Zitto, Mnyika walishangaa Bunge; “Liko ‘out of touch’ na wananchi asema Zitto!

Jamii Africa

Katika taarifa yake katika mitandao mbalimbali ikiwamo blogu yake, Zitto amesema inasikitisha kwamba Bunge laweza kukaa wiki nzima na kujadili masuala mbalimbali bila kutoa muda kujadili suala la mtikisiko katika sekta Afya. Kabla ya Zitto, wabunge kadhaa walitaka maelezo kwa serikali lakini Naibu Spika, Job Ndugai, alitumia kanuni za Bunge kupooza hoja za wabunge hao akiwamo Mbunge wa Wawi (CUF) Hamad Rashid Mohamed aliyetaka serikali kuchukua hatua za haraka.

Hata hivyo, akisitisha shughuli za Bunge Alhamis mchana, Naibu Spika amesema anatarajia serikali itatoa tamko kesho Ijumaa, vinginevyo Bunge litaendelea kujadili suala hilo bila ya kuwapo taarifa hiyo ya serikali.

Zitto ambaye katika siku ya kwanza ya kikao cha Bunge alitoa hoja ya kutaka serikali kutoa taarifa ya hali ya ilivyo katika sekta ya afya kutokana na mgomo wa madaktari, amesema alishangazwa na Spika, Anne Makinda kusema serikali itatoa taarifa ambayo hadi sasa bado.

“Siku ya kwanza ya Bunge nilisimama kutaka taarifa ya serikali kuhusu mgomo wa madaktari na taarifa hiyo ijadiliwe na Bunge. Spika akalojulisha Bunge kwamba Serikali imempa taarifa na itawasilishwa.

“Bunge likaahirishwa siku hiyo  bila kurejea. Kamati ya Uongozi ya Bunge ilipohitaji taarifa ya Serikali, Serikali haikuwa na taarifa. Kwa hiyo walifanya ujanja ujanja kuzuia mjadala wa mgomo wa madaktari,” anasema Zitto na kuendelea;

“Leo wabunge kwa mara nyingine wamesimama kutaka mjadala huu wa dharura. Naibu Spika wa Bunge akatumia sababu za kiufundi kuzuia mjadala. Inawezekana wabunge hawakuwaandaa wabunge kusimama kuunga mkono hoja, lakini ni jukumu la Kiti kuona umuhimu na udharura wa mijadala.”

Akiwa mmoja wa Wabunge wanaofuatilia sana mijadala ya mtandaoni, Zitto liendelea kwa kusema;

“Hii inadhihirisha kwamba sasa Bunge kama Mbunge mmoja mmoja au kwa ujumla wake na Taasisi ya Bunge imekosa mguso na Hali ya wananchi (out of touch).

” Hali hii ni hatari sana. Wananchi wanapoona chombo kinachowawakilisha hakitoi nafasi kwa masuala yanayowagusa, watachukua hatua zao wao wenyewe na hivyo kuhatarisha utulivu wa nchi. Bunge liache shughuli nyingine zote na kutoa fursa ya kupokea taarifa ya serikali kuhusu madai ya Madaktari, kuijadili na kuazimia kwa kuelekeza hatua za kutekelezwa na serikali.”

Naye Mbunge wa Ubungo Bw. John Mnyika naye akiandika katika mtandao wake (blogu) kuelezea kilichojiri Bungeni amesema kuwa Naibu Spika alitumia vibaya kanuni za Bunge kuzima mjadala wa mgomo wa madaktari. “Asubuhi ya leo Naibu Spika Job Ndugai alitumia kanuni vibaya kuzuia hoja ya dharura bungeni kuhusu mgomo wa madaktari. Kimsingi, sikuwasilisha hoja ila niliomba muongozo wa Spika ili niweze kupatiwa nafasi ya kuwasilisha hoja ya dharura.”

Bw. Mnyika ameendelea kusema kuwa “Kwa kuwa hoja kama hiyo iliwasilishwa juzi na ikaungwa mkono lakini Spika akasema ameshakubaliana na serikali kuwa ingewasilisha kauli. Hata hivyo, jana hakukuwa na kauli ya serikali huku wananchi wakiendelea kupata madhara ya mgomo. Hivyo nikata muongozo kwa kuwa Spika alitumia kanuni ya 49 (2) ambayo kimsingi inatoa mwanya kwa kauli ya serikali kuwasilishwa kwenye wakati atakaoona yeye kuwa na unafaa juu ya jambo linaihusu serikali na lisilozua mjadala. Nilitaka kanuni hiyo isitumike badala yake wabunge tutimize wajibu wa kuisimamia serikali kwa kutumia kanuni ya 47 kuhusu hoja ya dharura. Kwa kuwa ilikuwa muongozo hakukuwa na hitaji la kikanuni la wabunge wengine kuunga mkono lakini akaamua kuilinda serikali kwa kuwa hawakuwa wamejiandaa” ameandika Mnyika.

Pamoja na hilo kwa mujibu wa Mnyika “Lakini mwishoni (Ndugai) ameahidi kuwa kauli ya serikali itatolewa kesho.”

Taarifa kamili ya Zitto:

http://wp.me/pRboX-sO

Tovuti ya Mnyika

Na. M. M. Mwanakijiji

1 Comment
  • kweli wabunge wengi wanafuata mkumbo mfno CCM ni kukaa bungeni kupiga makofi na kulaa na kupiga stori huku sisi CHADEMA tukiangaika na wananchi wetu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *