kubana matumizi. Kama kuna taasisi yoyote inataka kulipia Bunge liweze kwenda live wanakaribishwa kuwasilisha ‘proposal’ kwa Waziri wa Habari kuomba rasmi kugharamia matangazo” 

Anasema Uhuru wa kupata taarifa bado upo nchini ikizingatiwa kuwa mitandao ya kijamii haijakatazwa kurusha matangazo ya Bunge kwasababu ni njia rahisi ya kupata taarifa.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akihojiwa Maria Sarungi katika kipindi cha Njoo Tuongee.

 

Takwimu za ripoti ya Twaweza.

Kulingana na ripoti ya Uchunguzi ya Shirika la Twaweza (2017) juu ya Sauti za Wananchi kuhusu kupata taarifa zinazohusu utendaji wa ofisi za umma imebainika kuwa kuna urasimu wa kupata taarifa hizo huku katika ofisi nyingine taarifa za umma huchuliwa kama siri za serikali.

Kutokana na wananchi wengi kutotambua kuwa wana haki kisheria kupata taarifa muhimu za viongozi waliowaweka katika ofisi za umma, wamejikuta wakikosa taarifa muhimu za maendeleo ya jamii.

Uchunguzi huo ambao ulihusisha wananchi 131 katika Halmashauri 26 za Tanzania Bara, ni wananchi 43 sawa na asilimia 33 ndio walipata taarifa katika ofisi za Halmashauri huku wananchi88 (67%) hawakupata taarifa kabisa.

Idara nyingine katika Serikali za Mitaa ni idara ya elimu ambapo wananchi 16 na wananchi 14 hawakupata taarifa walizozihitaji katika idara hizo. Lakini idara ya ujenzi ndio iliweza kwa asilimia 48 kuwapatia wananchi taarifa ikilinganishwa na idara nyingine ambazo zina urasimu wa kupata taarifa.

Kutokana na hali halisi ya upatikanaji wa taarifa katika ofisi za Umma, wananchi wamekuwa na maoni tofauti juu ya mmiliki wa taarifa za ofisi za serikali ambazo zina mahusiano ya moja kwa moja katika utoaji wa huduma za kijamii.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia 70 ya wananchi waliohojiwa mwaka huu wanasema taarifa zinazomilikiwa na mamlaka za Umma ni rasilimali za Umma na mwenye dhamana ya kuzitumia ni mwananchi wa kawaida ambaye analipa kodi.

Kiu ya Wananchi kupata taarifa za serikali

Chanzo: Twaweza-Sauti za Wananchi

Lakini haki ya wananchi kupata taarifa haiishii katika ofisi za umma lakini hata katika mazingira yanayomzunguka ili afahamu kinachoendelea na kujihakikishia usalama wa maisha yake.

Nguzo nyingine ambayo wananchi wamekuwa wakiitumia kupata taarifa ni vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Kwa nafasi yake vyombo hivi vimefanya kazi nzuri ya kuhabarisha na kuelimisha wananchi mambo muhimu yanayogusa maisha yao.

Lakini Vyombo vya Habari vinakabiliwa na tishio la baadhi ya watu katika jamii ambao hawataki taarifa muhimu ziwafikie wananchi. Kutokana na hali hiyo baadhi ya Waandishi wamekuwa wakipewa vitisho na kuwekwa vizuizini.

Pia katika kipindi cha hivi karibuni tumeshuhudia magazeti yakifungiwa kwa kile kinachodaiwa kuwa magazeti hayo yanaandika habari za uongo ambazo zinalenga kupotosha na kuchochea ubaya ndani ya umma. Mpaka sasa magazeti yaliyofungiwa katika awamu ya tano ya uongozi ni Tanzania Daima, MwanaHalisi, Mawio, Raia Mwema na Mseto.

Kupande mwingine, vyombo hivyo vya habari vinatekeleza wajibu wao wa kuongea ukweli ambao kwa namna moja au nyingine hauwapendezi baadhiya viongozi katika jamii.

Baadhi ya runinga na radio nazo zimekuwa zikipewa maonyo ya mara kwa mara ili kuziweka katika mstari unaotakiwa. Hali hiyo imeelezwa kuwa inahatarisha uhuru wa vyombo vya habari na haki ya wananchi kupata taarifa.

Matangazo ya Bunge ambayo yalikuwa yanarushwa na runinga yalisimamishwa kutokana na serikali kuja na sera mpya ya kubana matumizi. Fursa hiyo inatajwa kuminya haki yawananchi kufahamu mambo yanayojadiliwa na wawakilishi wao wakiwa bungeni.

Ripoti ya Shirika la Freedom Haouse (2017) linaloangazia Haki ya kupata Taarifa na Uhuru wa Kujieleza inaiweka Tanzania miongoni mwa nchi za Afrika ambazo uhuru wa vyombo vya habari umeshuka ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki kama Kenya ambayo uhuru unaonekana kuimarika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Twaweza, Aidan Eyakuze anasema upatikanaji wa taarifa katika ofisi za serikali bado ni changamoto kubwa japo zinapatikana lakini sio kwa kiwango cha kuridhisha. Pia huathiri haki ya wananchi kupata taarifa kupitia vyombo vya habari.

1 Comment
  • tanzania hatujawa na uruhuru wa habari bado nivyema wizara husika kufanyia kazi juu ya hili swala wakishirikiana na watanzania kwa ujumla 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *