NAIBU Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo, amesema serikali iko bega kwa bega na akinamama wanaojihusisha na miradi ya kupambana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi na kwamba endapo kuna mtu katika idara zilizo chini ya wizara yake atakwamisha jitihada zao, basi akinamama hao wawasiliane naye moja kwa moja.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa Green Voices nchini Tanzania uliofanyika kwenye Hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Jaffo alisema kwamba, wizara yake ndiyo yenye jukumu kubwa la kuwawekea mazingira mazuri akinamama hao kutekeleza miradi yao chini ya halmashauri husika, hivyo akawaahidi kuwapatia ushirikiano wa kutosha kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu na suala la mazingira linapewa kipaumbele.
Naibu Waziri wa Tamisemi, Selemani Jaffo, akiongea katika uzinduzi huo wa awamu ya pili ya mradi wa Green Voices kwa akinamama.
Mradi wa Green Voices unatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Kigoma, Mwanza na Kilimanjaro, kukiwa na miradi 10 ikiwemo ya kilimo cha mihogo, kilimo cha matunda, uyoga, ufugaji wa nyuki, ukaushaji wa mbogamboga na utengenezaji wa majiko rafiki wa mazingira.
Akinamama walioanzisha miradi hiyo – miradi na mikoa watokayo vikiwa kwenye mabano –ni Regina Kamuli (Mkuranga, Pwani – Majiko Banifu), Abiah Magembe (Kisarawe, Pwani – Usindikaji wa Muhogo na Mtama), Magdalena Bukuku (Kinondoni, Dar es Salaam – Kilimo cha Uyoga), Mariam Bigambo (Dakawa, Morogoro – Ufugaji wa Nyuki), na Esther Muffui (Morogoro – Ukaushaji wa Mboga na Matunda).
Wengine ni Farida Makame (Kilimanjaro – Majiko ya Umeme-Jua), Leocadia Vedastus (Ukerewe, Mwanza – Kilimo na Usindikaji wa Viazi Lishe), Monica Kagya (Kisarawe, Pwani – Ufugaji wa Nyuki), Dkt. Sophia Mlote (Kinyerezi, Dar es Salaam – Kilimo Hai cha Nyanya na Mbogamboga), na Evelyn Kahembe (Uvinza, Kigoma – Kilimo cha Matunda).
Kupitia miradi hiyo, zaidi ya wanawake 300 wamepatiwa mafunzo mbalimbali huku program nyingine za mafunzo kwa vitendo zikiendelea katika makundi yao.
“Serikali ya Tanzania na hasa wizara hii, na wizara hii Mheshimiwa Rais mwenyewe ni wizara yake, naomba niwahakikishie kwamba tutashirikiana na Green Voices kwa nguvu zote na nitawapa pasiwedi ya kuwasiliana na ofisi yangu moja kwa moja ili kama mnakwama mambo yenu yaweze kwenda huko katika halmashauri mlipo,” alisema Jaffo, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisarawe mkoani Pwani.
Akaongeza: “Nitawaunganisha na mkurugenzi maalum wa idara za serikali katika wizara yangu, kwamba ninyi mkikwama katika halmashauri kwa jambo lolote lile mnawasiliana naye moja kwa moja mradi mambo yenu yaweze kwenda mpate sapoti, sauti ya wanawake iweze kusikika, mambo ya mazingira yaweze kubadilika, kilimo, mifugo na kadhalika ili mwisho wa siku watu waseme kwamba kuna kundi la watu walikwenda Hispania na wakajifunza wakaleta mabadiliko nchini.”
Aidha, Naibu Waziri Jaffo alisema kundi hilo la akinamama wa Green Voices ni muhimu na serikali itahakikisha inawaunga mkono kwa kila hali.
"Ninyi ni kioo cha jamii na watu wengi wanatakiwa wajifunze kutoka kwenu. Kumbukeni, katika suala la mazingira maeneo mengi yameathirika sana, mnaweza kuona jinsi maeneo mengi yanavyokumbwa na mafuriko kutokana na watu kukata miti na kuharibu mazingira, wakati mwingine tunashuhudia ukame wa kutisha.
“Kwahiyo ninyi mradi wenu unakwenda kukabiliana na changamoto hizi, ni muhimu sana, mna wajibu mkubwa sana kwa sababu suala la mazingira ni muhimu na linaathiri dunia.
“Tunatakiwa tutoke katika miradi isiyo halisi (artificial projects) na kwenda kwenye miradi halisi ili tuweze kubadilisha maisha ya watu.”
Vile vile, aliwaasa akinamama hao kwamba, wakienda huko waongee lugha rahisi na wananchi ili iwe rahisi kueleweka.
“Ninyi hapa wote ni wasomi, lakini mkienda huko ongeeni lugha rahisi ili mwananchi wakawaida akisikia aweze kuielewa na kuleta mabadiliko ya kweli. Mama mwingine hajasoma hata darasa moja na inawezekana kuwepo kwako wewe kukabadili maisha yake,” alisema.
Mmoja wa washiriki wa mradi wa Green Voices, Mariam Bigambo, mkulima wa Mvomero ambaye amejikita katika ufugaji wa nyuki akiwa na kikundi cha wanawake 15, alisema kwamba licha ya umuhimu wa mradi huo, lakini wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinakwamisha maendeleo yao.
“Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo ni kushushwa kwa mizinga yetu na watu wasiojulikana kwa sababu tumeiweka porini,” alisema na kuongeza: “Kila mara tunakuta mizinga yetu imeshushwa, tumekwishatoa taarifa kwa serikali ya kijiji pamoja na kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na hata Polisi.”
Aidha, alisema kwamba, ufugaji wa nyuki unahitaji uvumilivu na mpaka sasa baadhi ya wanakikundi wamevunjika moyo kwa sababu bado hawajanufaika na matunda ya kazi yao.
Kutokana na hali hiyo, alisema, wameamua pia kugeukia kilimo cha uyoga ili kuongeza tija.
Mratibu wa mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Secelela Balisidya, alisema awamu ya kwanza ya mradi huo ililenga katika uanzishwaji na uzalishaji, lakini awamu ya pili inalenga kuwapatia stadi akinamama ili kuboresha bidhaa wanazozizalisha ili ziongezeke ubora la kuwaletea tija.
“Hivi sasa katika awamu ya pili akinamama watapatiwa mafunzo ya namna ya kutengeneza bidhaa zao kama vifungashio ili kuongeza ubora na thamani na tunataka bidhaa zao ziingie sokoni katika viwango ambavyo vinakubalika,” alisisitiza.
Akizungumza katika uzinduzi huo wa awamu ya pili, Mratibu wa mradi wa Green Voices kutoka Hispania kutoka taasisi ya Women for Africa Foundation inayodhamini mradi huo, Alicia Cebada, alisema wamefarijika na mradi huo kwa kuwa umeonyesha mafanikio makubwa nchini Tanzania katika awamu ya kwanza na ndiyo maana wameamua kuwaongezea uwezo akinamama hao katika awamu hii.
“Tumekuwa tukiwasiliana mara kwa mara na Secelela (Mratibu wa Green Voices Tanzania) kuhusu mafanikio na changamoto za mradi huu na kwa kweli tunafarijika kuona miradi yote inakwenda vizuri,” alisema Alicia.
Alisema, changamoto pekee ambayo ipo mbele yao ni kuhakikisha miradi hiyo inasimama na kuwafundisha wanawake wengi kadiri wawezavyo ili kuhakikisha wanajiletea maendeleo katika maeneo yao kiuchumi na kijamii.
Mwaka 2016 rais wa mfuko wa Women for Africa Foundation, Mama Maria Tereza Fernandez de la Vega, alizuru nchini Tanzania na kushiriki uzinduzi wa mradi huo Julai 11, 2016 ambapo ulizinduliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan.
Katika uzinduzi huo, Mama Samia aliahidi kwamba serikali yake itahakikisha inakuwa bega kwa bega kusaidia miradi hiyo iwe endelevu ili kuunga mkono juhudi za utunzaji wa mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kuongeza uhakika wa chakula, kuwakwamua wananchi na umaskini pamoja na kuongeza ajira, hasa kwa wanawake.
Kwa upande wake, Mama Maria Tereza, ambaye ni makamu wa rais mstaafu wa Hispania, alieleza kufurahishwa kwake na jitihada za akinamama wa Tanzania na kusema taasisi yake inaangalia namna ya kuwasaidia zaidi.