HATIMAYE yametimia. Akinadada wa Twiga Stars wamefanikiwa kufuzu kwa raundi ya kwanza ya Ubingwa wa Soka wa Wanawake Afrika.
Mabao matatu ya haraka haraka yaliyofungwa dakika za mwisho yameisaidia timu hiyo kuishushia kipigo kizito Namibia cha mabao 5-2 katika mchezo wa marudiano uliofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo Jumapili.
Wenyeji wakijivunia umati wa mashabiki kwenye uwanja huo unaingiza watazamaji 60,000, walianza kwa kasi mchezo huo, lakini walilazimika kusubiri hadi dakika ya 21 wakati Mwanahamisi Omary alipopachika bao la kuongoza.
Mwanahamisi, ambaye bao lake la dakika ya 88 liliiwezesha Twiga Stars kupata ushindi wa 2-0 ugenini wiki mbili zilizopita, alimzunguka mlinzi Stacey Naris karibu na eneo la hatari na kufumua shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni.
Bao hilo lilitokana na juhudi za Fatuma Mustafa, ambaye alikimbia na mpira kwenye wingi ya kulia kabla ya kumimina majaro kwa mfungaji.
Wanamibia walisawazisha bao hilo katika dakika ya 29 baada ya mlinzi wa Twiga, Etoe Mlenzi, kujifunga mwenyewe katika harakati za kuokoa mpira wa kocha iliyochongwa na Elmarie Frederick.
Katika dakika ya 46, Asha Rashid aliifungia Twiga bao la pili akiunganisha pasi ya Fatuma, ambapo alipasua katikati ya walinzi wawili na kumchambua mlinda mlango kabla ya kukwamisha mpira kimiani.
Twiga ilifanya mabadiliko katika dakika ya 52 kwa kumpumzisha mlinzi Pulkaria Charaji na kumwingiza Mwajuma Abdallah ili kuimarisha ngome.
Namibia ilisimama imara na hatimaye kusawazisha katika dakika ya 73 kupitia kwa Juliana Skrywer, dakika chache baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Alberte Dakies.
Hata hivyo, kasi ya Twiga iliongezeka bada ya bao hilo la wanamibia, kwani katika dakika ya 84 Etoe Mlenzi alirekebisha makosa yake na kwenda kuifungia timu bao la tatu akiunganisha mpira uliotemwa na kipa wa Namibia na kushindwa kuokolewa na walinzi wa timu hiyo.
Mnamo dakika ya 88, Asha Rashid akaipatia Twiga bao la nne akipokea pasi ya Mwanahamisi Omary.
Mabao yalikuwa bado yanakuja, kwani dakika ya 90 Mwanahamisi Omary, ambaye jana aling’ara, akafunga kitabu kwa kuandika bao la tano baada ya kuukimbilia mpira mrefu uliopigwa na Fadhila Hamad.
Kama washambuliaji wa Twiga Asha Rashid na Mwanahamisi Omary wangezitumia vyema nafasi walizozipata katika dakika ya pili na ya nne, timu hiyo ingeibuka na ushindi mkubwa zaidi ya huo.
Kwa matokeo hayo, Twiga imeweza kusonga mbele kwa jumla ya mabao 7-2 kufuatia ushindi wao wa mabao 2-0 ugenini na sasa inasubiri mshindi kati ya Misri na Ethiopia ambao walikuwa wanacheza leo jijini Addis Ababa.
Kocha wa timu hiyo, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’, amekisifu kikosi chake kwamba kimecheza vizuri kwa kujituma na hatimaye kupata ushindi huo mzuri na mnono.
“Ni ushindi mzuri na mnono, kwa kweli inatia moyo sana na ninawaomba Watanzania waendelee kutuunga mkono katika kampeni hizi kwa sababu bado tunapambana,” alisema Mkwasa.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah, ameipongeza timu hiyo kwa ushindi pamoja na kufuzu kwa raundi ya kwanza na kusema timu hiyo imewatoa kimasomaso Watanzania.
“Kwa kweli imetutia moyo na tunaahidi kuwa nao bega kwa bega kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi. Tunaomba wahisani wajitokeze kuisaidia timu hii ambayo mpaka sasa haina mdhamini wa kudumu,” alisem Osiah.
Vikosi vilikuwa: Twiga – Fatuma Omary, Fatuma Bushiri, Pulkaria Charaji/Mwajuma Abdallah (52), Fatuma Khatib ‘Foe’, Sophia Mwasikili (nahodha), Mwapewa Mtumwa, Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’, Etoe Mlenzi, Fatuma Mustafa, Asha Rashid ‘Mwalala’ na Fadhila Hamad.
Namibia – Susanna Eises, Uerikondjera Kasaona, Lovisa Mulunga, Esther Amukwaya, Stacey Naris, Alberta Dakies/Juliana Skrywer (69), Shirley Cloete, Leticia Manga, Thomalina Adams, Elmarie Frederick and Lydia Eixas.
Habari hii imeandikwa na Daniel Mbega