Tatizo la upofu wa macho linavyoitesa dunia

Jamii Africa

Daniel Samson

Jicho ni kiungo kimojawapo cha mwili kinachomsaidia mwanadamu na pia wanyama kuona vitu mbalimbali vilivyomo dunia.

Matatizo ya macho yapo ya aina mbalimbali: Mengine yanasababishwa na nzi, kama vile trakoma, na mengine yanasababishwa na mionzi ambayo inaweza kuwa ya jua, runinga na hata tarakilishi (kompyuta) ambavyo vinasababisha macho kutofanya kazi vizuri kama kushindwa kuona mbali au karibu.

“Siku moja nikiwa nimelala kitandani baada ya kuamka nikajikuta sioni mpaka leo”

Hayo ni maneno ya Patricia Patrick, mkazi wa Kijitonyama, Dar es salaam ambaye ana ulemavu wa macho (upofu) kwa zaidi ya miaka 15 sasa. Anasema alipata tatizo la kutokuona akiwa darasa la nne ambapo alilazimika kukatisha masomo na kukaa nyumbani muda wote.

Patricia ni miongoni mwa watu wengi duniani ambao wana ulemavu wa kuona kutokana na changamoto mbalimbali walizokutana nazo katika maisha. Anasema kutokuona hakumzuii kufanya shughuli zake za kila siku ambazo humpatia kipato kwa ajili ya familia yake.

Watu wengine huzaliwa wakiwa tayari na ulemavu wa kuona na wengine hukumbana na hali hiyo kutokana na mabadiliko mbalimbali ya kiafya na kijamii.

Tafsiri ya Upofu wa macho

Upofu ni hali ya kutokuona ambayo hutokana na sababu za kifisiolojia au zinazohusiana na mishipa ya neva. Upofu wa macho ni ukosefu wa kuona maumbo, mwanga na kurekodi ikifahamika kama ‘No Right Perception’ (NLP). Hata hivyo neno upofu wa macho hutumika mara nyingi likimaanisha kuharibika kwa macho au kuona kwa taabu

Kwa mujibu ya ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa kila sekunde tano mtu mmoja duniani huwa kipofu na kila mwaka zaidi ya watu milioni 7 hupata matatizo ya macho na kuwa vipofu.

Takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, zinathibitisha kuwa asilimia 1 ya watanzania wote wana upofu, huku asilimia 2.1 wana matatizo ya macho ikiwemo uoni hafifu.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa tatizo la upofu duniani limeongezeka huku nchi za Kusini na Mashariki mwa bara la Asia na zile za Afrika zikiwa na idadi kubwa ya watu wenye upofu.

Kulingana na utafiti wa jarida la Lancet linaloangalia Afya za Watu Duniani linasema upofu umeongezeka kutoka watu milioni 32.4 mwaka 2010 na kufikia watu milioni 36 mwaka 2015 na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia watu milioni 115 ifikapo mwaka 2050 kama tahadhari haitachukuliwa.

Watafiti wanasema ongezeko la idadi hiyo ya watu wenye upofu imechangiwa zaidi na ongezeko la watu wanaokabiliwa na matatizo ya kutokuona vizuri. Utafiti huo unaeleza kuwa mwaka 2010 kulikuwa na watu milioni 191 wenye shida ya kuona vizuri na miaka mitano iliyofuata idadi hiyo iliongezeka na kufikia watu milioni 216.6.

Mtafiti wa ripoti hiyo ya Afya ya Dunia, Rupert Bourne anasema matatizo ya kuona ni changamoto kwa wahusika kwa sababu hupunguza uwezo wa kujitegmea na kufanya shughuli za maendeleo.

“Matatizo ya kuona katika hatua yoyote huwa na madhara makubwa kwa maisha ya mtu hususani katika kupunguza uwezo wao wa kujitegemea katika kufanya shughuli mbalimbali” anaeleza Bourne.

 Zimetajwa sababu tatu ambazo ni kichocheo cha upofu kwa watu wengi; ongezeko la watu wenye umri mkubwa (watu wanaoishi miaka mingi), idadi ya watu duniani na watu wenye matatizo mbalimbali ya macho ambao hawajapata matibabu.

 

Watu ambao wako katika hatari ya kuwa vipofu

Utafiti wa WHO (2014) unaeleza kuwa watu wenye umri zaidi ya miaka 50 ambao kutokana na hali za afya zao wako katika hatari ya kupoteza uwezo wa kuona na mwishowe huwa vipofu. Kundi hili hujumuisha asilimia 82 (watu 8 kati ya 10) ya watu wote wenye upofu duniani.

Pia kundi hili ndilo hukumbwa zaidi na matatizo mbalimbali ya macho ikiwemo kupungua kwa uwezo wa kuona vitu vilivyo mbali na karibu. Kadiri nchi inavyokuwa na idadi kubwa ya watu wenye umri mkubwa ndivyo idadi ya watu wasioona huongezeka katika nchi husika.

Watoto walio chini ya miaka 15 nao wako katika hatari ya kupata ulemavu huo, ambapo watoto milioni 19 wana matatizo ya kutokuona vizuri duniani kote na watoto milioni 1.4 ni vipofu. Matatizo ya macho katika kundi hili husababishwa zaidi na mapungufu ya kuthibiti mwanga kwenye macho ambapo huathiri mboni ya jicho.

 

Mambo muhimu ya kuzingatia kujikinga na upofu

Mtaalamu na Mshauri wa Lishe, Dkt. Abdallah Mandai katika andiko lake la Upofu anashauri mambo muhimu ambayo kila mtu akiyafuata anaweza kujizuia kupata upofu:

  • Usifanye kazi sehemu yenye mwanga mdogo hii itasababisha macho yako kutumia nguvu nyingi sana kuona.
  • Usisome kitu chochote wakati unatembea.
  • Usiangalie moja kwa moja mwanga mkali kama jua au moto wa kuchomelea.
  • Kama unafanya kazi kwenye kifaa kinachotoa mwanga kaa umbali wa sentimita 25 mpaka 30.
  • Tumia miwani ya jua ukiwa unaendesha pikipiki, baiskeli au gari iliyofunguliwa madirisha kuepusha vumbi na wadudu machoni.
  • Usichangie taulo ya kuogea, ugonjwa wa macho unaweza kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
  • Kama macho yako yamefanya kazi mda mrefu. yapumzishe kwa kuangalia umbali mrefu na kuyageuza huku na kule, weka kitambaa chenye maji ya uvuguvugu machoni ili kuongeza mzunguko wa damu machoni.
  • Nenda kwenye uchunguzi wa macho angalau mara mbili kwa mwaka baada ya kufikisha miaka arobaini. soma hapa kwa maelezo zaidi.tembelea blog yetu ya kingereza hapa

Wananchi wanashauriwa kwenda katika vituo vya afya pale wanapogundua kuna hali isiyo ya kawaida katika macho yao ili kupata matibabu, kwa sababu asilimia 80 ya matatizo ya macho yanatibika.

 

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *