Daniel Samson
Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi 100 duniani zenye idadi kubwa ya watu ambao wanatumikishwa kwenye shughuli za ‘utumwa wa kisasa’ ambapo hali hiyo inatafsiriwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Kulingana na ripoti ya utafiti iliyotolewa na taasisi ya Global Slavery Index (GSI-2017) imeitaja Tanzania kushika nafsi ya 22 kati ya nchi 167 zenye idadi kubwa ya watu wanaotumikishwa kwenye aina mbalimbali za utumwa wa kisasa (Modern Slavery).
Ripoti hiyo inaelezwa kuwa inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2016, Tanzania ilikuwa na watu 341,400 ambao wanatumikishwa kwenye shughuli mbalimbali ambazo zinakiuka haki za msingi za binadamu. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 0.638 ya wananchi wote waliopo nchini.
‘Utumwa wa kisasa’ unahusisha vitendo vya kulazimishwa kufanya kazi ngumu, kuwaweka watu rehani (bonded labour), usafirishaji watu, utumwa wa watoto, ndoa za kulazimishwa na ndoa za utotoni. Waathirika wakubwa wa utumwa huo ni wanawake na watoto ambao kutokana na hali zao hawawezi kujizuia na matendo maovu yanayofanywa na baadhi ya watu katika jamii.
Tanzania imewekwa nafasi ya 22 kwasababu ya ongezeko la mimba za utotoni na utumikishwaji wa watoto kwenye kazi ngumu za migodini, mashambani na biashara. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania inatajwa kuwa ni nchi ya tatu barani Afrika kwa matukio ya ndoa za utotoni na mimba kwa asilimia 28, ambapo kila mwaka wasichana 8,000 hupata mimba na kukatisha masomo.
Tatizo hilo bado ni kubwa katika nchi za Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watu na Makazi (UNFPA) linaeleza kuwa msichana 1 kati ya 6 mwenye umri wa miaka 15 hadi 19 hupata mimba katika nchi hizo.
Kwa upande wa Afrika Mashariki, Tanzania imeshika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Uganda yenye ‘watumwa’ 244,400 ikishika nafasi ya 30 duniani. Nchi ya 3 ni Kenya (188,800) ikiwa nafasi ya 37 ikifuatiwa na Rwanda (74,100) pamoja na Burundi (71,400).
Nchi zote za Afrika Mashariki zimeingia kwenye nchi 100 zenye idadi kubwa ya watu wanaotumikishwa kwenye utumwa wa kisasa ambapo vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake vimeshika kasi kwenye nchi hizo.
GSI ilifanya utafiti katika nchi 167 duniani kuanzia mwaka 2014 na ilipofika 2017 walitoa ripoti hiyo ambayo inaelezwa kuwa licha ya biashara ya utumwa kukomeshwa Karne ya 19, vitendo vya utumwa vinaendelea kufanyika kwa siri na kwa njia mbalimbali ambapo huathiri ustawi wa binadamu na jamii.
Kuwepo au kutokuwepo kwa utumwa katika nchi husika kunapimwa kwa vigezo 4 ambavyo ni ulinzi wa raia na kisiasa, upatikanaji wa haki za kijamii na kiuchumi, ulinzi binafsi, idadi ya wakimbizi na mapigano ya ndani ya nchi.
Duniani kote zaidi ya watu milioni 45.8 wanatumikishwa kwenye aina mbalimbali za utumwa ambapo asilimia 58 ya utumwa huo unatokea kwenye nchi 5 za China, India, Pakistan, Bangladesh na Uzbekistan. Nchi nyingi zinawatumikisha na kuwalipa wafanyakazi ujira mdogo kwenye mashamba na viwanda vinavyotengeneza bidhaa zinazouzwa nchi za Ulaya, Japan, Amerika ya Kaskazini na Australia.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa nchi zenye kiwango kikubwa cha uwiano wa idadi ya watu walio kwenye utumwa wa kisasa ni Korea Kaskazini, Uzbekistan, Cambodia, India na Qatar. Nchini Korea Kaskazini upo ushahidi wa kweli ambao unaonyesha jinsi serikali inavyowalazimisha watu wake kufanya kazi ngumu kwenye kambi za kijeshi na wale wanaokiuka amri hiyo hufungwa jela.
Pia wanawake wanalazimishwa kuolewa na kuingia kwenye biashara na udhalilishaji wa kingono katika nchi ya China na nchi nyingine za jirani. Serikali ya Uzbekistan kila mwaka inawalazimisha wananchi wake kufanya kazi ya kuvuna pamba kwa ujira mdogo.
Hata hivyo, nchi zilizo na kiwango kidogo kabisa cha idadi ya watu walio utumwani ni Luxembourg, Ireland, Norway, Denmark, Switzerland, Austria, Sweden na Ubelgiji. Nchi zingine ni Marekani, Canada, Australia na New Zealand. Kwa ujumla nchi hizo zina uchumi mzuri, sera na sheria nzuri, kiwango kidogo cha mapigano na uthabiti wa kisiasa ambao unapambana na utumwa wa kisiasa.
Utumwa wa Kisasa nini?
Mtu anahesabika kwamba yuko utumwani ikiwa:
- Kalazimishwa kufanya kazi – kwa nguvu au kwa vitisho vya kiakili na kimwili.
- Kumilikiwa au kusimamiwa na mwajiri kwa kudhalilishwa kiakili, kimwili au vitisho
- Kukosa ubinadamu, kumchukulia, kumuuza au kumnunua mtu kama bidhaa/mali
- Vikwazo vya kutembea ikiwemo kwenda popote kwa kuwekewa vikwazo vya kisiasa au usalama.
Aina za Utumwa wa Kisasa
Shirika la Kimataifa la Kuzuia Utumwa (Anti-Slavery International) linaeleza kuwa makusudi ya unyanyasaji yanatofautiana kutoka udhalilishaji wa kingono na kazi ngumu mpaka ule wa ndoa za utotoni na ukeketaji. Aina za utumwa wa kisasa zimegawanyika katika matabaka mbalimbali:
- Kulazimishwa kufanya kazi – Kazi au huduma yoyote ambayo watu wanalazimishwa kufanya bila hiari yao kwa vitisho au aina fulani ya adhabu.
- Rehani ya madeni au kazi – Ni aina ya utumwa ambayo imeshika kasi duniani ambapo watu waliokopa fedha wakashindwa kulipa wanalazimishwa kufanya kazi ili kufidia madeni . Hupoteza utashi na usimamizi wa hali zao ikiwemo ajira na madeni.
- Usafirishaji watu – Inahusisha kusafirisha, kuajiri au kuwahodhi watu kwa nia ya kuwatesa, kuwadhalilisha, vitisho au kutumia nguvu.
- Utumwa wa Kurithishwa – Inatokea pale ambapo mtu amezaliwa kwenye familia ya watumwa na kwasababu jamaa zake walichukuliwa utumwani na yeye kwa asili anakuwa mtumwa.
- Utumwa wa watoto – Watu wengi wanachanganya utumwa wa watoto na kazi ngumu kwa watoto. Kazi ngumu kwa watoto ni hatari na kikwazo kwa maendeleo ya kielimu lakini utumwa wa watoto unatokea pale mtoto anaponyanyaswa na mtu mwingine ambapo inahusisha kusafirishwa, kuingizwa jeshini, ndoa za utotoni na ukatili unaotokea nyumbani.
- Ndoa za kulazimishwa na utotoni – Inatokea mtu akiolewa bila ridhaa yake na hawezi kutoka kwenye ndoa hiyo. Ndoa za utotoni zinatajwa kuwa ni utumwa kwasababu watoto hawana utashi wa kufanya maamuzi ya kimahusiano.
Hatua zilizochukuliwa
Serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amesema wizara yake imepokea taarifa kuwa wapo watanzania hasa vijana wanaosafirishwa nje ya nchi na kuingia nchini kutumikishwa kwenye shughuli za udhalilishaji na utumwa.
“Tumeona vijana wakiwa wamefungwa miguu juu vichwa chini wamefungwa mikono yote wakitandikwa viboko kwa madai kwamba miongoni mwao kuna aliyewapeleka akiwaambia kwamba twendeni kuna kazi nzuri ya kufanya lakini wakifika kule wanawekwa rehani pale walipo, wanatumikishwa kitumwa na wengine wananyanyaswa kikatili” amesema Waziri Mwigulu na kuongeza kuwa,
“Lakini wapo raia wanaoingia kwa makundi nchini kwetu na wale wanaowaleta wanatumia sababu tofauti wanapowaleta na wanapoingia wanawafanyisha shughuli tofauti na walizoombea vibali”.
Amebainisha kuwa wanachukua hatua za kisheria kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wale wote wanaowatesa na kuwatumikisha watanzania katika shughuli zisizo halali ili kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na kuendelezwa.
“Lakini wanaohusika na shughuli hizi waendelee kutafutwa, wakamatwe wafike kwenye mkono wa sheria ili sheria iweze kufuata mkondo wake”, ameagiza Waziri Nchemba.
Hata hivyo, shirika la Human Rights Watch limeishauri serikali ya Tanzania kupitisha mikakati maalumu kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na kuweka kanuni kali na uangalizi wa uajiri, programu za mafunzo ya haki, na msaada wa kujitosheleza kwa waathirika wa vitendo vya kitumwa vinavyotokea ndani na nje ya nchi.