WAKATI Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na mkewe Anna wamemua kugawana mali, walinzi wa ya Kampuni ya New Imara Security Limited wanaolinda katika mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira Coal Mine uliopo kati ya wilaya ya Kyela, Rungwe na Ileje mkoani Mbeya, jana waligoma na kutishia kuacha wazi lindo hilo baada ya kushindwa kulipwa mishahara yao ya miezi sita mpaka sasa.
Mkapa na mkewe walihusishwa na kashfa ya ubinafsishaji wa mgodi wa Mkaa wa mawe wa Kiwira, kupitia kampuni yao ya ANBEM Limited ambayo waliungana na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na wanafamilia wengine kuchukua hisa za mgodi huo kabla ya kujitoa.
Wakizungumza na Fikra Pevu Jumatano iliyopita Februari 9 mwaka huu, walinzi hao walisema kuwa kugoma kwao kulitokana na kutolipwa mishahara yao na kumwandikia barua ya kusudio hilo Mkurugenzi wa kampuni hiyo Essau Kamwela ambaye pia ni makamu Mwenyekiti wa Chama cha wamiliki wa makampuni ya ulinzi Tanzania (TISIA) kanda ya nyanda za juu kusini lakini hawakutekelezewa madai yao.
‘’ Tumefikia hatua ya kugoma baada ya kutotimiziwa mahitaji yetu ya kulipwa mishahara ya miezi sita sasa na tulimwandikia barua Mkurugenzi wetu juu ya kusudio hili la kuachia lindo wazi endapo hatatulipa mishahara yetu kwasababu malalamiko yetu tunahisi yanapuuzwa hata na Serikali maana hata Mkuu wa wilaya ya Kyela anayajua malalamiko haya ’’ walisema walinzi hao ambao waliomba hifadhi ya majina yao .
Aidha walieleza kuwa Serikali imekuwa ikiwalipa wafanyakazi wa mgodi huo ili hali inajua kuwa nao wanapaswa kulipwa kwasababu kampuni hiyo imeingia mkataba na Serikali hali wanayohisi kuwa kuna ubaguzi kati yao na wafanyakazi wa mgodi huo.
Fikra Pevu ilimtafuta Mkuu wa wilaya ya Kyela Abadallah Kihato ambaye anadaiwa kupelekewa malalamiko na askari hao ambaye alikiri kupokea malalamiko hayo na kwamba alipokea pia taarifa za kugoma kwa askari hao jana.
‘’ Ni kweli nina taarifa za malalamiko ya askari hao wanaolalamikia kutolipwa mishahara yao na leo nimepata taarifa za kugoma kwao lakini nilipojaribu kuwasiliana na viongozi wa Wizara wamesema kuwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo ndiye anatakiwa kufuatilia mishahara hiyo kwasababu ndiye anayetambulika tofauti na wafanyakazi wa mgodi ambao wapo kwenye malipo ya Serikali moja kwa moja’’ alisema Kihato.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya New Imara Security Limited Essau Kamwela alipoulizwa kuhusiana na mishahara ya askari wake alikiri kutowalipa mishahara hiyo na kwamba ni kutokana na kampuni yake kutolipwa na Wizara ya Nishati na madini zaidi ya Shilingi Milioni 40.
‘’Ni kweli askari wanaidai kampuni yangu na ni kutokana na Wizara kutonilipa zaidi ya Shilingi Milioni 40 na askari wangu wanaolinda mgozi huo ni karibu 60 hivi na ninaendelea kufanya mawasiliano na Meneja wa Mgodi Adam Abdul ambaye ndiye aliyesaini mkataba wetu’’ alisema Kamwela.
Kuhusu mgomo walioufanya walinzi hao alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kwamba baada ya kupata taarifa hizo alizungumza na uongozi wa Mgodi na uongozi wa askari hao ambao kwa pamoja walikubaliana kufanya mazungumzo huku wakisubiri malipo kutoka Wizarani.
Jitihada za kumtafuta anayedaiwa kuwa ni Katibu wa Wizara hiyo David Jairo ili kuthibitisha madai hayo hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa kwa muda mrefu.
Habari hii imeandikwa na Gordon Kalulunga – Mbeya