Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) limesema watoto milioni 77 ambao ni sawa na mtoto 1 kati ya 2 wanaozaliwa hawapati maziwa ya mama muda mfupi baada ya kuzaliwa ambapo wanakosa virutubisho muhimu, kinga ya mwili na kugusana na mama zao ili kuwakinga na magonjwa na vifo.
Wataalamu wa Afya wanashauri kuwa mtoto apewe maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa ili kumkinga na maambukizi ya magonjwa ya utotoni. Kutokana na sababu mbalimbali za kuchelewa kumnyonyesha mtoto baada ya kuzaliwa huwaongezea hatari ya kufa mapema kwa zaidi ya asilimia 80.
“Nilimzaa mtoto wangu nikiwa nyumbani, hakupata chanjo wala sikumyonyesha alipozaliwa”, hayo ni maneno ya Asha Maulid msichana wa miaka 17 mkaazi wa Mtwara ambaye ana mtoto wa miezi 6. Anasema mtoto wake anaumwa mara kwa mara na anatumia gharama kubwa kumtibu lakini hapati nafuu.
“Mwanangu anaumwa mara kwa mara, amedhohofika sina pesa ya kumpeleka hospitali na mimi nina maisha magumu sina uwezo kumtunza na kumpa lishe kamili”, amesema Asha.
Asha kama walivyo wasichana wengine ambao wanapata mimba za utotoni, wanakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo wa kuwatunza watoto wakiwa wadogo na kuwaweka katika hatari ya kushambuliwa na magonjwa na kufariki katika umri mdogo.
Anasema alikuwa anaishi Mtwara na mama yake lakini baada ya kupata mimba alifukuzwa nyumbani na alikimbilia Wilaya ya Mkurunga mkoa wa Pwani ambako huko alisaidiwa na dada mmoja aitwaye Monica na kujifungua mwezi Aprili mwaka huu. Kutokana na ugumu wa maisha alijifungulia nyumbani lakini tangu wakati huo mtoto wake hana furaha kwa sababu ya kukosa mlo kamili ana huduma muhimu za afya.
France Begin, Mshauri Mkuu wa Lishe wa UNICEF, anasema “Kuwaacha watoto kusubiri muda mrefu kabla ya kugusana na mama zao baada ya kuzaliwa kunapunguza nafasi ya watoto kuishi, kupata maziwa”, anaeleza katika ripoti ya UNICEF 2016 na kuongeza kuwa ikiwa watoto wote watanyonyeshwa maziwa ya mama na sio kitu kingine mpaka miezi sita, basi maisha ya watoto 800,000 yangeokolewa kila mwaka.
Mama akimnyonyesha mtoto wake
Takwimu za UNICEF zinaonyesha kuwa mikakati ya kuwawezesha watoto wanaozaliwa kupata maziwa muda mfupi baada ya kuzaliwa imepungua kwa miaka 15 iliyopita. Mfano katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, vifo vya watoto chini ya miaka 5 vimekuwa kwa kiwango cha juu kuliko maeneo mengine duniani.
Unyonyeshaji wa watoto muda mfupi baada ya kuzaliwa umeongezeka kwa asilimia 10 tangu mwaka 2000 katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika na hazijabadilika katika nchi za Magharibi na Afrika ya Kati.
Kulingana na ripoti ya Uchunguzi wa Lishe ya Taifa (NNS 2014) inaeleza kuwa mtoto 1 kati ya 2 walio na miezi 0 hadi 23 wanafaidika na mradi wa kunyonyeshwa maziwa ya mama. Lakini katika baadhi maeneo ya mikoa ya Tabora, Geita, Shinyanga, Rukwa na Katavi, unyonyeshaji wa maziwa kwa watoto uko chini ya 25%.
Inaelezwa kuwa kadiri mtoto anavyocheleweshwa kunyonyeshwa maziwa ya mama muda mfupi baada ya kuzaliwa hatari ya kufa katika miezi mitano ya maisha yake inaongezeka. Kuchelewa kunyonya kati ya saa 2 hadi 23 baada ya kuzaliwa kunaongeza hatari ya kufa kwa mtoto aliye na siku 28 kwa 40%. Hivyo hivyo kwa saa 24 au zaidi hatari huongezeka hadi asilimia 80.
UNICEF inasema kuwa maziwa ya mama ni kinga na ulinzi wa kwanza kwa mtoto dhidi ya udhaifu na magonjwa. Kukosa maziwa ya mama kunachangia karibu nusu ya vifo vyote vya watoto wachanga lakini maziwa ya mama yakiwekewa msisitizo italeta tofauti katika maisha na kifo kwa watoto.
Mila na Desturi, kukosa maarifa na kutoshirikishwa kwa wanawake wa Tanzania kunachangia kwa sehemu kubwa kwa watoto wachanga kutopata maziwa ya mama muda mfupi baada ya kuzaliwa. Pia kuwapa watoto vimiminika na chakula katika kipindi cha kwanza cha miezi sita ni sababu nyingine ya kuchelewa kuwanyonyesha watoto.
Mwakilishi wa UNICEF Tanzania, Maniza Zaman alinukuliwa na vyombo akisema wanaendelea kuweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha watoto na mama zao wanafaidika na program ya shirika hilo ya kuwanyonyesha watoto maziwa ya mama ili kuwaepusha na magonjwa na vifo vya utotoni.
Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 43 ya watoto wote walio chini ya miezi sita wanapata maziwa ya mama duniani kote. Watoto ambao hawapati maziwa ya mama kabisa wana uwezekano kufa mara 14 zaidi ya wale ambao wanapata maziwa ya mama pekee.
Ripoti ya NNS inaeleza kuwa 41% ya watoto walio chini ya miezi 6 walipata maziwa ya mama kwa mwaka 2014 nchini Tanzania. Katika baadhi ya maeneo ya Ruvuma na Tanga takwimu zinaonyesha kuwa ilikuwa ni chini ya 25%, huku Zanzibar ikiwa 20% lakini Pemba ikiwa chini ya 10% ya watoto wote waliokuwa wanapata maziwa ya mama kwa mwaka 2014.
Wataalamu wa Afya wanasema kuwa kiwango chochote cha maziwa ya mama kwa mtoto kinapunguza hatari ya kufa. Watoto ambao hawapati kabisa maziwa ya mama wana uwezekano mara 7 zaidi kufa kutokana na maambukizi ya magonjwa kuliko wale ambao wanapata maziwa ya mama katika kipindi cha miezi 6 ya kwanza ya kuzaliwa kwao.
Elimu zaidi inatakiwa kutolewa kwa wanawake na wauuguzi katika vituo vya afya na hospitali juu ya umuhimu wa maziwa ya mama kwa mtoto muda mfupi baada ya kuzaliwa. Pia mtoto anatakiwa kugusana na mama yake ili kuimarisha mahusiano na kumkinga na magonjwa ya utotoni
Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza:
Linapendekeza kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza katika maisha ya mtoto. Mama anatakiwa kupewa vyakula vyenye virutubisho muhimu.
- Mtoto anapaswa kuanza kunyonya ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa
- Mtoto lazima anyonye kulingana na mahitaji yake kila mara anapohitaji.
- Unyonyeshaji wa chupa unatakiwa kuepukwa