WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), imeanza uchunguzi wa vyeti vya Miss Tanzania 2014, Sitti Abbas Mtemvu, baada ya kuibuka utata wa taarifa za kuwapo vyeti viwili vinavyotofautiana maelezo.
Uchunguzi wa FikraPevu umethibitisha kuwapo upekuzi maalumu wa nyaraka alizowasilisha Sitti katika ofisi za RITA Temeke ili kubaini kwanza uhalali wa cheti, kabla ya kutafuta ukweli wa taarifa zilizowasilishwa chini ya kiapo.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Sura ya 108 Toleo la 2002), ni kosa la jinai kutoa taarifa za uongo kwa Msajili na pia ni kosa la jinai kughushi, mambo ambayo yakithibitika RITA watalazimika kulikabidhi suala hilo kwa Jeshi la Polisi.
Mkurugenzi wa Sheria wa RITA Emmy Hudson, ameithibitishia FikraPevu leo kwamba mamlaka hiyo inachunguza suala hilo kwa umakini ili kuhakikisha haki inatendeka kwa mhusika.
“Tunachunguza kutafuta ukweli na hatutamuonea wala kumlinda mtu kwani hili suala linagusa hadhi ya mamlaka na nchi kwa ujumla,” anasema Emmy akiwa ofisini kwake Dar es Salaam.
Uchunguzi wa RITA unahusisha pia nyaraka zote za watoto waliozaliwa Temeke katika miaka ya 1980 hadi 1990 kipindi ambacho Sitti alizaliwa. Kipindi hicho kulikua tayari na mradi maalumu wa uandikishaji wa watoto wanaozaliwa hospitalini na majumbani na hivyo kuwapo kumbukukumbu zote.
Katika mashindano ya Miss Temeke yaliyofanyika Jumamosi Agosti 23, 2014, Sitti aliyeibuka mshindi alidai amezaliwa mwaka 1991 kabla ya kupata cheti kilichodaiwa kutolewa na RITA Septemba 9, 2014 kikionyesha kazaliwa nyumbani Temeke Mei 31, 1991.
Cheti hicho kinaonekana kimetolewa wiki chache kabla ya kilele cha mashindano ya kumtafuta mrembo wa Tanzania ambayo tena Sitti huyo alitangazwa mshindi.
Hata hivyo, kupitia mtandao wa JamiiForums ulibuliwa ushahidi wa hati ya kusafiria ya Sitti ikionyesha alizaliwa Mei 31, 1989 na si 1991 kama alivyodai. Hati hiyo namba AB202696 ilitolewa Dar es Salaam, Februari 15, 2007.
Lilipoibuka suala la umri Mratibu wa Miss Tanzania, Hashim Lundenga alisema: “Acha watu waseme, ni upepo tu utapita” na baada ya kuibuka kwa hati ya kusafiria aliita waandishi wa habari na kuonyesha cheti ambacho kimeibua mazito zaidi yanayoweza kulifikisha suala hilo mahakamani.
Uchunguzi wa FikraPevu umegundua kuhusishwa kwa vyombo zaidi vya serikali kutokana kuwapo kwa sheria tofauti zinazogusa suala hilo na taarifa zinasema, “uchunguzi ni mzito kuliko tunavyoweza kusema.”
Katika cheti cha kuzaliwa inaonekana kwamba Sitti ambaye ni binti wa Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu alikula kiapo kuomba cheti hicho.
Kusema uongo chini ya kiapo ni kosa la jinai.