Mataifa mengi yaliyopiga hatua za maendeleo waliwekeza vilivyo katika tafiti. Tafiti hizo zilitokana na mapato ya ndani ya nchi hizo husika na hazikutokana na misaada ama zawadi kutoka kwenye nchi zingine ambazo zingeweza kuwa na ajenda binafsi.
Taarifa mbalimbali za kiuchumi zinadhihirisha wazi ya kuwa, utafiti umekuwa uti wa mgongo wa mataifa mengi kama vile; China ambayo ndio yenye uchumi wa pili bora duniani ambapo inatumia asilimia 23 ya bajeti yake yote katika kufanya utafiti, South Korea asilimia 18, Japan ni asilimia 16, Marekani asilimia 20, Uingereza asilimia 15 na Ufaransa asilimia 25.
Twakwimu hizo hapo juu zinadhihirisha wazi umuhimu uliowekwa katika eneo la utafiti kama sehemu kuu ya maendeleo katika nchi mbalimbali duniani.
Katika bajeti ya mwaka 2016/2017 ya Tanzania kwa mujibu wa Dk. Philip Mpango, shughuli zilizopewa kipaumbele kwenye mipango ya maendeleo ziligawanywa katika maeneo manne ambayo ni viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu, mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji na pia usimamizi wa utekelezaji wa mpango.
Kwa mtazamo wangu, nadhani ni wazi kabisa utafiti kama kipengele kinachojitegemea kilipaswa kuwa moja ya kipaumbele kikubwa kama tunataka kuwa nchi ya viwanda na hatimaye kuwa na uchumi wa kati.
Ila changamoto hapa ni kwamba, fedha kwa ajili ya utafiti zimerundikwa pamoja na fedha zingine za mipango ya maendeleo katika sekta ya viwanda, kilimo, mifugo, uvuvi na elimu ili hali sekta zingine zimebaki bila kutengewa fedha za utafiti kama vile afya, usafirishaji, nishati na madini, maji, huduma za jamii na demokrasia na utawala bora.
Kutokuwa na ulinganifu katika kugawa fedha za utafiti katika sekta zote kama ilivyoainishwa hapo juu kunafanya maendeleo kuendelea kusuasua. Pia kushindwa kung’amua matatizo hasa ya kutatuliwa na kubaki kutekeleza mambo yaliyotolewa ahadi katika ilani za vyama bila kuwa na twakimu zozote za kisayansi.
Hapa ndipo tunapoona umuhimu wa kuweka kipaumbele cha utafiti katika vipaumbele vya kila mwaka katika bajeti zetu ili ziweze kusaidia sekta zote na taasisi zilizo chini yake katika kuleta maendeleo endelevu kwa kuendelea kubuni mambo mapya yenye tija kutokana na taarifa na takwimu za kisayansi.
Ni wazi kwamba, Tanzania imekuwa ikiendelea kujitahidi katika kufanya tafiti mbalimbali ili kuweza kusaidia sekta mbalimbali ndio maana kumeundwa taasisi mbalimbali zinazosimamia tafiti katika maeneo mengi. Baadhi ya taasisi hizo ni; Taasis ya Utafiti wa Magonjwa ya Wanyama (ADRI), Kituo cha Kukuza Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC), Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Samski Tanzania(TAFIRI) na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).
Wataalamu wa maabara wakiendelea na shughuli zao
Taasisi hizi za serikali zinapaswa kuwa na fedha za kutosha kuweza kufanya tafiti mbalimbali ili kuweza kuchangia na kutoa mapendekezo katika mipango ya maendeleo ya nchi yetu na kuachana na ile miongozo tunayoiazima kutoka Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la IMF kama vile Structural Adjustment Programs (SAPs), Malengo ya Milenia (MDGs) ama huu mpango wa sasa wa Malendo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Mipango yote hii ya maendeleo haina maana kwetu kama taasisi zetu za kitafiti hazitakuwa na nguvu na rasilimali ya kutosha kuweza kufanya tafiti na kuja na mipango ambayo itakuwa dhahiri na mahususi katika mazingira yetu na kuacha hii mipango ya majaribio kutoka nchi za Ulaya na Marekani na kuendelea kutufanya vyombo vya majaribio vya tafiti zao.
Mara nyingi taasisi zetu za utafiti zimekuwa zikipata pesa chache kutoka kwenye bajeti yetu kwa kuwa sio kipaumbele chetu katika sehemu ya maendeleo yetu wenyewe. Taasisi hizi tumeziacha ziendelee kufadhiliwa na nchi za Ulaya katika kufanya tafiti ambapo mara nyingi nchi hizo za Magharibi zimekuwa zikishinikiza aina fulani ya tafiti kutokana na agenda zao binafsi.
Ni dhahiri ya kuwa kama Tanzania inataka kupiga hatua za maendeleo ni vyema ikasimamia mambo yake yenyewe ikiwemo kuhakikisha utafiti unakuwa sehemu muhimu ya kipaumbele na tena kinatengewa fedha na fedha hizo zitokane na mapato ya ndani na sio kusibiri misaada ama sadaka kutoka katika nchi nyingine.
Tafiti zitasaidia kutuletea mipango yetu wenyewe ya maendeleo na kuachana na ile ya kutoka nje ya nchi. Hivi sasa tunahitaji kuwa nchi ya viwanda ila tumeshajua tunataka viwanda vya namna gani na vipi vitatukwamua kwa haraka katika umasikini? Haya ni maswali ambayo yanapaswa kujibiwa na taasisi husika za utafiti Tanzania. Ila naona hatari pale tunapofungulia milango wawekezaji waje kutoka nje kuja kutuletea viwanda watakavyo wao hata kama sie hatuvitaki.
Faida ya kuzipa taasisi zetu nguvu ya kufanya tafiti kwa manufaa yetu kwa mapato ya ndani zitasaidia kuondoa mikanganyiko ya agenda binafsi za wale watoa pesa kutoka Ulaya kwa ajili ya kufanya tafiti zenye maslahi yao binafsi.
Mikanganyiko hi husababisha taifa letu kukosa dira na shabaha ya kile inachokitarajia katika maendeleo kwani tunashindwa kutoa kipaumbele kwa utafiti kwa kutumia wataalamu wetu wenyewe na kusubiri tafiti za wataalamu kutoka nje ambazo huzaa miongozo kandamizi isiyoweza kutekelezeka Tanzania
Nimalize kwa kusisitiza ya kuwa utafiti uwe kipaumbele muhimu katika bajeti zetu kama tunahitaji kufikia maendeleo endelevu kama vile tunavyojinasibu na tuache kutegemea miongozo kutoka nje ya nchi kama sehemu muhimu ya maendeleo yetu.