UTAFITI mpya uliotolewa na Chuo Kikuu cha British Columbia cha nchini Canada umebaini kuwa kunusa nguo ya mpenzi wako aliye mbali nawe kunasaidia kupunguza msongo wa mawazo na kudumisha upendo. Wanawake ndio wanaotajwa kufaidika zaidi kwasababu wana mfumo mzuri wa kunusa kuliko wanaume.
Majaribio ya utafiti huo yalihusisha wanawake 96 ambao waliambiwa wanuse mashati 3 ya waume zao ambayo hayajafuliwa. Baada ya kunusa mashati hayo walipewa majaribio ya kupima wanavyoweza kukabiliana na msongo wa mawazo ikiwemo mtihani wa hesabu na mahojiano yenye viashiria vya dhihaka.
Majaribio hayo yalilenga kubaini kiwango cha homoni ya 'Cortisol' inayozalishwa na mwili wakati mtu napokuwa na msongo wa mawazo ili kujihami na hatari yoyote ya mwili inayoweza kutokea. Homoni ya Cortisol ni mahususi kupambana na hasia hasi zinazokuja mwilini.
Matokeo ya utafiti huo yameonyesha kunusa nguo ya mpenzi wako hasa shati kunapunguza hisia hasi, msongo wa mawazo (sononeko, huzuni) na kuongeza uzalishaji wa homoni ya 'cortisol'. Wanawake hao waliweza kutambua harufu za waume zao kwa kutumia mashati waliyonusa. Utambuzi wa harufu uliwasaidia kupunguza madhara ya msongo wa mawazo na kuimarisha afya zao.
Jambo lililovutia ni wanasayansi hao kugundua kuwa kunusa nguo ya mtu usiyemfahamu pia kunaongeza kiwango cha uzalishaji wa homoni ya cortisol kupambana na mkazo ambayo hutusaidia kujilinda dhidi ya hatari inayokuja kwetu.
"Tangu umri mdogo, binadamu wanaogopa wageni hasa wageni wa kiume, kwahiyo inawezekana harufu ya mgeni wa kiume inachochea muitikio wa kujihami ambao hupelekea homini za cortisol kupanda", amesema Kiongozi Mwandishi wa utafiti huo, Marlise Hofer. "Hili haliwezi kutokea kama sisi hatujatambua".
Matokeo ya utafiti huo ambao umethibitishwa kwa vitendo unahimiza wenza ambao wanaishi mbali, wanaweza kunusa nguo za wapenzi wao kama njia ya kupunguza kiwango cha msongo wa mawazo. Licha ya utafiti huo kuhusisha mashati pekee lakini watafiti wanashauri kuwa nguo yoyote inaweza kutumika ikiwa tu haijafuliwa.