Shahidi katika kesi 457 asema hakuona uhusiano wa JamiiForums na Jamii Media

Jamii Africa

Shahidi  wa upande wa Jamhuri katika kesi 457 inayoikabili JamiiForums,  amekiri kutokuwepo kwa mahusiano kwa  kampuni ya Jamii Media na JamiiForum kwa kuwa kisheria kila kampuni inasimama peke yake.

Kesi hiyo ambayo ilianza kusikilizwa mwaka jana msingi wake ni polisi kuitaka JamiiForums iwapatie taarifa za mwanzisha mada na mchangiaji mmoja ili waweze kuwakamata na kuwahoji juu ya kashfa ya kuchafuliwa kwa kampuni ya CUSNA Investment na Oceanic Link ambayo ilidaiwa kufoji nyaraka bandarini, kukwepa kodi na kuwatesa wafanyakazi wazalendo na kupendelea wageni toka nje ya nchi.    

 JamiiForums inadaiwa kuwa ilikataa kutoa taarifa binafsi za mwanachama wake kwa kuamini kuwa chanzo hiki cha taarifa kilikuwa na nia njema hivyo kutaka kwanza iwepo Hati ya Mahakama inayoridhia kukamatwa kwa mhusika na kuelezwa kosa lake.

Akitoa ushahidi wake leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, shahidi huyo ambaye ni Msajili Msaidizi Mkuu kampuni kutoka Wakala wa Usajili wa Kampuni (BRELA), Rehema Kitambi amesema  mnamo 13 Desemba, 2016 alipokea barua kutoka kwa Mkuu wa Upepelezi wa Makosa ya Jinai ikimtaka athibitishe usajili wa JamiiForums na wakurugenzi wake.

 Anasema katika uchunguzi wao waligundua kuwepo kwa kampuni nyingine ya Jamii Media ambayo inaongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Maxence Melo lakini kampuni hiyo haina uhusiano na JamiiForums kutokana na taratibu za kisheria kila kampuni inasimama peke yake.

Majibu ya shahidi huyo yanatokana na swali aliloulizwa na Wakili wa Utetezi, Jeremia Mtobesya ambaye alitaka kujua uhusiano wa kampuni hizo mbili ikizingatiwa kuwa shahidi aliitaja Jamii Media ikizingatiwa  kuwa kwenye kesi ya msingi natajwa JamiiForums.   

Shahidi huyo anakuwa ni shahidi wa tatu kwa upande wa Jamhuri kutoa ushahidi katika kesi 457 inayosimamiwa na Hakimu Godfrey Mwambapa ambapo upande wa utetezi unawakilishwa na  Mawakili Jebra Kambole na Jeremia Mtobesya  na upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Mutalemwa Kisenyi.

Wakurugenzi wa Jamii Media, Maxence Melo (kulia) na Mike Mushi wakitoka katika Mahakama ya Mkazi Kisutu mara ya kumalizika kwa kesi 457 mapema leo jijini Dar es Salaam

Kesi hiyo imeendelea tena leo kwa shahidi huyo kutoa ushahidi wake na hali ilikuwa hivi:

 Hakimu Mwambapa: Kwa kumbukumbu, Shahidi wa leo ni shahidi wa tatu 

Shahidi: Naitwa Rehema Kitambi, dini yangu ni Mkristo. Cheo changu ni Msajili Msaidizi Mkuu wa Makampuni kwa muda wa kama miezi sita iliyopita sasa.

Wakili wa Jamhuri: Waajiri wako ni nani?

Shahidi: Ni BRELA

Wakili wa Jamhuri: Kituo chako cha kazi ni wapi?

Shahidi: Dar es Salaam

Wakili wa Jamhuri: Majukumu yako kama Msajili Msaidizi Mkuu wa makampuni ni yapi?

Shahidi: Majukumu ni kuhakiki nyaraka mbalimbali kwa ajili ya kufanya usajili kwa ajili ya makampuni mapya na na nyaraka baada ya usajili kwa ajili ya mabadiliko mbalimbali kwenye makampuni. Na kufanya usajili husika na majina ya biashara husika

Wakili wa Jamhuri: Nini pia unafanya tofauti na hilo?

Shahidi: Kuhakiki taarifa mbalimbali ikiwa ni kufanya mabadiliko mbalimbali katika kampuni na majina ya biashara. Pia kutoa ushauri wa kisheria, kujibu barua mbalimbali kutoka kwa mtu yeyote anayetaka kupata taarifa ikiwa ni Kampuni binafsi au taasisi za Serikali

Wakili wa Jamhuri: Nini kilitokea mnamo tarehe 13/12/2016?

Shahidi: Nilipatiwa barua nijibu taarifa ikitaka taarifa juu ya Maxmelo na kampuni ya Jamii Forum, na nilipewa barua nieleze.

Wakili wa Jamhuri: Barua ilitoka wapi?

Shahidi: Ilikuwa inatoka kwa Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai

Wakili wa Jamhuri: Barua ilikuwa inataka nini?

Shahidi: Ilikuwa inataka taarifa za usajili za kampuni ya Jamii Forum na kujua jina Maxmelo kama ni mmoja wa Wakurugenzi wa hiyo kampuni.

Wakili wa Jamhuri: Halafu ukafanya nini?

Shahidi: Kwa mujibu wa taratibu unaitisha jalada, kwa uchunguzi niliitisha jalada toka Masjala kulikuwa hakuna kampuni iliyosajiliwa kama Jamii Forum kwa siku hiyo tarehe 13/12/2016.

Tulitafuta kwenye system iitwayo Saperion, ambayo ina scan taarifa za usajili kwa kipindi fulani. Tuliingiza jina la Maxmelo akatokea kwenye kampuni tatu kwa tarehe hiyo, ambazo sizikumbuki lakini moja ilikuwa ni Jamii Media. Masijala wanafanya hii search then wanakuletea majalada hayo

Wakili wa Jamhuri: Halafu ulifanya nini?

Shahidi: Nikajibu barua ya Mkurugenzi wa upelelezi juua ya majina ya wasajiliwa, namba za usajili, tarehe za usajili na wamiliki wa hisa za hizo kampuni tatu alizotokea Maxmelo (akimaanisha Maxence Melo)

Wakili wa Jamhuri: Ukiona barua nini kitakutambulisha kama ni yenyewe?

Shahidi: Nembo ya BRELA na sahihi yangu mwenyewe

Baada ya Wakili wa Jamhuri kumaliza mahojiano na shahidi, anapewa nafasi Wakili wa utetezi Jeremia Mtobesya kumuuliza maswali shahidi.

 
Mtobesya
: Kwenye hii barua kuna sehemu yeyote umeeonyesha uhusiano kati ya Jamii Media na JamiiForums?

Shahidi: Kwenye barua nimesema hatukuona 

Mtobesya: Kwa maana hiyo nitakuwa sahihi nikisema havina uhusiano (Jamii Media na JamiiForums) wowote?

Shahidi: Kisheria kila kampuni inasimama pekee. Lakini barua ilitaka kujua kama Jamii Forum inatokea sehemu ndio maana tukajibu hivi

Mtobesya: Kwenye lile angalizo la kwenye barua yako ni nini hasa kimeelezewa?

Shahidi: Mbali na nyaraka zile za usajili za awali kampuni imewasilisha baadhi ya form kutaka kufanya mabadiliko katika yale tuliyofanya awali kwenye usajili; Mabadiliko ya Wakurugenzi na wamiliki, ila kwenye barua nimeandika na kadhalika.

Mtobesya: Wakati wewe unaandika barua hii mlikuwa mmesha-attend mabadiliko hayo?

Shahidi: Ndio ila hatukufanya changes kwa sababu ya kasoro kadhaa. Maombi yalikuwa yamepokelewa ila yanashughulikiwa kujibu barua hiyo ya mabadiliko.

Mawakili wote wanasema hawana maswali ya ziada kwa shahidi, anaruhusiwa kuondoka. Kesi itaendelea kesho, Jamhuri imesema inao mashahidi wawili wa kufunga ushahidi katika kesi hii hapo kesho.

Mwenendo wa kesi

Ikumbukwe kuwa shahidi wa kwanza upande wa Jamhuri alisema katika ushahidi wake Agosti 24 mwaka huu ambapo alidai kuwa Polisi hawana utaalamu wa kulazimisha kuingilia mawasiliano kimtandao.  Desemba 5 mwaka huu shahidi wa pili ambaye ni Mkuu wa Upepelezi wa Makosa yaJinai alitoa ushahidi wake na kukiri kuwa aliindikia barua JamiiForums kutaka impatie taarifa muhimu za wateja wake wawili lakini hawakutoa ushirikiano.

ikumbukwe kuwa mwishoni mwaka 2016, Maxence Melo alikamatwa na  kushikiliwa na Jeshi la Polisi katika kituo kuu cha polisi, Dar es Salaam, kwa madai ya kugomea agizo la muda mrefu la jeshi hilo kupewa taarifa za watumiaji JamiiForums bila mafanikio. siku chache zilizofuata alifikishwa mahakamani  kuachiwa kwa dhamana. 

Tangu wakati huo kesi inaendelea kusikilizwa na inatarajiwa kutolewa uamuzi mwishoni kabla ya mwaka huu kuisha.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *