Kukosekana kwa mifumo rahisi ya teknolojia ya mawasiliano katika taasisi za umma na binafsi ni kikwazo kwa wananchi kupata taarifa muhimu za maendeleo katika maeneo yao.
Inaelezwa kuwa taasisi nyingi za serikali hazijaunganishwa na mifumo ya kisasa ya kuhifadhi na kusambaza taarifa ili kuwawezesha wananchi kuzipata taarifa popote walipo. Hali hii inatajwa kuwalazimisha wananchi kutumia gharama kubwa na muda mwingi kuzifuata taarifa hizo katika taasisi husika.
Teknolojia inaozungumzwa hapa ni ile ya kutumia mitandao ya kijamii, tovuti, barua pepe au ujumbe mfupi wa simu ambapo ni njia rahisi kwa mtu kupata taarifa muhimu za bajeti ya serikali, miradi ya maendeleo na mfumo mzima wa utendaji serikalini.
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa Twaweza (Machi, 2017) juu ya upatikanaji wa taarifa, uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari umebaini kuwa teknolojia ya kisasa hazitumiki kupata taarifa kwasababu ya utendaji duni wa mifumo ya mawasiliano katika taasisi za serikali.
“Wananchi nane kati ya kumi (82%) wanasema wangeenda kwenye ofisi husika kama wangehitaji taarifa. 6% wangepiga simu, na wachache zaidi wangetuma barua pepe (1%) au wangetafuta taarifa hizo kwenye mtandao (1%)”, imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Takwimu za utafiti huo zilikusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,519 katika awamu ya 25 ya kundi la pili la Sauti za Wananchi, zilizokusanywa kati ya Novemba 7 na Novemba 27 mwaka 2017 ili kuchambua uzoefu wa wananchi wa kupata taarifa na maoni yao kuhusu vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza nchini ikizingatiwa kuwa serikali inayoongozwa na rais John Magufuli imekuwa ikilalamikiwa na baadhi ya watu kuwa inaminya uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa muhimu za maendeleo.
Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa ya mwaka 2016 pamoja na kanuni zake zilizopitishwa mwaka huu inatoa fursa kwa wananchi kupewa taarifa kwa njia mbalimbali kutoka taasisi za umma kwa sababu taarifa hizo ni mali ya wananchi.
Hata hivyo, Ukosefu wa mifumo ya kisasa ya kutunza taarifa katika taasisi za umma umechangiwa na uelewa na muamko mdogo wa wananchi kudai na kuzitafuta taarifa hizo. Na wengi hutafuta kama kuna ulazima wa kufanya hivyo na sio kwa manufaa ya kuongeza uelewa wa mambo muhimu yanayoendelea katika jamii.
Watafiti wa Twaweza waliuliza swali, mara ngapi wananchi huomba taarifa kutoka katika ofisi mbalimbali za umma na watoa huduma? Na wakagundua kuwa wananchi wengi hawatafuti taarifa jambo linazidisha pengo la teknolojia katika ofisi za serikali kuwafikia wananchi wengi.
“Mwananchi mmoja kati ya hamsini (2%) amewahi kutafuta taarifa kutoka kwenye tovuti ya serikali. Idadi kama hiyo wametafuta taarifa kutoka katika taasisi zisizo za kiserikali (2%), ofisi za serikali au wizara (5%) au ofisi za vyama vya siasa (5%)”, inaeleza ripoti hiyo na kufafanua kuwa,
“Kufuata taarifa katika ofisi zinakotolewa huduma za umma ni njia iliyozoeleka zaidi, lakini idadi kubwa ya wananchi hawajawahi kufanya hivyo. Mwananchi mmoja kati ya sita (16%) amewahi kutafuta taarifa kutoka shule ya serikali na idadi karibu na hiyo (13%) kwenye ofisi ya serikali ya mtaa”.
Kutoka katika ofisi zote nane zilizoainishwa, taarifa iliyoongoza kwa kuulizwa ni taarifa kuhusu bajeti, rasilimali na wafanyakazi (48%). Maombi mawili kati ya matatu ya taarifa (67%) yalifanikiwa kutolewa kwa wakati.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema “Pale ambapo wananchi hawatafuti taarifa kutoka serikalini na hawafahamu sheria zinasema nini kuhusu taarifa, wanaendelea kubaki gizani na kushindwa kushiriki katika kupigania huduma zinazokidhi mahitaji yao pamoja na kuiwajibisha serikali”.
Wakazi wa kata ya Kasulo wilaya Ngara katika mkutano wa kupata taarifa ya maendeleo
Nini Kifanyike?
Wananchi wengi wanaendelea kuamini kuwa taarifa zinazomilikiwa na serikali ni mali ya umma na zipatikane kwa wananchi, na uwazi wa taarifa hizo ni njia nzuri ya kupambana na rushwa na kulinda rasilimali za rushwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk. Vicensia Shule ameshauri kuwaongezea uwezo na teknolojia watumishi wa umma ili taarifa zinazotolewa ziwafikie wananchi kwa urahisi na muda mwafaka.
“Ni lazima tuwaongezee uwezo hawa watoa taarifa Serikalini. Ukienda kuomba taarifa unapewa kwa sababu ya 'muonekano' wako. Watoa taarifa wengi ambao ni Maafisa habari wana 'low self esteem' na wanataka kukuonesha nafasi yao”, ameshauri Dk. Vicensia.
Kwa upande wake Saimon Nyakaya kutoka Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) amesema serikali inapaswa kupokea taarifa za wananchi na kuzitolea ufafanuzi rasmi ili kuondoa malalamiko katika jamii kwa baadhi ya mambo yenye utata ambayo yanaweza kuvuruga mfumo wa utendaji wa jamii.
Akizungumza kwa niaba ya serikali, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas amesema serikali inaendelea na mchakato wa kuboresha mfumo wa upatikanaji taarifa serikalini na tayari imeanza kutoa mafunzo na kuwajengea uwezo Maafisa Habari katika wilaya zote nchini.
Mwaka 2017 serikali ilijitoa kwenye Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (OGP), jambo lililoibua mjadala juu ya dhamira ya dhati ya serikali katika upatikanaji wa taarifa kwa wananchi.