Siku za hivi karibuni tumesikia ugunduzi wa madini ya aina mbalimbali hapa kwetu Tanzania. Mpaka sasa tumesikia ugunduzi wa madini adimu duniani kama vile Graphite, Niobium na Helium (he).
Ugunduzi wa madini haya ya Helium umetokana na utafiti ulifanywa na vyuo vikuu vya Oxford na Durham katika Ziwa Rukwa ambako madini haya yamepatikana katika mita za ujazo bilioni 52.2. Madini haya ambayo yalidhaniwa kuanza kutoweka duniani hutumika kwa ajili ya mitambo ya Apollo na pia kutumika kwenye vifaa vya matibabu kama MRI na NMR.
Kwa upande mweingine, kampuni ya Volt Resources inayofanya utafiti wake wa madini ya graphite mkoani Mtwara katika wilaya ya Masasi imegundua uwepo mkubwa wa graphite ya hali ya juu katika mradi wao ujulikanao kama Namangale Graphite Project. Katika mradi huu wamegundua uwepo wa madini haya kwa kiasi cha tani milioni 214.4.
Madini haya hutumika kutengeneza betri za magari, betri za simu, penseli na pia betri za redio. Aidha maudhui makubwa ya kampuni ya Volt Resources ni kutumia madini haya kwa ajili ya muendelezo wa kutengeneza magari yanayotumia nishati ya umeme, kwani madini haya yatatumika kuhifadhi nishati ya umeme pindi gari inapochajiwa kama vile unavyochaji simu yako ya kiganjani.
Na hivi karibuni tena huko mkoani Mbeya katika eneo la Panda Hill lililoko katika Kata ya Songwe yamegundulika madini adimu aina ya niobium ambayo hutumika kutengeneza vifaa vya ndege na kompyuta. Mpaka sasa madini hayo huchimbwa kwenye bara la Amerika tu, hivyo kugundulika kwa madini hayo Tanzania kunaifanya nchi hii kuwa mgodi wa nne duniani na wa kwanza barani Afrika.
Haya ni baadhi ya madini yaliyogundulika katika miaka ya hivi karibuni na muda si mrefu uchimbaji wake rasmi utaweza kuanza.
Hii inadhihirisha utajiri uliopo nchini Tanzania katika aina hii ya madini na yale mengine ambayo tayari yamekwishaanza kuchimbwa kama vile dhahabu, almasi, makaa ya mawe, gesi asilia, tanzanite, madini ya chuma na mengine mengi.
Rai ya makala hii ni kusihi wataalamu wetu, watendaji na wananchi kwa ujumla kutorudia makosa yale ambayo tumeyashughudia na tunaendelea kuyashughudia katika madini mengine mbalimbali yanayoendelea kuchimbwa Tanzania.
Kwa miaka mingi tumeshughudia na tunaendelea kushughudia migogoro mingi na mikubwa katika rasilimali za madini na gesi asilia. Migogoro mingi imeibuka kutokana na kutokuwepo na uwazi katika mikataba na faida itokanayo na rasilimali madini.
Aidha kwa kiasi kikubwa tangu utafiti (exploration) mpaka uchimbaji wa madini mbalimbali nchini Tanzania wananchi wa maeneo husika hawakushirikishwa ama walishirikishwa kwa kiwango kidogo sana. Katika sekta hii ya madini kumekuwa na ushirikishwaji hafifu wa wananchi kwani maamuzi mengi yamekuwa yakitoka juu kwenda chini huku wananchi wasijue cha kufanya, hali hii imeleta migogoro mingi katika maeneo ya uchimbaji madini na gesi nchini Tanzania.
Swala lingine amabalo limeleta na linaendelea kuleta migogoro katika sekta ya madini ni fidia ya ardhi kwa wazawa husika. Tatizo kubwa katika sekta hii ya madini ni namna ambavyo fidia ya ardhi imekuwa ikifanyika wakati miradi imekwisha anza na sio kabla ya zoezi zima la utafiti na uzalishaji ili kuweza kuwaondoa wananchi katika maeneo ya migodi mapema kabla uzalishaji hujaanza ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima. Ni vyema sasa katika ugunduzi huu mpya fidia zote stahiki kwa wananchi ukaanza mapema kabla ya uzalishaji kuanza.
Kitu kingine ambacho huleta migogoro mingi katika sekta ya madini ni nafasi ya wananchi wanaozunguka migodi kwani kwa kiasi kikubwa tunashughudia umaskini wa hali ya juu uliokidhiri katika jamii zilizo pembezoni mwa migodi hiyo.
Ukienda katika migodi ya North Mara, Buzwagi, Bulyanhulu, Geita pamoja na kwenye uchimbaji wa gesi SongoSongo na MnaziBay. Wananchi hawa wanaozunguka migodi hii wako gizani wasijue ni fursa zipi wanazoweza kuzitumia kwa kuwa karibu na wawekezaji. Ni vyema sasa wananchi wakaelekezwa fursa zote ambazo wanaweza kuzitumia kwa wawekezaji wa mgodi ili waone manufaa ya kuwa karibu na rasilimali zao.
Ugunduzi wa madini aina mbalimbali unaendana sambamba na upatikanaji wa wataalamu watakaoweza kufanya kazi katika migodi hiyo. Imejidhirisha kwa miaka mingi sasa Tanzania inakosa wataalamu wa kutosha katika sekta ya madini na gesi. Ni vyema sasa wataalamu husika wakaanza kuandaliwa mapema ili uzalishaji utakapoanza kuwepo na wataalamu wa kutosha na kujiepusha na yale yanayotokea kwenye sekta ya gesi sasa ambako wataalamu wanaandaliwa kwa haraka mno kwa kuwa kuna uhitaji wa hali ya juu.
Mfumo wa kuandaa utendaji kazi baina ya makampuni machanga ya kitanzania na yale ya kutoka nje ukaanza kuandaliwa mapema ili waweze kufanya kazi sambamba na kupata ujuzi ili mwisho wa siku rasilimali hizi ziwe chini ya watanzania wenyewe. Kwa sasa hali ilivyo ni tofauti sana kwani wataalamu na makampuni ya kitanzania hayana fursa sawa na makampuni ya kigeni. Hili limezua mgogoro mkubwa sana katika sekta ya gesi huko Mtwara na Lindi ambako makampuni ya kitanzania yanakosa namna ya kuwa sehemu ya rasilimali hiyo na ndipo Tanzania Petroleum Development Corporation (TPDC) ikasema inafanya kazi kwa niaba ya makampuni machanga ya kitanzania. Ni wakati sasa hili likaangaliwa kwa ukaribu ili kuondoa migogoro katika ugunduzi mpya huu wa madini Tanzania.
Kwa kumalizia ni vyema mifumo thabiti ya kuchakata rasilimali madini ikaandaliwa ili uchakataji huo uanze hapa nchini badala ya kupeleka madini hayo kuchakatwa nje ya nchi ambako tunapoteza pato jingi kutokana na kile ambacho hupotelea huko nje. Katika mikataba inayotiwa sahihi ni vyema kukawa na makubaliano na makampuni ya kigeni ya uchimbaji kuweka miundombinu ya uchakataji nchini ili kuweza kupata faida ya kutosha kama taifa badala ya kwenda kunufaisha wengine. Sambamba na hili, katika mikataba hususani Profit Sharing Agrements (PSA) baina ya serikali na makampuni husika ifike mahali iwe nusu kwa nusu (50-50) ama 60-40 kwani tofauti na hapo makampuni ya kigeni yatapata faida kubwa na nchi itabaki na faida kiduchu tu isiyotosha kuwanufaisha watu wake wote.
Ningependa kuona sisi wananchi tukiwa sehemu ya maendeleo endelevu katika sekta hii ya madini kwa maana kwamba kuwepo na mijadala huru ambapo serikali na wadau wataweza kupata maoni ya namna bora ya kutumia rasilimali zetu. Mijadala hii inaweza kufanyika kama vile ambavyo tulifanya michakato ya katiba ili tuwe na makubaliano ya pamoja ambayo yatasaidia kupunguza migogoro katika sekta hii ya madini ambayo inazidi kila kukicha.
Rasilimali za taifa hili ni zetu sote wataalamu waje kwa wananchi kupata maoni na mirejesho kisha wakaandae sera, sheria na miongozo bora itakayoleta tija kwa taifa letu kwa ujumla.