Wahudumu wa afya ya msingi vijijini, wamelalamikia viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Bunda, kwa kile walichoikiita kutothamini kazi yao.
Rhobi Sira ambaye ni mhudumu wa afya katika kijiji cha Nyabehu, kilichopo kata ya Guta wilaya ya Bunda, anasema wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu bila malipo yoyote.
Anasema yeye kama mhudumu wa afya ya msingi anatakiwa kuzunguka katika kijiji kizima, kuhamasisha akinamama kuwapeleka watoto kupata chanjo na kuhakikisha, anaandika idadi ya watoto wanaozaliwa, lakini anasema pamoja na kufanya haya yote hakuna motisha yoyote wanayopata.
Naye Anastazia Otieno mhudumu wa afya kijiji cha Nyabehu, analamimikia hali hiyo ya kufanya kazi bila malipo, huku wakikosa hata sare za kazi na mafunzo yoyote, pamoja na kuwepo kwa mabadiliko mbalimbali katika utoaji wa huduma ya afya.
Wahudumu wa afya msingi katika kijiji cha Nyabuhe, Anastazia Otieno na Rhobi Sira wakiwa kazini
“Tuna watoto wanaotutegemea, na huku tunatakiwa kutenga muda kwa ajili ya kwenda kuwaelimisha akinamama, lakini Halmashauri yetu inatukatisha tamaa kwani hawatujali kwa chochote.” Anaeleza Anastazia.
Mratibu wa afya ya mama na mtoto wilayani Bunda Daines Lyimo amekiri kutowapatia malipo wahudumu wa afya msingi vijijini, lakini akaweka wazi mipango iliyopo kwamba mwaka huu wataanza kuwalipa.
“Tunatambua umuhimu wa wahudumu wa afya ya msingi, na tunawahakikishia kwamba mwaka huu wataanza kupata pesa yao.” Anaeleza Daines.