Tanzania kwa muda mrefu sasa tangu ipate uhuru imekuwa ikipata mikopo na misaada mbalimbali kutoka kwa mataifa ya kibepari ambayo leo tunayaita wahisani wa maendeleo kwa nia ya kulikomboa taifa kutoka katika dimbwi la umasikini.
Tafakuri yangu hii inalenga kuibua mijadala juu ya mikopo na misaada ambayo Tanzania imepata na inaendelea kupata.
Swali la msingi la kutafakari hapa je, misaada na mikopo ambayo nchi yetu imekuwa ikipata tangu uhuru imelikomboa taifa letu kutoka katika dimbwi la umasikini?
Katika swali hili ni ukweli ulio wazi kwamba misaada na mikopo ambayo nchi yetu imekuwa ikipata na inaendelea kupata haijasaidia kuondoa na haitafanikiwa kuondoa umasikini Tanzania kamwe. Inaweza ikawa kauli isiyofurahisha masikioni mwetu ila ukweli ndivyo ulivyo na inabidi kujitafakari upya na kuona ni nini hasa taifa linahitaji kufanya ili tuweze kujiendeleza wenyewe bila misaada na mikopo.
Hapa kunaweza kuzuka hoja tutafanyaje ili tuweze kuishi bila mikopo na misaada kutoka kwa nchi za kipepari?
Kiuhalisia inaweza ikawa ngumu kuona uwezekano wa hili kwa kuwa tayari tumeshaathirika na utamaduni wa kuishi kwa misaada na mikopo ambayo ni sehemu kubwa ya bajeti ya taifa letu. Utegemezi huu wa hali ya juu unatufanya kama taifa na mtu mmoja mmoja kuona ya kuwa bila misaada na mikopo taifa letu haliwezi kusonga mbele. Ila ni vyema tukafahamu ya kuwa, pale ambapo dhamira ya kweli ya kisiasa itakuwepo itaweka mikakati ya kuanza kujiondoa katika utegemezi huu na kuanza kutumia rasilimali zetu wenyewe.
Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwa Botswana na Afrika ya Kusini ni kwa jinsi gani nchi hizo mbili zimeweza kujiendeleza bila ya kutegemea misaada na mikopo kutoka kwa nchi za kibepari.
Swali la kujiuliza hapa, inakuwaje nchi hizi mbili zimefanikiwa katika vita hii ili hali sisi kama taifa tumeshindwa?
Ukweli ni kwamba Tanzania kama taifa haijawa na nia ya dhati ya kupambana na vita hii ya mikopo na misaada kwa kuwa kama nchi tumeshaathirika na utegemezi uliokithiri kiasi cha kudhani bila misaada na mikopo hatuwezi kusonga mbele. Kwa upande mwingine, misaada na mikopo hii imepelekea kuwapo na ubadhilifu mwingi kwa kuwa baadhi ya viongozi wetu hawapati uchungu na hizo fedha kwani wanajua zimetoka kwa wahisani.
Ni vema tukafahamu ya kuwa, kuendelea kupata misaada na mikopo kutoka kwa nchi wahisani kama tunavyowaita hupelekea kuua ubunifu na fursa za uwekezaji wa ndani kwani wengi wetu tunaacha kujituma tukijua kuna watu wako kwa ajili ya kutuletea maendeleo. Hii inajidhihirisha wazi nchini kwetu ambapo leo tunashughudia msisitizo mkubwa kwa wawekezaji kutoka nje kana kwamba wao ndio mwokozi wa taifa letu kutoka katika dimbwi la umasikini. Msisitizo huu wa wawekezaji kutoka nje ni moja ya sehemu ya misaada na mikopo kutoka kwa mabepari.
Ili kuweza kuachana na misaada na mikopo kutoka kwa nchi wahisani tunapaswa kuwa na mfumo tunaouamini sote kama taifa. Sina hakika leo hii kama taifa tunafuata na kuamini mfumo gani ambao utatutoa katika dimbwi la umasikini. Yamkini tunaendeshwa na sera za vyama ambazo nazo msingi wake haujulikani uko katika mfumo upi unaoongoza nchi.
Katiba yetu ya mwaka 1977 inasisitiza ya kuwa nchi yetu ni ya Ujamaa na Kujitegemea. Ila sina hakika hichi kilichoandikwa kama bado kinaakisi hali ya maisha ya leo. Kama tunaona mfumo huu hautufai kwa nini tusianze mchakato wa kubadili ama kuuboresha mfumo huo? Kwa maoni yangu, kukosa mfumo madhubuti kama taifa kunafanya utegemezi mkubwa wa mikopo na misaada kama nguzo kuu ya maendeleo ya nchi yetu.
Azimio la Arusha (1967) likaenda mbali zaidi na kuuliza je, hata tukipata fedha za kutosha kutoka nje ya nchi za kuweza kukidhi mahitaji yetu yote nchini je, hichi ndicho tunachokihitaji? Azimio la Arusha likazidi kufafanua na kukumbusha zaidi ya kuwa uhuru unamaana kujitegemea, uhuru hauwezi kuwa wa kweli kama taifa litakuwa linategemea zawadi na mikopo kutoka nchi nyingine kwa maendeleo yake. Hata kama kungekuwa na taifa au mataifa ambayo yako tayari kutupatia fedha zote tunazotaka kwa ajili ya maendeleo yetu, isingekuwa sahihi kwa sisi kukubali msaada huo bila kujiuliza wenyewe ya kuwa misaada hii inamadhara gani kwa uhuru wetu na namna tutakavyoishi kama taifa.
Je, tunaweza kuacha uchumi wa nchi yetu mikononi mwa wageni ambao wangerudisha faida wanayoipata kwenda nchini mwao? Ama basi, wakiamua ya kuwa hawatapeleka faida nchini mwao na faida hiyo wangeiwekeza hapa nchini; je, tunaweza kukubali hali hii bila ya kujiuliza ni hasara gani taifa letu litapata? Je, hali hii itaruhusu Ujamaa kama lilivyo lengo letu kuujenga?
Tunawezaje kutegemea zawadi, mikopo, na uwekezaji kutoka nchi za nje na makampuni ya nje bila kuhatarisha uhuru wetu? Waingereza wanamsemo usemao ‘Yule anayemlipa mpiga zumari ndiye huchagua wimbo’. Tunawezaje kutegemea serikali za nje na makampuni yao kwa kuleta maendeleo ya nchi yetu bila ya kuwapa serikali na nchi hizo sehemu kubwa ya uhuru wajifanyie vile wanavyotaka? Ukweli ni kwamba hatuwezi.
Dr. Dambisa Moyo katika kitabu chake cha Dead Aid amesisitiza ya kuwa kamwe Afrika haiwezi kutoka katika dimbwi la umasikini kwa kutegemea misaada na mikopo kutoka kwa wahisani mpaka pale nchi za Afrika zitakapoamua kwa dhati kujiletea maendeleo wao wenyewe.