Ukweli kuhusu minara ya simu kusababisha kansa kwa binadamu

Jamii Africa

Daniel Samson

Ukuaji wa sekta ya mawasiliano unaochochewa na ongezeko la idadi ya watu wanaotumia simu za mkononi umeibua mjadala juu ya usalama wa afya za watumiaji wa teknolojia hiyo muhimu ya kuwaunganisha watu katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonesha hadi kufikia Disemba 2017, idadi ya watumiaji wa simu za mkononi ilifikia  milioni 40 kutoka milioni 27.62 mwaka 2012 huku mtandao wa Vodacom ukiongoza kwa kuwa na watumiaji wengi waliosajiliwa.

Kuongezeka kwa watumiaji wa simu za mkononi kumesababisha ongezeko la minara ya simu inayojengwa katika maeneo mbalimbali ya makazi ya watu nchini.

Kulingana na Jarida la Tower Exchange (2016), inakadiriwa kuwa kuna zaidi ya minara 8,800 ya simu nchini Tanzania na 3,582 kati ya hiyo inamilkiwa na kampuni ya Helios Towers Africa ambayo inatoa huduma kama hiyo katika nchi za Ghana, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (Congo DRC) na Congo Brazzaville.

Minara ya simu ni vituo vya mawasiliano vyenye vifaa vya kielektroniki na antenna zinazopokea na kusambaza mawimbi ya radio (radiofrequency signals). Minara hiyo inatakiwa iwe na urefu wa futi 50 hadi 200 angani ili kuwa na uwiano mzuri wa mawimbi yanayotumika kwenye simu za mkononi.

Minara ya simu hupokea mawimbi ya mtumiaji wa simu na kuyabadilisha katika mfumo wa mawimbi ya radio ili kurahishisha mawasiliano baina ya watu wawili wanaozungumza wakiwa katika maeneo tofauti.

IDADI YA WATUMIAJI WA SIMU ZA MKONONI WALIOSAJILIWA TANZANIA (2017)

                Chanzo: TCRA

 

Minara ya simu inasababisha kansa?

Baadhi ya watu wamekuwa wakijenga hoja kuwa kuishi, kutembea au kusoma karibu na minara ya simu kunawaweka watu katika hatari ya kupata kansa au matatizo mengine ya afya.

Lakini mpaka sasa hakuna ushahidi wa moja kwa moja juu ya hoja hiyo. Katika nadharia za afya kuna sababu chache ambazo zinakubaliana na dhana ya minara ya simu kusababisha kansa. Chama cha Kansa cha Amerika (ACS) kimeeleza sababu mbalimbali za kwanini minara ya simu sio tishio kwa afya ya binadamu:

Kwanza, Nguvu ya mawimbi ya radio yanayotumiwa na minara ya simu ni ndogo ukilinganisha na mionzi mingine kama ya jua (ultraviolet light), Eksirei (x-rays) na nyuklia (gamma rays) ambayo inaongeza hatari ya kupata kansa. Mionzi ya mawimbi ya radio inayotolewa na minara ya simu haina nguvu ya kutosha kuvunja kemikali zilizoungana za vinasaba (DNA) vilivyopo mwilini.

Suala lingine ni urefu wa mawimbi. Mawimbi ya radio yana urefu ambao unaweza kujikusanya kwa inchi 1 au 2 na sio zaidi ya hapo. Hii ina maana kuwa mionzi ya mawimbi ya radio haiwezi kujikusanya kwa ukamilifu kuhatarisha seli za mwili.

Hata kama mawimbi ya radio kwa sehemu yangekuwa yanaathiri seli za mwili yasingefanikiwa kwasababu kiwango cha mawimbi hayo kinachopatikana ardhini wanakoishi watu ni kidogo sana kuliko kile kinachopendekezwa na watalaamu wa mawasiliano.

Mionzi ya simu za mkononi haina madhara sawa na ile ya radio inayopatikatikana katika maeneo ya mjini ambayo inazalishwa na vituo vya runinga na radio.

Hoja hizo zinaungwa mkono na Mhandisi Msaidizi wa Vodacom Kanda ya Kati, Eng. Josiah Kizindo wakati akihojiwa na vyombo vya habari amesema mionzi inayotoka kwenye minara haina madhara kama ambavyo imekuwa ikielezwa na baadhi ya watu.

“Kwa hiyo effect (athari) unayoongelea kwamba kutoka kwenye dishi (juu ya mnara) yaani umekaa mbele limekutaza iwe ndani ya mita mbili uwe umekaa tu kwenye dishi kwa muda mrefu hapo ndio unaona athari ya moja kwa moja”, amesema na kuongeza kuwa,

“Lakini zikishapita mita mbili kunakuwa hakuna athari, hii ni sawa na ile tochi unawasha mwanga unauona ukiwa kule mlimani, mwanga unauona lakini haukudhuru. Kwa hiyo kimsingi (minara ya simu) haina madhara yoyote”.

 

Utafiti uliofanywa kwa watu

Katika utafiti uliofanywa nchini Uingereza ulilinganisha kundi la familia za watoto 1,000 ambao walikuwa na kansa na kundi lingine la familia za watoto wasio na kansa. Walibaini kuwa hakuna uhusiano kati ya wanawake ambao walikuwa wanaishi karibu na minara ya simu wakati wa ujauzito na hatari ya kupata kansa kwa watoto waliozaliwa.

Utafiti mwingine ulifanya ulinganifu wa kundi la watoto zaidi ya 2,600 wenye kansa na wale wasio na kansa. Walibaini kuwa watoto waliokuwa wanaishi mjini ambako kuna kiwango kikubwa cha mionzi ya mawimbi ya radio lakini hawakuwa katika hatari kubwa ya kupata kansa.

Hata hivyo, utafiti huo haujazungumzia idadi ya minara iliyokuwepo na ni umbali gani ambao watoto hao walikuwa wanaishi ukilinganisha na minara ilipo.

Watafiti wengine kutoka nchi hiyo, walichunguza vinasaba (DNA) na madhara ya seli za damu kama kiashiria cha kusababisha kansa. Walibaini kuwa hakukuwa na madhara yoyote kwa watu waliokuwa wanaishi karibu na minara ya simu ukilinganisha na wale ambao hawako karibu na minara hiyo.

Kiasi cha miozi inayopatikana kwa kuishi karibu na minara ni kidogo kuliko kile kinachopatikana katika matumizi ya simu za mkononi. Karibu tafiti 30 zilizofanyika juu ya mahusiano ya kutumia simu na kutokea kwa kansa zimebaini kuwa hakuna mahusiano ya moja kwa moja.

 

Uchunguzi Maabara

 Uchunguzi wa maabara za sayansi umefanyika kubaini kama mionzi inayotoka kwenye mawasiliano ya simu inaweza kusababisha kuharibika kwa DNA. Tafiti nyingi zinakubaliana na hoja kuwa mionzi inayotolewa na simu za mkononi na minara haina nguvu ya kutosha kuharibu DNA moja kwa moja.

Kutokana na hoja hizo za utafiti sio sahihi kusema kwamba simu na minara zinaweza kuwasababisha kansa lakini utafiti katika eneo hili ni muhimu ili kujiridhisha madhara mengine ya kiafya ambayo mtu anaweza kuyapata.

 

Kuna haja kukaa mbali na minara ya simu?

Minara ya simu bado haijathibitishwa kusababisha madhara yoyote ya kiafya.  Lakini ukiwa unaishi karibu na minara ya simu na ukahisi hali tofauti ya kiafya uliyoizoea ni muhimu kumuona daktari kwa ajili ya uchunguzi na ushauri.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *