Katika kukabiliana na changamoto ya mikopo katika elimu ya juu, wanafunzi waliokosa mikopo wametakiwa kuwasilisha maombi yao kwa asasi za kiraia ili wapatiwe fedha kwa ajili ya kugharamia masomo yao.
Kutokana na changamoto hiyo ya baadhi ya wanafunzi kukosa mikopo, Taasisi ya Msaada wa Kijamii Tanzania (TSSF) kama mdau muhimu wa maendeleo ya elimu nchini imeendelea na mchakato wa kutoa mikopo kwa wanafunzi ili kuwawezesha kutimiza ndoto zao za kitaaluma.
Hatua hiyo, inatokana na taarifa ya hivi karibuni ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kutoa bilioni 72 kwa wanafunzi wapya 21,677 kati ya 30,000 waliokidhi vigezo vya kupatiwa mikopo na bodi hiyo. Na wanafunzi 8,323 waliobaki watapata mikopo ya bilioni 36.6 ambayo itatolewa katika awamu inayofuata.
Mikopo hiyo inahusisha gharama za ada, chakula, maradhi, vitabu na vifaa vya shule, na inatolewa kwa mafungu kulingana na mahitaji ya mwanafunzi husika na masomo anayosomea.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji, Donati Salla inaeleza kuwa wamechukua uamuzi huo ili kuwasaidia wanafunzi ambao wamekosa mikopo kupitia HESBL kuwawezesha kupata elimu ya juu kama wanafunzi wengine.
Wanafunzi 61,000 walituma maombi kwa HESBL lakini mpaka sasa walio na uhakika wa kupata mikopo ni 30,000 pekee kutokana na serikali kutokuwa na fedha za kutosha kugharamia masomo ya wanafunzi wote wanaodahiliwa katika vyuo vikuu mbalimbali nchini.
Baadhi ya vigezo vilivyotumika kutoa mikopo ni wanafunzi waliopata nafasi katika vyuo vikuu, kuwa raia wa Tanzania, wawe wamemaliza kidato cha sita si kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita na vingine vyote vilivyoelekezwa na HESLB.
“Mkopo utagharamia asilimia 25, 50% na 75% ya ada ya chuo kulingana na mfumo wa malipo wa chuo husika. Waombaji watakaopewa kipaumbele ni wanafunzi ambao wanasomea fani ya ualimu, sayansi ya afya, sayansi asilia, viwanda, biashara na sayansia ya jamii”, anaeleza Donati Salla katika ripoti hiyo.
Licha ya juhudi hizo za Asasi za kijamii kuwawezesha wanafunzi kupata elimu bora itakayowakomboa kifikra na kuchangia katika maendeleo ya taifa, bado idadi kubwa ya wanafunzi waliodahiliwa katika vyuo mbalimbali huenda wasiendelee na masomo kutokana kukosa fedha za kugharamia masomo katika vyuo hivyo.
Msimamo wa HESLB ni kutoa mkopo kwa wanafunzi 30,000 ambao wamedahiliwa kwa mara ya kwanza katika vyuo vikuu na wale ambao wanaendelea na masomo yao. Kwa tafsiri rahisi ni kuwa wanafunzi wengine wanatakiwa kutafuta njia mbadara kujisomesha.
Kauli za Wabunge
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Hussein Bashe akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo Mei 13 mwaka huu aliliambia Bunge wamebaini wanafunzi wengi watakosa mikopo ya elimu ya juu licha ya kuwa na sifa zote za kusoma katika vyuo mbalimbali.
Alisema mwaka jana (2016/2017) wanafunzi 48,502 waliomba mkopo kwa HESLB lakini 25,555 tu ndiyo walipata mikopo na hivyo kuwaacha wengine 22,947 wakiwa hawana mikopo kutokana na bajeti iliyotengwa ya Sh. Bilioni 427.5 kutofikia mahitaji ya wanafunzi wote.
Bashe ambaye ni Mbunge wa Nzega Mjini (CCM) alisema mwaka 2017/2018, HESLB iliomba sh. Bilioni 427.5 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi sawa na bajeti ya mwaka jana ili hali ufaulu wa wanafunzi waliohitimu kidato cha sita umeongezeka kutoka asilimia 88 mwaka 2012 hadi asilimia 99 mwaka huu.
“Kamati inaona kwamba suala la elimu ya juu ni haki ya msingi kwa watu wenye sifa. Katika mwaka ujao wa fedha, wanafunzi wengi zaidi watakosa mikopo licha ya ufaulu wao mzuri”,
Kamati inashauri serikali kuongeza bajeti ya HESLB ili wanafunzi wengi zaidi wanaostahili kupata mikopo kwa maendeleo ya taifa letu, Alisema Bashe.