Ukeketaji unavyoendelea kuwaathiri wanawake Tanzania

Jamii Africa
Wanawake wakiwa na watoto. Ukeketaji huathiri wanawake wakati wa kujifungua na kusababisha wapoteze damu nyingi na hata kutishia maisha yao. Picha kwa hisani ya Shirika la Mamaye.

* Utafiti unaonyesha kuwa kwa kila wanawake 10 waliopo Tanzania, mmoja amekeketwa jambo linalotishia afya zao

AISI SOBO

Dar es Salaam. Wakati ukeketaji ukiendelea kushika kasi katika maeneo mbalimbali ulimwenguni, hali ni tofauti kidogo nchini baada ya vitendo hivyo kupungua kidogo ndani ya miaka 20 iliyopita.

Uchambuzi wa takwimu rasmi uliofanywa na Fikra Pevu unaonyesha kuwa ukeketaji umeshuka kutoka asilimia 16 mwaka 1996 mpaka asilimia 10 mwaka 2016, kiwango ambacho baadhi ya wadau wanasema bado kakiridhishi.

Hii ina maana kwa sasa, kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kwa kila wanawake kumi nchini mmoja wao ameguswa na ukeketaji na wengi wao hufanyiwa tohara mara tu wanapozaliwa.

Hata wakati vitendo hivyo vikionekana kupungua kidogo, Ripoti ya utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania 2015-16 uliotolewa na NBS inabainisha kuwa bado kuna baadhi ya mikoa nchini ikiwemo Manyara ambayo zaidi ya nusu ya wanawake wa wamekeketwa.

Hii inatokea licha ya uelewa wa wanawake kuhusiana na ukeketaji kungezeka. Ripoti hiyo inabainisha kwa wanawake 97 kwa kila 100 wenye elimu ya sekondari au zaidi wanafahamu athari za ukeketaji ikilinganishwa na wanawake 71 kwa wasio na elimu.

Mikoa mitano inayoongoza kwa ukeketaji kulingana na takwimu hizo ni Manyara, Dodoma, Arusha, Mara na Singida.

Wakati mikoa hiyo ikiongoza kwa ukeketaji, ipo mingine kumi ambayo imefanya vizuri katika vita dhidi ya ukeketaji au haina kabisa vitendo hivyo ni Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa, Ruvuma, na Kaskazini Pemba.

Mingine ambayo ina kiwango kidogo cha ukeketaji ni Kusini Pemba, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja na Kusini Unguja.

 

Tatizo la Dunia nzima

Tatizo hili siyo la ndani pekee. Pamoja na jamii ya kimataifa kupinga ukeketaji au tohara kwa wanawake na wasichana vitendo hivyo vimeongezeka kwa zaidi ya mara mbili ndani ya miaka mitatu ulimwenguni.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani(WHO) mwaka 2016 zinaonyesha zaidi ya wanawake milioni 200 katika nchi 30 barani Afrika, Mashariki ya kati na Asia wamepitia au kuguswa na ukeketaji hali ambayo inaongeza mwamko wa mapambano dhidi ya mila hii hatarishi. Kiwango hicho ni kikubwa ikilinganishwa na wanawake milioni 91.5 waliokuwa wamefanyiwa ukeketaji miaka mitatu iliyopita.

Wakati baadhi ya jamii zikiendelea kukumbatia ukeketaji kama suala la ‘kiutamaduni’, WHO inaeleza kuwa ukeketaji husababisha matokeo mabaya katika kipindi kifupi ikiwa ni pamoja na mshituko, kutokwa na damu nyingi na matatizo katika njia ya mkojo.

Pia huleta matatizo ya muda mrefu ambayo huweza kumpata mwanamke aliyekeketwa kuwa ni maambukizi ya VVU,  matatizo wakati wa kujifungua, kuongezeka kwa hatari ya vifo vya watoto wachanga, maumivu wakati wa kujamiiana, matatizo ya kisaikolojia na kifo.

Namna za ukeketaji

Zipo na nne zinatotumika kuwakeketa wanawake ambazo zimebainishwa na Shirika la afya duniani(WHO) na kutofautisha kati ya aina moja na nyingine.

Aina ya kwanza ni ile ambayo ngariba huondoa kinyama na sehemu inayozunguka au nyama ndogo sehemu za siri.

Aina ya pili ni ile ambayo mkeketwaji hukatwa eneo linalozunguka nyama na midomo ya ndani au sehemu yake.

Shirika  la Afya duniani limetaja aina ya kwanza na ya pili kuwa hufanyika duniani kote kwa kiwango cha asilimia 80.

Aina ya tatu ni ile ambayo hugusa sehemu yote ya siri ya nje ambapo  hushonwa ili kuzuia kujamiiana na kuachwa tundu dogo kwa ajili ya mkojo na hedhi ambayo imeonekana kufanyika kwa asilimia 15.

Aina hii ya tatu hulazimu mwanamke aliyekeketwa kufunguliwa kabla ya kushiriki ngono au kujifungua hali ambayo humsababishia mwanamke maumivu.

Aina hii imetajwa kuwa ni kati ya aina mbaya zaidi ya ukeketaji ambayo imeenea katika pembe ya Afrika na maeneo yake jirani Somalia, Djibouti na Eritrea, na katika baadhi ya maeneo ya nchi ya kaskazini mwa Sudan na kusini mwa Misri.

Aina ya nne ambayo  hufanywa kwa asilimia 5 ni ile ambayo mwanamke huunguzwa, kutoboa, kukata au kukaza sehemu ya siri ya ndani.

Pia aina hii huhusisha kumegwa kwa sehemu ya uke na kuanzisha vijipele ndani ya uke kwa kutumia dawa za asili kwa lengo la kufanya uke kuwa mdogo na kuubana.

Hali hiyo inafanana kabisa na inayoendelea Tanzania. Utafiti wa NBS unabainisha kuwa wanawake 81 kwa kila 100 waliokeketwa, wameondolewa kabisa nyama wakati saba wakiwa wameshonwa kabisa. Tisa kati ya 100 waliokeketwa hata hawajui aina ya ukeketaji uliofanyika katika mwili wao huku watatu pekee wakiwa hawajaondolewa nyama yote.

Ukeketaji hausababishi tu matatizo kwa wanawake. Wanaume ambao hukutana kimapenzi na wanawake waliofanyiwa vitendo hivyo baadhi hushindwa kuendelea nao kutokana na mapungufu katika maumbile yao.

 

Mwanaume aliyekutana na aliyekeketwa

“Kabla sikuwahi kukutana na mwanamke aliyekuwa katika hali ile kabla ya hapo, nilipokutana nao watatu Simanjiro mkoani Arusha, nilishtuka.  Wanawakata sehemu kubwa sana hata wanawaharibu maumbile yao,” anasema Frank kijana ambaye aliomba jina lake la pili kutotumika.

Frank (37), ambaye kwa sasa anaishi Dar es salaam akiwa na familia yake, anasema hakuweza kuoa yeyote kati ya wanawake waliokeketwa kwa kuwa hakuwa akifurahia kushiriki mapenzi nao.

Pia kutokana na kuondolewa sehemu kubwa ya uke na kuwafanya wasichana hao kuwa na sehemu za siri kubwa na hawakuwa wakifurahia kufanya mapenzi.

Frank anasema kuwa jamii ya kimasai hujuvunia sana mila na desturi zao ikiwa ni pamoja na ukeketaji na sio jambo rahisi kuwabadilisha.

Ni aibu kwa binti wa kabila hilo kutokukeketwa na hata hufikia hatua ya kutengwa pale anapofikia hatua ya kuolewa endapo atagundulika kuwa hakupitia mila hiyo.

“Hawaoni aibu kutokana na kukeketwa, kwa kuwa wengi wao hutegemea kuolewa na wanaume wa kabila lao ambao pia huunga mkono mila hiyo.

Lengo kubwa la kuwakeketa ni kuwafanya wanawake wasiwe wahuni au kuwa katika mahusiano na wanaume wengi ndio maana huwaondoa sehemu ile ambayo inaaminika kuwa huwa inawaletea hamu ya kufanya mapenzi,” anabainisha Frank.

Frank anaishauri serikali kuhamasisha zaidi wanaume kutokuunga mkono suala la ukeketaji kwani kama wao watakataa kuoa mwanamke aliyefanyiwa mila hiyo basi watoto wa kike hawatofanyiwa ukatili huo.

Kutokana na vitendo hivyo kuwa na madhara makubwa ya kiafya na kijamii, Serikali na wadau wamekuwa wakiendesha kampeni za kupinga ukeketaji katika mikoa mbalimbali ambayo imeshamili vitendo hivyo.

Msimamo wa wizara

Msemaji wa Wizara ya Afya kwa upande wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Erasto Ching'olo anasema Serikali inaendelea kupinga matendo yote ya ukatili na ukeketaji dhidi ya wanawake kwani matendo hayo huongeza wimbi la ndoa za utotoni.

"Ukeketaji unatekeleza mila, jadi na utamaduni wa kumuandaa msichana aweze kuolewa hata kama alikuwa bado ana fursa ya kuendelea na masomo yake," anabainisha Ching'olo.

Pia, amekubaliana na ushauri uliotolewa na Frank wa kuhamasisha wanaume kutokubaliana na ukeketaji, amesema tayari upo mpango kazi wa Serikali unaoendelea kuhusiana na kupinga ukatili kwa wanawake na watoto ambao umetambua umuhimu wa kuelimisha wanaume ili kupunguza wimbi la malendo hayo.

Anatolea mfano wa kampeni ya Magauni Matatu inayoendeshwa na Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, inayolenga kupinga mila potofu, ukatili, kumfanya mwanamke apate elimu na kuolewa na mwanaume atakayemchagua mwenyewe pale umri sahihi utakapofikia.

Moja ya sababu zinazopelekea kuwepo kwa ukeketaji ni kumuandaa msichana ili awe tayari kwa kuolewa bila ya kujali kuwa msichana huyo alikuwa na ndoto gani ikiwa ni pamoja na kumnyima fursa ya kupata elimu.

Katika kampeni ya kupinga vitendo vya ukeketaji Naibu waziri Wizara ya Afya, Wazee, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Dkt. Hamis Kigwangala alichapisha katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter namna ambavyo Serikali inapinga mila hizi potofu.

"Tanzania imezuia kutahiri wasichana/wanawake na tumefanya ukeketaji kuwa kosa la jinai, tunahamasisha njia mbadala za unyago". Dkt. Kigwangala.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *