ExxonMobil (Marekani)

• Aina: Kampuni ya Umma

• Imeandikishwa: Soko la Hisa la Marekani

• Kuanzishwa: 1999

• Makao Makuu: Texas, Marekani

• Wahusika Wakuu: Rex Tillerson (Mwenyekiti na Afisa Mkuu)

• Kipato: Dola za Marekani bilioni 411.94 (2014)

• Faida Halisi: Dola za Marekani bilioni 41.06

• Asilimia ya Mabadiliko Mwaka uliopita: +34.8%

• Jumla ya Uwekezaji: Dola za Marekani bilioni 349 (2011 mwishoni)

• Jumla faida ya Uwekezaji: Dola za Marekani bilioni 154.4

• Waajiriwa: 75,300

• Tovuti: www.ExxonMobil.com

Mwaka 2012 ExxonMobil ilishika nafasi ya kwanza miongoni mwa kampuni kubwa za Marekani katika orodha ya Fortune 500, taasisi inayotazama mapato ya kampuni. Mwaka 2014 ilishika nafasi ya nne katika kampuni 10 bora duniani. Ilianza kama Standard Oil Company mwaka 1982 na ikawa ExxonMobil mwaka 1999 baada ya muungano wa kampuni mbili za Standard Oil ya John D. Rockfeller na Exxon & Mobil. ExxonMobil ina vitengo kadhaa na mamia ya washirika wenye majina yanayojumuisha ExxonMobil, Exxon, Esso au Mobil.

Mwishoni mwa mwaka 2011, kampuni ilikuwa inamiliki akiba iliyothibitishwa ya mapipa bilioni 24.9 ya mafuta wakati wastani halisi wa uzalishaji ulikuwa mapipa milioni 4.5.

exxonmobil-gate

Mwaka 2008 wakati bei ya mafuta ilipopanda duniani, ExxonMobil ikawa kampuni inayothaminiwa zaidi kuliko zote duniani wakati hisa zake zilipoongezeka kwa asilimia 40 ndani ya mwaka mmoja. Mwaka 2010 waliinunua kampuni ya XTO Energy, iliyokuwa ikiongoza katika uendelezaji wa rasilimali zisizo za kawaida, ikiwemo mafuta na gesi ya kwenye miamba laini ambayo inahitaji utaalamu wa hali ya juu katika uchimbaji wake. Mnamo Agosti 2011, Exxon iliingia ubia wa dola bilioni 3.2 na Rosneft kuendeleza utafiti katika bahari ya kina kirefu, wenye hadhari ya hali ya juu, katika eneo la Arctic na Bahari Nyeusi ya Urusi.

Ripoti ya ExxonMobil ya mwaka 2010 inaonyesha kwamba mtaji na matumizi ya utafiti kwa mwaka huo vilifikia dola bilioni 32.2, na kwamba kampuni hiyo ilipanga kuwekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni 165 kwa miaka mitano iliyofuata.

Thamani ya mtaji kwa kampuni iliongezeka kwa asilimia 12.9 kufikia dola bilioni 364 mwaka 2010 wakati wa ongezeko la bei ya mafuta, baada ya kushuka mwaka 2009. Faida halisi pia iliongezeka kwa asilimia 58 kutoka mwaka 2009 kufikia dola bilioni 30.46, lakini ikiwa pungufu ya faida ya 2008 ya dola bilioni 45.2. Takwimu hizo zinajumuisha rekodi ya mapato ya kemikali.

ExxonMobil yaingia Tanzania

Kampuni ya Uzalishaji na Utafiti ya ExxonMobil Tanzania (ExxonMobil Exploration and Production Tanzania Limited – EMEPTL) inamilikiwa na ExxonMobil yenye asilimia 35 ya hisa katika eneo la Kitalu namba 2 kwenye bahari ya kina kirefu kutoka mwambao wa Tanzania, ambacho kinaendeshwa na Statoil Tanzania yenye asilimia 65 ya hisa. EMEPTL ni kampuni iliyoanzishwa Tanzania Februari 2, 2010 na kupewa cheti cha usajili Namba 74849.

Taarifa ambazo FikraPevu inazo zinaeleza kwamba, EMEPTL na washirika wake wamekamilisha ugunduzi wa maeneo manne ya gesi asilia hadi sasa yenye futi za ujazo trilioni 21. Ugunduzi huo uko kwenye maji yenye kina cha mita 2,500. Ushirika wa Statoil na ExxonMobil umetangaza ugunduzi wa tano wa gesi katika eneo la Kitalu Namba 2 mbali na Pwani ya Tanzania. Ugunduzi huo ni wa kati ya futi za ujazo trilioni 2 na 3 za gesi iliyopo kwenye kisima cha Mronge-1.

Statoil na ExxonMobil wamefanya ugunduzi mwingine mkubwa wa gesi mbali na mwambao na wanapanga kuanza uchimbaji wakati wowote kuanzia sasa na kuweka hai matumaini ya Tanzania kuwa msafirishaji mkubwa wa gesi nje ya nchi. Kampuni hizo zimekuta futi za ujazo trilioni 2 hadi 3 za gesi iliyopo, au mapipa milioni 360 hadi 560.

Taasisi ya Offshore Energy iliripoti kwamba Statoil na ExxonMobil wamefanya ugunduzi mwingine mkubwa katika eneo tarajiwa la Piri-1, ukiwa ni ugunduzi wao wa sita.

Ugunduzi huo umeleta jumla ya ujazo uliopo kufikia takriban futi za ujazo trilioni 20 kwenye eneo la Kitalu namba 2. Kisima cha Piri-1, kilichochimbwa na meli ya kuchimbia ya Discoverer Americas, kipo kilometa 2 kusini magharibi mwa kisima cha Lavani-1 ndani ya mita 2,360 za maji. Discovery Americas sasa inachimba eneo tarajiwa la Binzari kwenye Kitalu namba 2.

Mnamo mwaka 2012 na 2013, ExxonMobil na Statoil zilifanya ugunduzi mkubwa wa gesi katika visima vya Zafarani, Lavani, Tangawizi na Mronge kwenye eneo la Kitalu namba 2, lenye kilomita za mraba takriban 5,500 na lipo katika kina cha maji kati ya mita 1,500 hadi 3,000. Ugunduzi huo umethibitisha futi za ujazo trilioni 17 hadi 20 za ujazo uliopo na unaonyesha hatua muhimu kuelekea uwezekano wa maendeleo ya uzalishaji gesi asilia nchini Tanzania.