ASILIMIA 11 ya wananchi wa Tanzania, waamini Serikali ya Rais John Magufuli, inaongoza kwa mfumo wenye viashiria vya kidikteta.
Vitendo kama vile kuzuia kurushwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya bunge, kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari, kufikishwa mahakamani kwa Watanzania sita kwa madai ya kumtukana Rais na kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa, vinasababisha wananchi kuona hakuna demokrasia nchini.
Mnamo Juni 7 mwaka 2016, Jeshi la Polisi lilitoa zuio kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara. Kwa upande wa vyama vya upinzani, vizuizi hivyo vilichukuliwa kama ukiukwaji wa haki zao za kikatiba, kidemokrasia, kukatazwa kukusanyika na kuminywa kwa uhuru wa kutoa maoni.
Ripoti iliyoifikia FikraPevu kutoka taasisi ya Twaweza, shirika lisilo la serikali kupitia utafiti wake wa Sauti za Wananchi wenye jina la “Demokrasia, udikteta na maandamano: Wananchi wanasemaje?” uliofanyika kuanzia tarehe 24 hadi 29 Agosti mwaka huu, unakuja na matokeo kwamba
Baadhi ya wanasiasa na wasomi wanautafsiri uongozi wa Rais Magufuli kama udikteta, na neno hilo likiwa ni mojawapo ya maneno yanayounda UKUTA, ambapo baadhi ya vyama vya upinzani walilitafsiri kama ‘Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania’
Asilimia 11 ya wananchi hao, wanakubaliana kwamba nchi inaongozwa katika misingi isiyofaa, hivyo kumuona rais kama kiongozi anayetumia mabavu. Asilimia 58 wanapinga kuwepo uongozi mbaya, asilimia 31 hawana uhakika kuhusu kuwepo ama kutokuwepo kwa uongozi mbovu.
Kati ya wanaouona uonevu, asilimia 13 ni wanaume, huku asilimia 8 pekee wakiwa ni wanawake.
Makundi ya vijana, matajiri na wenye elimu ya juu, wanamuona Rais Magufuli kuwa ni dikteta kuliko wazee, masikini na wenye elimu ya chini.
Aidha, asilimia 29 ya wananchi waliokaribu na vyama vya upinzani, wanamwona Rais Magufuli kama dikteta, huku miongoni mwa wale ambao wanajiona wapo karibu na chama tawala, CCM, asilimia 5% tu wana mtazamo huo, ikimaanisha kuwa mmoja kati ya wafuasi ishirini wa CCM anamuona Rais Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho kama dikteta.
Vyama vya upinzani viliongeza kulalamika baada ya serikali kukataa kutoa kibali cha kufanya maandamano yaliyopangwa kufanyika tarehe 1 Septemba, 2016 nchi nzima kupitia umoja wao uliopewa jina la UKUTA. Hii ilikuja baada ya katazo la awali la kuendesha mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa majimboni.
Viongozi wa UKUTA walielezea kuwa kuzuiwa kufanya mikutano ni ukiukwaji wa haki za binadamu na uhuru wa kujieleza na kuwa karibu na wapigakura wao.
Kwa undani zaidi, utafiti unaonesha kuwa, wananchi wana mitazamo mchanganyiko na inayokinzana kuhusu nchi inavyoongozwa, wengine wakidai uongozi uko sawa na wengine wakiwa na malalamiko.
Wakati baadhi ya wananchi wakimchukulia rais kama kiongozi anayetumia ubavu, wananchi 6 kati ya 10 wanaunga mkono uzuiaji wa mikutano na maandamano ya vyama vya siasa katika kipindi kisicho cha kampeni za uchaguzi.
Uungwaji mkono huo ni mkubwa kwa asilimia 70, miongoni mwa wafuasi wa chama tawala (CCM), na ni mdogo asilimia 31 miongoni mwa wafuasi wa vyama vya upinzani. Pamoja na hayo, wazee wengi zaidi wanaunga mkono uamuzi huo (asilimia 70) kuliko vijana (asilimia 55).
Kwa ujumla, uwepo wa vyama vingi na uhuru wa kutoa maoni unapendekezwa na wananchi walio wengi kwa kuona ndio mfumo wa vitendo vya demokrasia.
Wakati uhuru wa mikutano na kujieleza kwa kutoa maoni kukipendekezwa kama njia ya kutokomeza udikteta nchini, baadhi ya wananchi hawakubaliani na mbinu zinazotumiwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani katika kuhakikisha demokrasia hiyo inalindwa.
Wananchi wanasema baadhi ya vizuizi kwenye haki za kidemokrasia ni muhimu, ili kulinda amani na kuharakisha maendeleo, lakini iwapo vitendo visivyo vya kidemokrasia vitafika mbali zaidi, utayari wao wa kukubaliana navyo huenda ukabadilika.
Idadi kubwa ya wananchi wanaunga mkono uhuru wa kutoa maoni, kuhudhuria mikutano na viongozi waliowachagua, na haki yao inayopotoshwa ya kuikosoa serikali pale inapoteleza kwenye uamuzi wake.