TUCTA watumbukia katika kashfa ya kutakatisha mabilioni ya fedha mali ya TRA

Jamii Africa

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limeingia katika kashfa kubwa ya kutumika kutakatisha fedha.

Katika mbinu za hali ya juu za kuingiza fedha haramu katika mzunguko halali, baadhi ya watumishi wa TUCTA wametumia shirikisho hilo kupitisha sehemu ya Sh. bilioni tano zilizotakatishwa.

FikraPevu limebaini kuwa hata baada ya kugundulika kwa “uporaji” huu, waliotiwa mbaroni na hata kesi kuanza, ni watendaji wadogo- wenye nafasi za chini, huku wahusika wakuu wakiendelea “kula bata” mitaani. Wako huru.

Imebainika kuwa fedha hizo zilizokuwa za malipo ya kodi kutoka Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kwenda Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA), zilichepushwa “safari” na kuingia kwenye akaunti kadhaa ikiwamo ya TUCTA na “kupotea.”

FikraPevu ina taarifa kuwa wahusika wakubwa wanatembea vifua mbele mitaani, baada ya kufanikiwa kuukwepa mkono wa sheria.

Kwa kuzingatia haya, FikraPevu inaweka wazi njia haramu zilizotumika kutakatisha fedha hizo kutoka kwa mmoja wa walipakodi wakubwa nchini.

Shilingi bilioni tano zilivyotakatishwa

Mnamo 20 Januari 2017, Hakimu Mkazi wa Kisutu, Reanatus Rutatinisibwa, aliwahukumu kifungo cha miaka mitano jela, aliyekuwa Mhasibu wa Masuala ya Kodi wa TTCL, Marcus Mussa Masila, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la jinai ya kutakatisha fedha zaidi ya Sh. bilioni tatu.

Pamoja na Masila, watu wengine wanne walioshirikiana naye katika kutenda jinai hiyo, walitiwa hatiani pia. Hao ni Justice Lumina Katiti,  Mhasibu wa TRA; Kanuti Ferdinand Ndomba, Meneja Miradi wa kampuni ya UEE Tanzania Limited; Gidion Wasonga Otullo, Mkurugenzi wa East Africa Procurement Services Ltd; and Robert Phares Mbetwa, Mkurugenzi wa Romos Technology Company Ltd.

Kwa mujibu wa hukumu, mahakama ilithibitisha pasipo shaka, kwamba, kati ya mwaka 2007 na 2009, watu hawa walikula njama na kufanikiwa kuchepusha Sh. 3,399,251,740 mali ya kampuni ya TTCL, zikiwa ni fedha kwa ajili ya malipo ya kodi zilizokuwa njiani kwenda TRA.

Pamoja na kwamba, mahakama imethibitisha kiasi nhicho cha fedha, FikraPevu imefanikiwa kupata taarifa zinazothibitisha kwamba, kiasi halisi cha fedha zilizochepushwa na “wapigadili” hawa ni Sh. 5,409,808,750.

Hii maana yake ni kwamba, kiasi cha Sh. 2,010,557,010 kiliporwa na hakuna ushahidi wa kimahakama wa kuwatia hatiani wahusika.

FikraPevu ina taarifa kuwa fedha hii imetakatishwa kwa kununua mali kama vile magari na majengo, kuanzisha biashara kama vile shule na kuendesha kampuni za kuweka na kukopa fedha, yaani, Microfinance Institutions (MFI’s).

Kwa ujumla, FikraPevu imebaini kwamba kuna kampuni kuu nne zilizotumika kufanikisha mchepuko huu wa kifedha. Kampuni hizo ni: International Legal Consultants, Eastgate Relocation Service, Six Dessile Traders, Trade Union Congress Of Tanzania (TUCTA) na UEE Tanzania Limted.

Nyaraka zinaonesha kwamba, viwango vya fedha zilizochepushwa kwenda katika kila kampuni ni kama ifuatavyo:

Jina la Kampuni

Anwani

Kiasi cha Fedha

Akaunti Na.

Cheki Na.

International Legal Consultants

P.O.Box 65534 DSM

 

300,731,421

0016011762,

Barclays Bank, Ohio Branch

 

36360

 

Eastgate Relocation Service

P.O.Box 108151 DSM.

304,302,521

0016008397, Barclays Bank, Ohio Branch

36678

 

Six Dessile Traders

P.O.Box 63378 DSM

 

740,750,237

0156003956, Barclays Bank, Kisutu Branch

37258 na

38165

Trade Union Congress Of Tanzania (TUCTA)

  P.O.Box 15359 DSM

 

671,212,379

01j1007892600, CRDB Bank

35973

 

UEE Tanzania Limted

P.Bo.Box Tarime, Mwanza

 

2,511,841,809

0102020446000, Standard Chartered Bank International House Branch

37532,

38092 na

37842

Nyaraka hazisomeki

Nyaraka hazisomeki

880,970,381

Nyaraka hazisomeki

36601

JUMLA (TZS)

 

5,409,808,750

 

 

Ni wazi kwamba, sehemu kubwa ya fedha iliyotoroshwa iliingizwa katika akaunti ya UEE Tanzania Limted, yenye makazi yake Tarime, huko Mara. Akaunti hii ilipokea kiasi cha Sh. 2,511,841,809.

Hata hivyo, kwa sehemu kubwa, akaunti hii ilikuwa ni daraja la kupeleka fedha hizo kwenye akaunti za kampuni nyingine nne za wapigadili. Kampuni hizo ni: HG Equipment and Parts, East Africa Procurement Services Limited, Plant And Machinery System na Romos Technology Co.Ltd. Mgawanyo wa fedha hizi kati ya kampuni hizi ulikuwa kama ifuatavyo:

Jina la Kampuni

Anwani ya kampuni

Akaunti  Na

Kiasi cha fedha 

Eastafrica Procurement Services Limited

P.O.Box 11175 DSM

 01j1021186000, CRDB Holland Branch, DSM

600,915,093

Hg Equipments And Parts

P.O.Box 7309 DSM

  56000283, Baclays Bank, Dsm

548,742,850

Plant And Machinery System

P.O.Box DSM

 102040067900, Standard Chartered Bank Kariakoo Branch, DSM

515,234,290

Romos Technology Co. Ltd

P.O.Box DSM

 240603610, Kenya Commercial Bank, Dsm

898,205,945

JUMLA (TZS)

 

 

2,563,098,180

Mbali ni wingi wa fedha zilizochotwa kimafia na wapigadili husika, jambo jingine linaloshangaza akili ni namna fedha hizo zilivyoweza kutoroshwa, kwa kipindi cha miezi sita mfululizo, tangu Juni 2008 mpaka Desemba 2008, bila taasisi husika kubaini ufisadi huo.

Jinsi utoroshaji wa fedha ulivyotekelezwa

FikraPevu imebaini kuwa wahusika walifanikisha njama za kupora fedha za serikali kwa ufundi mkubwa kupitia ushirikiano kati ya wafanyakazi wa TTCL na TRA, kama ifuatavyo:

Ndani ya TTCL, ilikuwa ni kawaida kuandaa na kupeleka kodi ya serikali kwenye ofisi za TRA kwa kutumia hundi.

Hundi hizo zilikuwa zinaelekezwa kwenye akaunti ya TRA iliyoko “NBC Corporate branch,” jijini Dar es Salaam. Chini ya utaratibu huu, NBC alikuwa ni wakala wa kukusanya kodi kwa niaba ya TRA na hatimaye kuwasilisha kodi hiyo katika akaunti ya TRA iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT). 

Hundi husika ilikuwa inaambatana na nakala tatu za fomu ya TISS (mfumo wa kufanya malipo ya kielektroniki kwenda BoT). Fomu hii ilikuwa inabeba maagizo yafuatayo: 

Please transfer from my/our account the amount of TZS ABC to Commissioner for Large Taxpayers, Tanzania Revenue Authority, Bank of Tanzania, Account Number PQR, Swift Code XYZ.

Yaani (tafsiri isiyokuwa rasmi), “Tafadhali hamisha kutoka kwenye akaunti yangu kiasi cha TZS ABC kwenda kwa Kamsihna wa Walipa Kodi Wakubwa, wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, iliyoko Benki Kuu ya Tanzania, Akaunti namba PQR, kwa kutumia nywila XYZ.

Fomu ya TISS pamoja na hundi zilikuwa zinabebwa na Mhasibu wa Kodi wa TTCL na kupelekwa benki ya NBC. Ni wakati wa safari hii, alipofanya uchakachuaji wa nyaraka, katika namna ambayo ilifanikisha uchepushaji wa fedha kwenda mahali kusikokusudiwa na mlipa kodi.

Katika uchakachuaji huo, fomu halali ya TISS ilikuwa inabadilishwa na nafasi yake kuchukuliwa na na fomu feki ya TISS, safari hii, fomu feki ikiwa inaielekeza benki kufanya malipo nje ya akaunti ya TRA  (“non-TRA Transfers).

Fomu feki ya TISS ilikuwa inataja kampuni binafsi ambayo ilioneshwa kama mlipwaji aliyekuwa ametoa huduma kwa TTCL.

Vinara wakuu wa mchongo wote huu walikuwa ni watu watano; Marcus Mussa Masila, Justice Lumina Katiti, Kanuti Ferdinand Ndomba; Gidion Wasonga Otullo na Robert Phares Mbetwa.

Japo, Mahakama haikuweza na huenda haitawezekana kubaini kisheria, wahusika wote waliokuwa nyuma ya pazia la mchongo huu, watu hawa watano ndio walikuwa “wanajeshi” waliokuwa mstari wa mbele, katika “uwanja wa mapambano,” kila mmoja akiwa na majukumu yake maalum. Lakini, mhusika mkuu ni Marcus Mussa Masila.

Wakati Masila akiwa safarini kwenda benki, huku akiwa amebeba hundi na fomu halali za TISS, alikuwa akifanya mambo matatu, hatua kwa hatua.

Kwanza, alikuwa anatenganisha hundi halali na fomu halali za TISS na kuzitunza fomu hizo halali mahali anakokujua yeye.

Pili, alikuwa anaandaa nakala tatu za fomu feki ya TISS, na kuziwekea mhuri feki wa TTCL na sahihi feki za maofisa wa TTCL. Katika fomu feki za TISS alionesha kwamba mwenye haki ya kulipwa, sio TRA, bali kampuni feki alizokuwa ameandaa yeye.

Tatu, angeunganisha hundi halali na fomu feki za TISS na kuzikabidhi kwenye benki ya NBC.

Mara baada ya benki kuzipokea nyaraka hizi, yaani, hundi halali na fomu halali za TISS, NBC wangezigonga mihuri, kuzisaini, kuhifadhi hundi halali na kubakiza nakala moja ya fomu ya TISS na kisha kumrudishia Marcu Mussa Masila, nakala mbili za fomu feki za TISS, lakini zenye saini na mihuri halali ya benki ya NBC.

Katika hatua ya nne, Marcus Mussa Masila, angefanya maandalizi ya kuzikabidhi nakala mbili za fomu feki za TISS kwenye ofisi za TRA, ili wathibitishe kama tayari malipo yamefanyika benki, wazisaini fomu hizo, wahifadhi nakala moja na kumpa nakala nyingine Masila kwa ajili ya kumbukumbu za TTCL.

Kwa vile, nyaraka feki zisingerudishwa ndani ya TTCL, wala kuhifadhiwa katika mafaili ya TRA, alilazimika kufanya uchakachuaji maalum hapa.

Fomu feki za TISS zenye mihuri halali ya benki ya NBC alizitupa, na kutafuta fomu halisi za TISS alizokuwa ameficha mahali hapo awali, safari hii, fomu halali za TISS zikigongwa mihuri feki na kuwekewa saini feki za wafanyakazi wa benki ya NBC.

Kwa vile wafanyakazi wa benki walioitwa mahakamani walikana kuhusika katika hatua hii ya uchakachuaji, hitimisho la kimantiki ni kwamba, Masila alichonga mihuri feki na kuitumia kwa ajili hii. Bila shaka, atakuwa alitafuta wataalam wa kughushi saini za wafanyakazi wa benki pia.

Baada ya hapo, katika hatua ya tano, Masila angewasilisha fomu halali za TISS, lakini zenye saini na mihuri feki ya benki, kwa Justice Lumina Katiti. Kwa kuwa hakuna hata senti moja ilikuwa imeingia kwenye akaunti ya benki ya TRA, ni wazi kwamba, Katiti “aliwezeshwa.”

Hivyo, Katiti akajifanya kaona fedha imelipwa, kusaini fomu husika, na baadaye kusawazisha hesabu kwenye mtandao wa kompyuta. Mwisho wa siku, kompyuta ilikuwa inaonesha kwamba fedha imepokelewa na TRA, na TTCL hadaiwi kitu!

Na hatimaye, katika hatua ya sita, Masila, angerudisha ofisini fomu halisi ya TISS, ikiwa na mhuri halali wa TRA, lakini yenye mhuri feki wa benki, na kuitunza katika mafaili ya TTCL.

Mchezo huu uliendelea kwa miezi sita mfululizo, mpaka hapo, “msamaria mmoja” ndani ya benki aligundua kwamba fedha zinazoingizwa na kutolewa kwenda kwa kampuni mbalimbali, kwa kuangalia wingi  wake, zilikuwa ni sawa na kodi ambayo alizoea kuona ikilipwa na TTCL kwenda TRA. Hivyo, msamaria mwema huyu akawapigia simu TTCL kuwatahadharisha juu ya mashaka yake. Hivyo, ndivyo siri ilivyofichuka!

Wahusika wakuu wakimbia kazi ndani ya TTCL

Baada ya siri hii kufichuka, baadhi ya wahusika wakuu walikuwa ndani ya TTCL wakaacha kazi kimyakimya. Miongoni mwao ni watumishi wawili wa Idara ya Fedha ndani ya TTCL.

FikraPevu linaweza, kwa uhakika kabisa kutaja namba zao za ajira kuwa ni PF 23187 na PF 90091.

Hata hivyo, majina yao kwa sasa hatutayataja kwa kuwa bado FikraPevu inaendelea na kazi za kiuchunguzi juu ya kashfa hii kubwa ndani ya taasisi ya umma.

Pamoja na hayo yote, kuna maswali kadhaa bado hayana majibu: Je, hizo Sh. bilioni tano zilizoporwa zitarudi serikalini? Na je, ilikuwaje, TUCTA inayojinasibu na kambi ya watetezi wa maadili, wakaanguka katika shimo la kashfa kubwa namna hii? Muda ni hakimu mzuri.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *