BAADHI ya wanawake waliohojiwa mkoani Kigoma wamelalamikia waume zao kuwa kikwazo kwao kujiunga na uzazi wa mpango kwa kuwa wao wanawachukulia kama chombo cha kuongeza familia kwa kuzaa watoto wengi kadiri inavyowezekana.
“Wanaume wengi hawana elimu ya uzazi wa mpango na wengi bado wanakumbatia mila na desturi za zamani eti mwanamke anaolewa ili aje kuongeza familia ya upande wa mume, hivyo ukimhusisha suala la kupanga uzazi anasema zaa mpaka watoto waishe tumboni,”anasema Bi.Magdalena Simon mkazi wa wilaya ya Kibondo.
Bi.Fortunata Leonard pia mkazi wa wilaya ya Kibondo anasema baadhi ya kina Baba bado hawana elimu ya uzazi wa mpango na kwamba neno la Mungu alilosema kuwa zaeni muijaze dunia linawagharimu sana akina mama kwa kujikuta wakiambiwa na waume zao kuwa kazi ya wanawake ni kuzaa na ndio maana wanawake waliopata elimu ya uzazi wa mpango huwaficha waume zao.
Je Ni kweli maandiko haya yanamaanisha binadamu kuzaana kwa wingi. Na je hivi ndivyo viongozi wa kidini wanavyohubiria waumini wao?
Mchungaji Naftari Nkilaha kutoka kanisa la Anglikana Kibondo mjini, anasema ni kweli mwanadamu alipewa uwezo wa kuendeleza uumbaji hapa ulimwenguni lakini kwa njia nzuri.
“Hata katika kuzaa lazima mwanadamu aangalie anazaaje, je wale watoto atakaowazaa anaweza kuwasaidia waweze kusimama katika nafasi yao kutimiza mpango wa Mungu,”alisema Mchungaji Naftari.
Anasema sio kwamba wachungaji wanahubiri watu kuzaa kiholela kwa kuwa Mungu hawezi kuwapongeza wazazi ambao watazaa watoto wasiwe na afya nzuri, wasiende shule ama wapoteze maisha na kwamba hilo halikubaliki mbele za Mungu, ingawa anasema wako wahubiri wengine wanatafsiri vibaya maandiko.
Je nini kifanyike?
Ili kuendelea kupunguza vifo vya kina mama vinavyotokana na uzazi mchungaji Naftari Nkilaha anasema kuwa kuna haja ya kuelimisha jinsia zote wanaume na wanawake na kuongeza kuwa mapendekezo yatolewe kwa makundi yanayoelimisha jamii kwa maana ya shule na taasisi mbali mbali za kiraia na zisizo za kiraia.
Ikiwezekana sera ya uzazi wa mpango iwekwe kwenye mitaala mashuleni na wapatikane walimu watakaokuwa wakifundisha somo linalohusu uzazi wa mpango ili mtoto wa kike na wa kiume aweze kufahamu masuala yahusuyo afya ya uzazi akiwa mdogo.
Kwa upande wake Bi.Martha Jerome kutoka Women’s Promotion Centre anasema jamii iachane na mila zote zilizopitwa na wakati na jamii ione umuhimu na ustawi wa mwanamke na mwanaume na mtoto ndani ya familia.
Serikali ishirikiane na asasi zisizo za kiserikaali kuhakikisha kuwa elimu inatolewa kwa watoa huduma wa ya afya ya uzazi ikiwemo uzazi wa mpango na pia jamii iweze kuelimishwa zaidi kuhusu faida na umuhimu wa kupanga uzazi.
Kuwepo na huduma za uzazi wa mpango za kutosha kwa sababu kuna maeneo mengine huduma za uzazi wa mpango hazipatikani kwa kuwa dawa hazipo.
Vifaa vya kutosha viwepo ili watu wakishaelimishwa na wakahitaji huduma waweze kuipata tofauti na hali ilivyo hivi sasa.
Ili kuondokana na tatizo hilo ipo haja kwa serikali kulipa kipaumbele suala la uzazi wa mpango kwa kuongeza bajeti yake ili kuwezesha huduma kupatikana kwa wingi katika kliniki, vituo vya afya na hospitali pote nchini.
Mwaka 2011/12 Serikali ya Tanzania ilitenga shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya dawa za uzazi wa mpango lakini hadi kufikia juni 2012 haikuwa imetoa chochote.
Katika mkutano wa London juu ya uzazi wa mpango mwaka 2012, Rais kikwete alibainisha juhudi ambazo Tanzania inaendelea kuzifanya kuboresha huduma za uzazi wa mpango
Kwa mujibu wa Shirika la Maendeleo ya Watu Tanzania (HDT), katika kipindi cha 2010/11, fedha zilizotakiwa ili kufikia malengo ya asilimia 60 ya matumizi ya dawa za uzazi wa mpango ifikikapo 2015 ni shilingi billioni 19.
Lakini Serikali ilipanga kutoa shilingi billion 3, sawa ma asilimia 16 tu ya mahitaji. Hivyo, kama serikali itaendelea kutoa fedha hizo kwa kusuasua, Tanzania haiwezi kufikia malengo ya millennium hasa namba 4 na 5, kupunguza vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano na Kuboresha upatikanaji wa jumla wa huduma za afya ya uzazi ifikapo 2015.
Kulingana na shirika la health promotion hatua za kisera zinazopaswa kuchukuliwa na serikali ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa sera inayowahakikishia wanawake masikini wa vijijini huduma za uzazi wa mpango.
Kuziagiza halmashauri zote kuweka huduma za uzazi wa mpango kuwa kipaumbele katika mipango yao ya maendeleo na bajeti kwa kutumia chombo au mfumo wa kutengeneza mipango na bajeti, kuhimiza huduma za uzazi wa mpango za kuwafikia watu walipo kwa kupitia mifumo ya kijamii.
Tanzania ikoje?
Tanzania ni mojawapo ya nchi ambazo zina viwango vya juu vya vifo vya wanawake vitokanavyo na matatizo ya uzazi.Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa mwaka 2010 na Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) karibu wanawake 20 hufariki kila siku kutokana na matatizo hayo nchini.
Na zaidi ya hili ni muhimu kujua kwamba zaidi ya akina mama 250,000 wanapata vilema vya kudumu kila mwaka kutokana na matatizo ya uzazi .Idadi hii ni kubwa, inatisha na inahitaji dhamira ya dhati kuondokana na tatizo hili.
Kutokana na hali hiyo nchi imejiwekea malengo ya kupunguza kiwango cha vifo kutoka 454 kwa kila wanawake 100,000 hadi 193 ifikapo mwaka 2015.
Mikakati kadhaa imewekwa kufikia malengo hayo; kuongeza matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango ili yafikie asilimia 60, ambapo kwa sasa ni asilimia 27 tu ya wanawake walioolewa ndio wanaotumia njia hizo.
Ufafanuzi uzazi wa mpango
Martha Jerome ni mratibu kutoka shirika la Women’s Promotion Center Mkoani Kigoma, anasema uzazi wa mpango ni uamuzi wa hiari wa mtu au wenza juu upangaji wa Familia. Akifafanunua anasema kuwa nimpangilio wa kuzaa kati ya uzazi mmoja na mwingine, idadi ya watoto wa kuzaa na lini waache kuzaa pamoja na kuzuia wingi wa mimba unaodhaniwa kuleta madhara ya aina moja au nyingine.
Anasema kupanga uzazi hakuishii kwa watoto kupishana umri tu kama ambavyo wengi wanadhani bali pia ni kuwa na uwezo wa kuwahudumia watoto hao na kuongeza kuwa umri wa kuzaa unaoshauriwa ni kati ya miaka 20 hadi 35.
Kulingana na wataalam wa Afya, pamoja na kumuwezesha mama na mtoto kuwa na afya njema, uzazi wa mpango una faida nyingi kwa wanawake, wanaume, watoto, familia na jamii kwa ujumla. Unamsiadia mama kurudi katika hali yake ya zamani ambayo ilitikiswa na hali ya ujauzito, uchungu na kujifungua.
Mama atakuwa mwenye nguvu, afya nzuri na mchangamfu na pia atakuwa na muda mzuri wa kurudisha afya yake kabla ya kupata ujauzito mwingine.Katika hili Mama anapata muda wa kutosha wakujishughulisha na mambo mengine ya kiuchumi na kimaendeleo kwa ajili ya familia na jamii kwa ujumla.
Licha ya faida zinazotajwa kutokana na uzazi wa mpango bado kuna idadi ndogo ya watu wanaotumia njia za uzazi wa mpango mkoani Kigoma. Mkoa huu kwa mujibu wa takwimu zilizopo ni asilimia 12 ndio wamo katika harakati za uzazi wa mpango na wengine wanasita kutokana na kuona madhara.
“Njia za uzazi wa mpango nazo zina miiko yake, sio kuchukua tu kutafuna kama Karanga. Kuna watu wengine wakiwa na dalili Fulani hawatakiwi kutumia dawa za uzazi wa mpango na kama akitumia ni lazima apate maelekezo, lakini ni wapi akapate ushauri, hakuna,”alisema Bi.Martha.
Kwa mujibu wa Bi.Martha Jerome wanawake wengi wanaogopa kutumia njia za uzazi wa mpango kwa kuogopa madhara ambayo wengine huwapata au kusikia kutoka kwa ndugu au rafiki zao.
Mfano halisi anasema ni Bi.Subira Maulid, Mama wa watoto watano ambaye aliamua kwenda kupanga uzazi ambapo alichagua njia ya Sindano. Kwa kuwa hakupata ushauri au kupimwa ili kuona ni njia gani sahihi kwake yeye kutumia aliishia kupata madhara hivyo anasema hawezi tena kupanga uzazi.
“Hata kama mtu akija na kunipa hela zimejaa boksi anishawishi kujiunga na njia za uzazi wa mpango siwezi kwenda kwa sababu zimeniletea madhara,”alisema Bi.Subira.