Uelewa mdogo wa wananchi kudhoofisha harakati za upatikanaji wa katiba mpya

Jamii Africa

Matamanio ya watanzania wengi ni kuwa na katiba bora itakayoweza kusimamia rasilimali za nchi na kuhakikisha zinamnufaisha kila mwananchi na kuwa na ustawi mzuri wa jamii.

Licha ya matamanio hayo uelewa wa neno katiba bado ni mdogo miongoni mwa wananchi wengi. Huenda hali hiyo ikawa ni kikwazo kwa wananchi kupata katiba wanayoitaka. Juhudi za kuipata katiba mpya zimeanza muda mrefu lakini zimekuwa zikikwamishwa na baadhi ya watu ambao wanahofia kupoteza maslahi yao.

Kenya wamefanikiwa kupata katiba nzuri ambayo kwa kiasi kikubwa inakidhi matakwa  ya wananchi wa taifa hilo. Uelewa wa wananchi hao katika masuala ya sheria na katika umewaunganisha na kuwaweka katika muelekeo sahihi. Kenya inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye katiba bora Afrika.

Mathalani  mchakato wa katiba mpya ulikwama katika Bunge la Katiba mwaka 2015 baada ya makundi yenye maslahi kuibuka na kuipinga Katiba ya Warioba ambayo ilibeba maoni mengi ya wananchi. Katiba hiyo ikabadilishwa na kunyofolewa baadhi ya vipengele muhimu kama tunu za taifa, ukomo wa Ubunge, mfumo wa serikali tatu na nguvu aliyonayo rais.

Kutokana na  uelewa mdogo wa katiba, wanasiasa wameitumia hali hiyo kama fursa ya kuendelea kujinufaisha na kuyaweka kando maslahi ya wananchi na taifa.

Uchunguzi  uliofanywa na Shirika la Twaweza (2017) juu ya Sauti za Wananchi unaonyesha kuwa wananchi wengi wamesikia kuhusu mchakato wa katiba lakini hawajui hasa maana ya katiba na majukumu waliyonayo katika kuhakikisha katiba inatekelezwa ipasavyo katika kupata haki za msingi.

“Asilimia 93 ya Watanzania wameshawahi kusikia kuhusu katiba, lakini kati ya hao, asilimia 58 hawafahamu katiba ni nini”, inaeleza sehemu ya ripoti hiyo ya uchunguzi ambapo wananchi 6 kati ya 10 hawajui maana ya katiba.

Ikiwa zaidi ya nusu ya watanzania hawajui maana ya katiba, uwezekano wa kupata kilicho bora ni mdogo na hapo ndipo wale wachache huibuka na kuwachagulia wananchi kinachowafaa.

Ripoti ya Uchunguzi huo pia inaeleza kuwa iliwahoji wananchi 1,745 kati ya Juni na Julai 2017 ambao wengi wao walionyesha kuwa na uelewa mdogo juu ya katiba ambayo ni sheria mama ambayo inasimamia na kuweka utaratibu wa kiungozi katika jamii, 

“Wananchi wengi wamesikia kuhusu katiba lakini ni mwananchi 1 tu kati ya 3 anayeweza kueleza maana yake”.

 

Hata walipoulizwa maana ya katiba yalipatikana majibu tofauti  tofauti ambayo yalikuwa yanaelezea kazi za katiba katika nchi na wengine walishindwa kabisa kuelezea dhana hiyo.

“ Asilimia 22 wanasema katiba ni mkusanyiko wa kanuni zinazotumika kuongoza nchi na asilimia 12 wanasema kuwa katiba ni azimio la kisheria linalotumika kuongoza nchi. Ni asilimia ndogo tu (asilimia 1) wanaosema ni azimio la haki za wananchi. Maelezo yote matatu yanaweza kuwa sahihi, kwakuwa yanaeleza kazi moja ama zaidi za katiba ya nchi”, inaeleza ripoti hiyo.

Uelewa tofauti wa katiba miongoni mwa wananchi ni matokeo ya kutofautiana kwa kiwango cha elimu. Wananchi ambao wana elimu ndogo uelewa wao wa katiba ni mdogo ikilinganishwa na wananchi ambao wamepata elimu ya sekondari na chuo.

“Uelewa kuhusu maana ya katiba ni mkubwa miongoni mwa wenye elimu ya sekondari na elimu ya juu (asilimia 49) kuliko wale ambao hawajahitimu elimu ya msingi (asilimia 22)”, inafafanua ripoti hiyo lakini hata hao walio na elimu ya sekondari bado wapo wengi ambao hawaelewi katiba.

Asilimia 49 ni ndogo ikilinganishwa na 51% ya walioelimika ambao hajui katiba na maana, tafsiri yake ni kuwa bado tuna idadi kubwa ya watu wasiojua sheria mama na kuweza kuitetea kama dira ya kuwaongoza na kunufaika na rasilimali za nchi.

Uelewa pia unatofautiana kwa umri, watu wazima ambao wana umri zaidi ya miaka 50 wanauelewa mkubwa ikilinganishwa na vijana walio chini ya miaka 30 ambao wengi wao wako shuleni au wako katika sekta ya ajira.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa “Vilevile utofauti ni mkubwa miongoni mwa wananchi wenye umri zaidi ya miaka 50 (asilimia 45) kuliko wenye umri chini ya miaka 30 (asilimia 29)”, hii ina maana kuwa vijana 3 kati ya 7 ndio wenye uwezo wa kuelezea maana ya katiba na waliobaki  hawaelewi chochote na hawa ndio wanaathiriwa na mfumo mbovu wa elimu ambao haulengi kujenga uelewa kwa wanafunzi zaidi ya kuwawezesha kufaulu mitihani.

 

Uchunguzi huo wa Twaweza umeenda mbali na kubainisha kuwa hali ya kimaisha pia inachangia kutofautiana kwa uelewa , ambapo matajiri (watu wenye kipato kizuri) uelewa wao wa katiba uko juu kuliko wananchi maskini ambapo ni asilimia 28 kwa maskini na 40% kwa matajiri.

 Bado tofauti ya uelewa wa matajiri na maskini unadhihirisha wazi kuwa bado juhudi zinahitajika kuongeza uelewa wa masuala ya katiba kwa wananchi ikizingatiwa makundi yote mawili hayafikia japo nusu ya ulewa wa matakwa yao kisheria.

“Hata hivyo, suala lililojitokeza zaidi ni tofauti ya uelewa wa dhana hiyo kati ya wanaume na wanawake, asilimia 47 ya wanaume waliweza kueleza maana ya katiba, ukilinganisha na asilimia 22 ya wanawake’, inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.  Uchunguzi huu pia unatoa picha ya hali halisi ya mapambano ya kumkomboa mwanamke kielimu ili awe na mchango katika rasilimali za taifa.

Juhudi hizo ni muhimu ziende sambamba na kuwawezesha wanawake na wanaume kukua kifikra na kuwa na uwezo wa kuzipigania haki zao. Asilimia 47 ya wanaume na 22 ya wanawake bado haiakisi mafanikio makubwa ya mapambano ya kuleta usawa katika jamii.

 

Nini kifanyike?

Mifumo ya kutoa elimu ya uraia katika shule na vyuo iimarishwe na kulenga zaidi kuwajengea uwezo wanafunzi kuelewa masuala muhimu yanayohusu maisha yao ikiwemo katiba.  Ni muhimu wanasiasa kutanguliza maslai ya taifa mbele na kuwapa fursa wananchi kuchagua kile wanachokitaka.


 
Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *