Ucheleweshaji wa miradi ya maji unavyowagharimu wananchi vijijini

Jamii Africa
Wananchi wakiteka maji. Wananchi wengi hususan wa vijijini wanakabiliwa na uhaba wa maji safi na salama. Picha kwa hisani ya Water Aid.

Baadhi ya wananchi wa vijijini nchini huenda wakasubiri kwa muda kupata maji ya uhakika baada ya Serikali kushindwa kufanikisha ujenzi wa zaidi ya nusu ya vituo vya huduma hiyo muhimu katika maisha ya mwanadamu.

Takwimu zilizopo katika ripoti ya maendeleo ya sekta ya maji mwaka 2016, zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2010/11 na mwaka 2015/16, Serikali ilipanga kujenga jumla ya vituo vya maji 99,515 lakini ilishia kujenga vituo 42,718 pekee.

Vituo hivyo vilivyojengwa ni asilimia 43 tu ya malengo jambo ambalo linaloonyesha kuwa idadi kubwa ya wananchi waliotakiwa kupata huduma hiyo wameshindwa kupata kwa wakati.

Hali hiyo siyo bahati mbaya. Ripoti hiyo iliyotolewa Oktoba mwaka jana inaeleza kuwa theluthi ya miradi hiyo ya maji haikutekelezwa ndani ya awamu ya kwanza ya mpango wa maendeleo ya sekta ya maji (WSDPI) jambo lilofanya baadhi ya vituo vya maji vichelewe kujengwa.

“Hadi Juni 2016, jumla 1,210 kati ya 1,810 iliyopangwa ilikuwa imetekelezwa na kusambaza maji kwa wananchi. Miradi mingine 374 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji katika mwaka huu wa fedha wa 2016/17,” inasomeka sehemu ya ripoti.

Kwa mujibu wa wizara ya maji na umwagiliaji, utekelezaji wa miradi hiyo ilikwama kutokana na sababu mbalimbali yakiwemo masuala ya kifedha.

Wizara hiyo imeeleza kuwa ugawaji wa fedha kwa halmashauri ulizingatia kanuni maalum badala ya mahitaji halisi ya mamlaka zilizotakiwa kuitekeleza na kuzisababishia kushindwa kupata kiwango kinachotakiwa kufanikisha miradi.

Mbali na matatizo katika mgawanyo, pia hakukuwa na fedha za kutosha kugharamia miradi hiyo.

“Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ulikuja na miradi ambayo haikuwa na fedha za kuitekeleza,” inasema ripoti hiyo iliyochambuliwa na Fikra Pevu.

Hata wakati kukiwa na matatizo, ripoti hiyo inaeleza kuwa baadhi ya halmashauri hazikuweka miradi ya maji kama kipaumbele huku usimamizi wake ukilegalega.

Pamoja na kutofikiwa kwa malengo hayo, bado vituo hivyo vimekuwa vikiongezeka mwaka hadi mwaka kutoka Julai 2007 japo si kwa kasi na malengo yaliyotarajiwa.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa vituo vya maji viliongezeka kutoka 2,603 mwaka 2017/08 hadi kufikia 50,995 na kuwanufaisha wananchi milioni 11.6.  

Kwa pamoja, ripoti hiyo inabainisha kuwa hadi mwaka jana,  Serikali imefanikiwa kujenga vituo vya maji  95,733 vinavyowahudumia wananchi 22.79 milioni waishio vijijini Tanzania bara ikiwa ni takriban robo tatu (asilimia 72) ya watu wote wanaoishi katika maeneo hayo kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012.

Kiwango cha wananchi wanaopata maji vijijini kimekuwa mwenendo mseto. Kimekuwa kikipanda na kushuka kutoka mwaka 2005. Kiwango cha juu kufikiwa ni mwaka jana hasa baada ya kuporomoka hadi asilimia 49 mwaka 2013 ikilinganishwa na asilimia 54.7  wakati Rais Jakaya Kikwete anaingia madarakani.

Katibu Mtendaji wa Chama cha Wasambazaji Maji Tanzania (Atawas), Martha Kabuzya anasema mikakati wanayotumia kusambaza maji kwa sasa ni ile iliyopo katika mpango wa maendeleo ya maji.

Anasema kuwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, idadi ya watu wanaopata maji imeongezeka na kwamba wananchi wengi wa mijini wanatumia maji yaliyounganishwa majumbani mwao kuliko kwenye vituo vya umma.

“Kwa vijijini vituo vya maji vya umma bado ni muhimu kutokana na mazingira yake lakini watu wengi wa mijini hawavitumii hivyo kwa kuwa wameshaunganishwa na mfumo wa bomba,” anasema Kabuzya ambaye ni mtaalamu wa rasilimali maji.

Atawas  inajumuisha mamlaka za usambazaji maji zote nchini zikiwemo Shirika la Maji Safi na Taka (Dawasco) na mamlaka ya usambazaji safi na taka Morogoro (Moruwasa).

Kuhusu baadhi ya mamlaka za maji kutotosheleza mahitaji, Kabuzya anasema kuwa idadi ya watu imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka ndiyo maana wakati mwingine kiwango cha wanaopata maji kimekuwa kikipanda na kushuka.

Hata hivyo, ucheleweshaji wa fedha za ujenzi ni moja ya changamoto zinazozikabili mamlaka hizo katika jitihada za kuongeza wigo wa usambazaji maji kwa wananchi.

Changamoto nyingine anaitaja kuwa upotevu wa maji ambao unaotokea kutokana na miundombinu kuchakaa au watu wasio waaminifu kuiba maji ili kukwepa kulipia huduma hiyo.

“Kwa sasa fedha za ujenzi wa miradi zinatoka serikali kuu na kazi za mamlaka ni kuendesha mradi na kuufanyia matengenezo. Hii ina maana kadri miradi inavyocheleweshwa ndivyo na sisi tunavyochelewa usambazaji maji kwa wateja wetu ambao ni wananchi,” anasema Kabuzya.

Ukosefu wa maji unazigharimu zaidi familia nyingi hususan akina mama na watoto ambao hulazimika kutembea umbali mrefu kuyasaka hususan maeneo ya vijijini yenye ukame wa maji.

Hellena Longo, mkazi wa Madibira wilayani Mbarali, Mbeya anasema wakati maji ya bomba ya umma iliyowekwa kwenye kitongoji chao cha Tolinyengo yanapokatika hususan wakati wa kiangazi, hulazimika kwenda mtoni kuteka maji. Mto huo uitwao Lyandembela upo takriban kilomita nne kutoka nyumbani kwake.

Hivi karibuni akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Lindi, Rais John Magufuli alikasirishwa na kucheleweshwa kwa mradi wa maji wa Ng’apa baada ya kubaini kuwa umetumia miaka sita kujengwa.

Kutokana na kucheleweshwa huko, Rais alimwagiza Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kumnyang’anya pasi ya kusafiria mkandarasi wa mradi huo hadi hapo atakapoukamilisha.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, mhandisi Mbogo Futakamba anasema kuwa katika awamu ya pili ya mpango wa maendeleo ya sekta ya maji wamejipanga kuondoa mapungufu yaliyojitokeza yakiwemo yakiundeshaji.

Awamu ya kwanza ya mpango huo ilikuwa kati ya mwaka 2006/07 na 2013/2014.

Futakamba ameeleza katika ripoti hiyo iliyotolewa mwishoni mwa mwaka jana kuwa katika awamu hii kuna zaidi ya wakala 300 wa utekelezaji miradi ya maji nchi nzima ili kufanikisha usambazaji wa huduma za maji safi na salama kwa wananchi zaidi milioni 20.

Mipango ya awali ya kutekeleza mpango huo inabainisha kuwa mahitaji ya awali ya kifedha ni Dola za Marekani 3.32 bilioni sawa na Sh7.23 trilioni.

Hadi Oktoba mwaka jana, Futakamba anasema kiwango ambacho kilishakuwa kimeahidiwa kutolewa kilikuwa Dola za Marekani 1.65 bilioni sawa na Sh3.59 trilioni.

“Kuna jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha kuwa fedha zinawafikia watekelezaji wa miradi kurahisi kutoka kwenye chanzo kikuu.  Baadhi ya wadau wa maendeleo wameanzisha mipango ya kifedha ambayo imelenga kuongeza upatikanaji wa maji nchini,” anasema Futakamba.

Awamu ya pili ya mpango wa maendeleo ya maji (WSDP II) ilianza kutekelezwa mwaka 2014/15 na inatarajiwa kukamilika mwaka 2018/19.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *