Utamaduni wa Kisandawe waviza kiswahili shuleni

Kiswahili ni lugha ya kibantu yenye misamiati mingi ya kiarabu,lugha hii kwa sasa inazungumzwa katika maeneo mengi ya afrika ya mashariki.
 
Historia inaonesha kuwa Kiswahili kilianza kutumika zaidi ya miaka 1000 iliyopita katika mazingira ya vituo vya biashara ya utumwa huko Pwani ambapo wafanyabiashara kutoka uarabuni walikutana na wenyeji waafrika.


Nchini Tanzania lugha hii ni ya taifa  ni lugha ya kwanza kwa shughuli zote za kiserikali na mawasiliano ya watu wa aina mbalimbali.
 
Pamoja na Serikali kuamua lugha ya Kiswahili itumike kufundishia karibu masomo yote ya shule za msingi lakini wilaya za Chemba na Kondoa zinakabiliwa na changamoto kubwa inayosababisha wanafunzi wengi kufeli  mitihani yao ya taifa kutokana na asilimia kubwa ya wanafunzi kuzungumza  lugha ya Kisandawe wanapokuwa maeneo ya shule badala ya lugha ya Kiswahili.
 
Mwandishi wa makala hii alitembelea shule mbalimbali katika wilaya hizo mbili,baadhi ya shule hizo ni pamoja na Pongai, Kelema maziwani, Mondo, Waudi, Makamaka, Cheko, Piho, Farkwa, Kurio na Kwamtoro.
 
Wanafunzi wa shule hizo waliozungumza na mwandishi wa makala hii,wamekiri  kuzungumza lugha yao ya kikabila yaani Kisandawe ambapo wamesema kuwa sababu kubwa ni mazoea kwani wakazi wengi wa Vijiji wanamoishi wanazungumza Kiswahili kwa asilimia ndogo sana.
 
Mwanafunzi Habiba Hassan wa shule ya msingi Pongai anasema kuwa majumbani kwao wazazi wanatumia lugha hiyo na sio Kiswahili ndio maana imewajengea mazoea ya kuizungumza hata katika maeneo ya shule.
 
Mwanafunzi huyo anasema kuwa Kishwahili hutumiwa sana katika maeneo muhimu kama vile kwenye vituo vya afya,msikitini na makanisani lakini majumbani hutumia lugha ya Kisandawe kwao kujua kiswahili hakuna maana yoyote.
 
Mwanafunzi mwingine ni James Mgoli yeye anasema kuwa anaishi nyumbani na  bibi na babu yake ambao hawajui kabisa kuzungumza lugha ya Kiswahili,hivyo wakati wote na yeye akiwa nyumbani anaitumia lugha hiyo ya Kisandawe.

Anasema kuwa hali hiyo ya kuzama zaidi katika utamaduni inawaathiri na wanajikuta wakitumia lugha ya Kisandawe katika maeneo ya shuleni.

Baadhi ya wazee katika wilaya ya Chemba,wanasema kuwa kabila lao linajali  sana utamaduni katika mambo yote ndio maana hata leo wanaendelea kuudumisha kizazi hadi kizazi.

Mzee Hamisi Keila ambaye ni kiongozi wa msikiti anasema kuwa wasandawe wanazingatia sana mila zao na ndio maana hata watoto wao wameathirika na kujikuta wanapenda kutumia lugha yao ya kiutamaduni hata katika maeneo ya shule.

Mzee huyo anafafanua kuwa wao wanaamini kuwa utamaduni wao umewasaidia  vijana na watoto wao kuwa watu wema na hawajihusishi na mambo mengine maovu.

Amesema kwa mfano katika watu karibu 200 wa Kijiji chake waliopima ukimwi  katika kipindi cha mwaka jana hakuna hata mmoja aliyegundulika na virusi vya  ukimwi hii inatokana na kwamba mila na tamaduni zao zinawasaidia wasijihusishe na maovu.

Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Chuo kikuu cha Dodoma,Frenk John anasema kuwa yeye kwa upande wake anadhani kwamba huenda elimu ilichelewa kuingia  maeneo hayo ndio maana bado watu hawaoni umuhimu wa kutumia lugha ya  taifa.

Kwa upande wake afisa elimu wa wilaya ya Kondoa bwana Andason Mwalongo  amekiri kuwepo kwa tatizo hilo ila amesema kuwa ni kwa baadhi ya shule zilizopo maeneo ya pembezoni mwa wilaya na sio za mijini.

Amekiri kuwa hali hiyo inaawaathiri wanafunzi katika masomo yao kwani hata  katika mitihani muhula baadhi ya wanafunzi wasiojua Kiswahili kwa ufasaha wanashindwa kufanya vizuri.

Anafafanua kuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita shule za msingi za  Kondoa na Chemba zilishika nafasi ya mwisho kimkoa katika mtihani wa taifa  wa darasa la saba.

Naye afisa elimu wa wilaya ya Chemba,Elieta Erdwad,amekiri kwa baadhi ya shule zake wilayani humo kukabiliwa na changamoto hiyo lakini amesisitiza kuwa tayari wameshalitafutia ufumbuzi tatizo hilo.

“Unajua kwa miaka ya sasa tatizo hili ndugu mwandishi limepungua tumetumia mbinu nyingi ikiwemo kutoa adhabu kwa mtoto anayeongea kilugha katika mazingira ya shule,mbinu nyingine walimu hutembelea wanafunzi majumbani na mikutano ya wazazi ambapo wanaelezwa wasisitize watoto wao kutumia zaidi Kiswahili”alisema Edward.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk Rehema Nchimbi,ameeleza kuwa tayari amepokea taarifa kutoka idara ya elimu mkoani hapa ambayo inaeleza kuwa changamoto hiyo inaendelea kushughulikiwa.

Dk Nchimbi anaeleza kuwa anaamini wataalamu wake watalimaliza suala hilo japokuwa linaweza kuchukua muda.

“Unajua wale wanaoanza darasa la kwanza ndio tuaamini kuwa utamaduni umewaathiri sana tofauti na wanafunzi wa darasa la tatu hadi la saba ambao sasa wanaona umuhimu wa kutumia lugha ya Kiswahili,kwani mkazo tunauweka  kwa hawa wanaoanza” alisema Dk Nchimbi.

1 Comment
  • Ni kweli kabisa lakini serikali inatusaidiaje maana hata huduma kijamii kwetu ni shida mfano maji na barabara zetu ni mbovu na elimu bado kabisa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *