MALENGO ya kuzalisha kahawa nchini kufikia tani 80,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2016 huenda yasifikiwe kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, iliweka malengo hayo katika kuhakikisha ili kukidhi mahitaji ya masoko ya ndani na nje.
Mabadiliko ya tabia nchi yamesababisha kuwepo kwa mbadiliko ya hali ya hewa ikiwemo ukame, hali ambayo kwa kiasi kikubwa imeanza kuathiri kilimo cha kahawa katika baadhi ya mashamba kutokana na mimea yake kukauka kwa kukosa maji.
Baadhi ya wakulima wa Wilaya ya Mbeya wakizungumzia mabadiliko ya tabia nchi, wamesema athari zake zimeanza kuonekana kutokana na kupungua kwa kiwango cha mvua huku maeneo mengine yakikosa mvua kabisa na kusababisha miche ya kahawa kuathirika kwa ukame.
“Kukauka kwa miche na miti ya kahawa kutayumbisha uchumi wa kaya nyingi ambazo zinategemea zao hilo kwa ajili ya kusomesha watoto, kuongeza pato la familia, kumudu huduma za afya pamoja na kushiriki katika kuchangia shughuli za kijamii,” anasema Gibson Mposa, mkulima na mkazi wa Kijiji cha Idugumbi wilayani humo.
Mposa anasema kahawa ndilo zao kuu la biashara linalotegewa wilayani humo hivyo wanaiomba Serikali kulinusuru kwa kuwajengea miradi ya maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
“Kahawa pia inachangia kiasi kikubwa katika mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, hivyo kutetereka kwake kutayumbisha hata uchumi wa Taifa,” anasema.
Rose Mwakatwila, mkazi wa Kijiji cha Msiha, anasema ukosefu wa mvua za kutosha pamoja na athari zinazotokana na kuathirika kwa zao la kahawa ni hatari kwa kuwa inaweza kuhatarisha amani na usalama katika maeneo wanayoishi.
“Shughuli za kilimo cha kahawa ndizo zinategemewa na wengi, hivyo athari zake zinasababisha kukosekana kwa mapato na kuna uwezekano wananchi, hasa vijana, wakajiingiza kwenye uhalifu na pia vita ya kugombea maji baina ya wakulima,” anasema.
Anasema ipo haja kwa kuanzia seriali za vijiji na serikali kuu kuweka mikakati ya kujenga miundo mbinu ya kilimo cha umwagiliaji pamoja na uhifadhi wa maji.
Ofisa Kahawa wa Wilaya ya Mbeya, Lupakisyo Masuba, anasema mabadiliko ya tabia nchi yanayosababishwa na kasi kubwa ya uharibifu wa mazingira, ni miongoni mwa chanzo kikubwa kinachochangia kupunguza kiwango cha mvua na kuleta ukame.
“Hakuna mvua za kutosha kwa sasa kutokana na uharibifu wa mazingira unaofanywa na shughuli za kibinadamu, hii ni hatari, siyo kwa zao la kahawa tu, bali kwa kilimo kwa ujumla,” anasema.
Meneja wa Mradi wa Kuboresha na Kuongeza Uzalishaji wa Kahawa katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, unaofadhiliwa na Shirika la Hanns R. Neumann Stifftung la Ujerumani, Webster Miyanda, anasema ili kuepukana na athari hizo ni lazima wakulima kuzingatia na kufuata mafunzo ya kilimo hifadhi mazingira ili kuhifadhi uoto wa asili.
Anasema wanachofanya wao ni kutoa elimu na kuwawezesha wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuboresha uzalishaji wa kahawa, zao ambalo mahitaji yake ni makubwa kuliko uzalishaji.
“Tunawaelekeza wakulima kutunza mazingira kwa kufuata elimu ya kilimo bora, kama wanalima kwenye miinuko ni lazima watumie matuta na kuweka makingamaji ili kuepusha mmomonyoko wa udongo, lakini pia wajitahidi kupanda miti kuzunguka mashamba yao ili kuhifadhi uoto wa asili,” anasema.
Meneja wa Nyanda za Juu Kusini wa Kituo cha Utafiti wa Kahawa (TaCRI),kilichopo Mbimba wilayani Mbozi, Isaac Mushi, anasema wameanza mpango wa utafiti ambao utawawezesha wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Anasema mabadiliko ya tabia nchi yameathiri uzalishaji wa kahawa kutokana na hali ya hewa isiyotabirika na mvua zisizotosheleza mahitaji.
“Katika kukabiliana na changamoto hiyo tumezalisha mmea mpya wa kahawa ambao unakabiliana na ukame, utafiti unafanyika katika Kijiji cha Bora na umeweza kudumu kwa miaka miwili,” anasema na kuongeza kuwa utafiti huo unaweza kuchukua miaka mitano hadi saba kukamilika.
Mushi anasema wakulima wadogo ndio wanaoathirka zaidi na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwa hawawezi kumudu kuendesha kilimo cha umwagiliaji na kwamba wanaomudu ni wakulima wakubwa tu.