AHADI ya Idara ya Uvuvi ya kuwapatia wavuvi wa Makoongwe, Pemba boti za injini na nyavu za kuvulia bahari kuu, haijatekelezwa kwa miaka mitatu sasa.
Idara ya uvuvi ambayo ni ya serikali, ilileta mpango huo ikiwa na shabaha ya kusitisha uvuvi kwenye maeneo karibu na mwambao kwa kile ilichoita “kuzuia uvuvi unaoharibu mazalia ya samaki na viumbe wengine wa bahari.”
Maeneo yaliyotengwa yaliitwa “maeneo tengefu” ambako sasa ni marufuku kuvua. Idara ilielekeza watu wote kuvua kwenye bahari kuu – mbali na mwambao.
Kwa kupitia mradi wa MACEMP–Marine and Costal Area Envirnment Menagement Programe iliwataka wavuvi kuunda vikundi ili iweze kuwapatia boti zenye mashine na nyavu za kuvulia katika bahari kuu, ikiwa njia ya kujipatia kipato.
Hata hivyo, pamoja na wavuvi kupokea amri ya kusitisha uvuvi karibu na mwambao na hata kuunda vikundi vya ushirika, kwa matumaini makubwa, utekelezaji wake umekuwa kinyume na matarajio yao.
Hali hii ya kutotekelezewa ahadi imewakumba wananchi wapatao 2,000 wa kisiwa cha Makoongwe kilichopo wilaya ya Mkoani katika mkoa wa Kusini Pemba.
“Sisi hatuna kipato, kwa maana ya kitu cha kutuletea chakula na hata fedha kwa matumizi yetu” anaeleza kwa sauti ya uchungu.alisema sheha wa shehia hiyo Ali Muhammed Haji.
Akielezea utekelezwaji wa mipango ya utoaji wa vifaa vya kuvulia na uwekwaji wa eneo maalum kwenye bahari ya karibu ili kulinda mazalia ya bahari, Muhammedamesema taratibu zote za kutengeneza boti, kununua vifaa vya kuvulia na mashine zilifanywa na idara ya uvuvi kupitia mradi wa MACEMP bila kuwashirikisha wavuvi wenyewe.
Alisema kawaida, kwa kuwa wavuvi ndio wanaifahamu bahari kuu na mahitaji ya chombo cha uvuvi kinachofika huko, walitarajia kuwa wao ndio wangeulizwa ni boti yenye ukubwa gani, au uwezo gani inayohitajika; lakini haikuwa hivyo.
Haji alisema kutoshirikishwa huko kwa wavuvi katika kufanya maamuzi juu ya ununuzi wa vifaa; au juu ya mambo yanayohusu hifadhi ya mazingira ya bahari, kunaweza kupelekea kutofikiwa kwa malengo ya mpango wa maeneo tengefu.
Chini ya mpango wa Marine and Costal Area Envirnment Menagement Program(MACEMP), wavuvi huzuiliwa kufanya shughuli zozote za uvuvi katika maeneo ya yaliyotengwa isipokuwa katika bahari kuu.
Aidha, alisema ikiwa wananchi hawatashirikishwa na kuwezeshwa kufikia bahari kuu, wanaweza kuendelea, hata kwa uficho, kuvua kwenye eneo maalum la kulinda maliasili za baharini.
Inakadiriwa zaidi ya watu (1000) ya wakaazi wa shehia ya Makoongwe hujishughulisha na kazi za uvuvi zikiwa njia kuu yao ya kujiletea kipato.
Kazi hizi zimekuwa zikifanywa na wanaume ambao huvua kwa kutumia nyavu, mishipi au vichokoa. Wanawake wamekuwa wakijishughulisha na uvuvi wa kombe na chaza waishio kwenye matumbawe.
Wananchi wachache wasiojishughulisha na uvuvi, hufanya kazi za kilimo katika ardhi ndogo iliyomo ndani ya kisiwa hicho.
Kwa miaka nendarudi, wavuvi wamefanya shughuli zao kwa kutumia nyanvu za macho makubwa na madogo, mishipi na madema katika pwani ya karibu na ya mbali ya kisiwa hicho bila uingiliaji wowote.
Kwa wavuvi hawa, hizo zilikuwa nyakati bora kwao. Bali dalili za kupungua samaki na kuwepo kwa uharibifu wa mazingira ya bahari ambayo ni kuharibu mazalia ya samaki wadogo na matumbawe kumeifanya hali kubadilika alisea mataala wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi Sharif Mohammed.
Kwa wavuvi wa Makoongwe hali ilibadilika baada ya kuanzishwa kwa Mradi Pemba Chanel Conservation Authority (PECCA)na ule wa ukanda wa pwani, Marine and Costal Area Envirnment Menagement( MACEMP). Miradi hii imekuwa ikisimamiwa na Idara ya Uvuvi Pemba kwa miaka minne sasa.
Ni miradi hii iliyoleta amri ya kusitisha uvuvi kwa kutumia nyavu za kukokota (makokoro); kuacha kuvua katika bahari ya karibu na kusababisha kuwepo eneo maalum la kulinda maliasili bahari.
Haji Mcha Makame, mvuvi na msimamizi wa maeneo maalum ya maeneo tengefu katika kisiwa cha Makoongwe amesema mpango wa maeneo tengefu ni mzuri lakini wavuvi hawakupewa fursa ya kutosha kuamua njia bora ya kuutekeleza wala njia mbadala ambayo ni kupewa zana za uvuvi mbali na mwambao.
Alisema kwa kushindwa au kukataa kushirikisha wananchi wahusika, baadhi ya vifaa vilivyonunuliwa kupitia mradi wa Marine and Costal Area Envernment Menagement Program (MACEMP), kama vile boti, haviwezi kufanya kazi iliyokususdiwa.
Haji alitaja baadhi ya vifaa ambavyovilinunuliwa miaka minne iliyopita lakini havitumiki kutokana na kutokukidhi ubora. Hali alisema boti iliyogharimu Sh. 3,700,000/=,mashine ya boti ya Sh. 3,500,000/= na mishipi na ndoana vya thamani ya Sh. 700,000/= kwa ajili ya kikundi cha uvuvi cha Roho Haikongi, havina uwezo wa kuvua bahari kuu.
Haji Mcha Makame, ambaye ni mwanachama wa kikundi hicho cha ushirika chenye wavuvi 10, alisema vifaa vilivyokusudiwa kusaidia kikundi vimeegeshwa ufukweni bila matumizi yeyote kwa sababu “havina sifa ya kufanya kazi iliyokusudiwa.”
Akifafanua sifa zinazotakikana, Makame alisema sharti iwe boti kubwa yenye mashine kubwa na inayoweza kuhimili vishindo vya bahari kuu ambapo alisema ukubwa wa uzito wazana za uvuvi zinategemea na bahari yenyewe ikoje .
Nae Mkuu wa Idara ya Mkoani Jabu Khamis Mbwana alisema vifaa vyote vya uvuvi huwa vinanunuliwa kupitia mgawanyo wa watu wakiwemo wavuvi wenyewe na wataalam pamoja na wakuu wa Idara hiyo ya uvuvi.