MAENDELEO mazuri ya kukua na kuongezeka kwa urefu na uzito, ni muhimu kwa afya ya mtoto.
Lakini kwa mtoto Emmanuel John, mwenye umri wa miaka 2 ni tofauti; ngozi yake imekunjamana na anaonekana mwenye huzuni, ikiashiria ana matatizo ya kiafya.
Akiwa karibu na mama yake, Janeth Elias, ambaye anauza chakula eneo la Kijitonyama, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Emmanuel anaonekana kuwa na tumbo kubwa na urefu wake hauendani na umri alionao. Mtoto huyo amekumbwa na udumavu tangu akiwa mdogo.
Emmanuel ni miongoni mwa asilimia 24 ya watoto wote duniani waliodumaa, ambapo kati ya watoto wanne walio chini ya umri wa miaka mitano, mmoja amedumaa na inakadiriwa zaidi ya watoto milioni 165 duniani wana udumavu.
Shirika la Afya Duniani (WHO), linaeleza kuwa matatizo ya kudumaa ni miongoni mwa majanga makubwa yanayokwamisha maendeleo ya binadamu.
Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu vya udumavu, ikiungana na nchi nyingine za Afrika ambazo zinakumbwa na ukame, ukosefu wa chakula na huduma mbovu za afya ya mama na mtoto.
FikraPevu imepata Ripoti ya Uchunguzi ya Taifa ya Lishe (2014) ambayo inabainisha kuwa asilimia 34.7 ya watoto wenye umri wa mwezi 0 hadi miezi 59 (0-59) wamedumaa au wana Utapiamlo wa kiwango cha juu.
Kwa Tanzania Bara, matokeo ya uchunguzi yanaonesha kiwango cha utapiamlo kiko juu zaidi ya asilimia 40 kwa mikoa 9 (Iringa, Njombe, Kagera, Dodoma, Ruvuma, Rukwa, Kigoma, Katavi na Geita) na katika mikoa hiyo iko yenye kiwango cha juu ya asilimia 50, Iringa (51.3%), Njombe (51.5%) na Kagera (51.9%).
Zanzibar ina viwango vya udumavu ambavyo vinatofautiana kati ya eneo na eneo, Mjini Magharibi ni asilimia 20 na Unguja Kusini ni asilimia 30.4.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, zadi ya watoto milioni 2.7 walio chini ya umri wa miaka mitano wamedumaa nchini Tanzania ripoti hiyo inaeleza na kushauri hatua za haraka zichukuliwe katika mikoa ya Kigoma, Kagera, Mwanza, Iringa na Mbeya ambayo tatizo ni kubwa.
FikraPevu imeelezwa kuwa utapiamlo unatajwa kuwa sababu kubwa inayofanya watoto wengi kutokuwa na maendeleo mazuri ya ukuaji. Lishe duni isiyo na virutubisho muhimu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano humfanya mtoto kupungua uzito na urefu kutoendana na umri alionao.
Takwimu kutoka Shirika la Misaada la Marekani (USAID), zinabaanisha kuwa utapiamlo unachangia karibu robo tatu ya vifo vya vichanga na watoto nchini Tanzania na asilimia 21 ya watoto wanaozaliwa wana uzito wa chini kuliko ule wanaopaswa kuwa nao.
Pia lishe duni kwa wanawake wakati wa ujauzito huchangia watoto wengi wanaozaliwa kudumaa. Kukosa virutubisho muhimu kwa mjamzito husababisha maambuki ya magonjwa ambayo humdhuru kiumbe aliyepo tumboni.
Mimba za utotoni, shinikizo la damu na kuzaa watoto mfufulizo bila kufuata uzazi wa mpango huongeza ukubwa wa tatizo kwa wajawazito kujifungua watoto waliodumaa.
Udumavu huathiri zaidi ufahamu wa mtoto na kupunguza uwezo wa kujifunza na kupokea maarifa mapya. Wanafunzi wengi wanafeli mashuleni na kukosa muelekeo wa maisha kwa sababu ya udamavu wa akili ambao huanzia wakiwa tumboni.
“Mwanangu amefikia umri wa kuanza shule lakini mwalimu wake ameniambia uwezo wake ni mdogo na hawezi kuhesabu wala kuandika,” Judith Robert mkazi wa Kijitonyama, Dar es Salaam, ameiambia FikraPevu.
Judith ambaye ni mama wa mtoto Herry mwenye umri miaka 7, mwanaye ameandikishwa darasa la kwanza mwaka huu, lakini maendeleo yake darasani siyo ya kuridhisha kutokana na udumavu.
Judith anasema miaka miwili iliyopita alimpeleka mtoto wake katika darasa la awali, lakini huko nako alikuwa haelewi masomo. Anaongeza kuwa “wakati wa nikiwa na ujauzito nilipatwa na matatizo ya kiafya, labda ndiyo yamesababisha hali hii kwa mtoto wangu.”
Tatizo la kudumaa linatokea zaidi maeneo ya vijijini ambako elimu ya uzazi, huduma za afya na miundombinu iko katika hali mbaya, wajawazito na watoto hawapati huduma zinazotakiwa.
Shirika la Global Volunteers kwa kushirikiana na wadau wa afya na elimu nchini limezindua kampeni maalumu ya kuwasaidia wajawazito na watoto wa Kijiji cha Ipalamwa, Wilaya ya Iringa Vijijini, mkkani Iringa, kuepukana na tatizo hili.
Kijiji cha Ipalamwa chenye wakazi zaidi ya 5,000, wananchi wake wengi ni maskini na hawawezi kumudu mahitaji yao ya kila siku. Kwa mujibu ya Global Volunteers asilimia 50 ya watoto katika kijiji hicho wamedumaa.
Mwezeshaji wa kujitolea kutoka Shirika la Global Volunteer, Elise Kendali anasema wameweka kambi katika kijiji hicho ili kutoa elimu na kuwasaidia wajawazito na watoto kupata chakula na virutubisho muhimu.
“Tafiti zinaonesha kuwapatia wazazi maarifa muhimu na teknolojia inayoendana na mazingira yao, kutembelea nyumba kila wiki kutasaidia wazazi kupokea maarifa mapya na kuzuia udumavu” anasema Kendali na kuongeza kuwa
“Watalaamu wetu wanatoa huduma mbalimbali ikiwemo elimu ya afya na usafi kwa wazazi na watoto, virutubisho vyenye madini na kuwawezesha wanafunzi kulima bustani za mbogamboga ili kuepukana na njaa”
Kendali anasema mkakati huo hautaishia kwenye kijiji hicho bali mkoa wote wa Iringa ambao kwa kiasi kikubwa umeathirika na udumavu na kuhakikisha watoto wanapata elimu na kuwa na afya bora na kuondokana na umaskini.
Ili kufikia lengo la kuwa nchi yenye uchumi wa kati (middle income status) kufikia 2020, Tanzania inapaswa kutokomeza udumavu na utapiamlo ili kuongeza nguvu kazi ya uzalishaji inayopotea kwa watoto kukosa afya bora na elimu.