Wasafiri kutoka China kuipata thamani sekta ya utalii Tanzania

Jamii Africa

“Nafikiri kichocheo kikubwa cha uchumi wa Tanzania kitakuwa utalii,” hayo yalikuwa maneno ya Gavana Mstaafu, Prof Benno Ndulu wakati wa Mkutano wa mwaka wa taasisi ya utafiti wa uchumi na Jamii (ESRF) Mie 3 mwaka huu.

Kauli hiyo ilikuwa ni kuikumbusha serikali kuwa ikitumia vizuri fursa ya utalii inaweza kuwa nguzo muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa nchi siku zijazo. Umuhimu huo unajitokeza katika sura tofauti ikizingatiwa kuwa Tanzania inaweza kunufaika na watalii kutoka China wanaopendelea zaidi kutalii katika nchi za Afrika.

Kwa mujibu wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) wasafiri kutoka China wanaongoza kwa matumizi ya pesa na muda kwenye sekta ya utalii duniani ambapo mwaka 2017 pekee walitumia Dola za Marekani 260 bilioni. Matumizi hayo yanafanyika zaidi Afrika kutokana na urahisi wa upatikanaji wa visa, vivutio vingi vya kitamaduni na kihistoria.

Hali hiyo imeifanya Afrika kuwa kivutio kikubwa kwa watalii kutoka China. Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Jukwaa la Usafiri duniani la Travelzoo umebaini kuwa bara la Afrika limekuwa chagua la kwanza la mapumziko ya watalii wa China kwa mwaka 2018 na kuzipiku Japan na Australia.

Watalii hao hutembelea zaidi nchi za Morocco,Tunisia, Afrika Kusini, Namibia, Madagascar na Tanzania. Mwaka huu, nchi jirani ya Kenya imezindua kampeni ya masoko kuifikia China ikitarajia kuwapata wageni 53,000 kutoka China ambao tayari walitembelea nchi hiyo mwaka uliopita.

Jambo la kuvutia katika nchi za Afrika ni kuanzishwa kwa visa zenye masharti rahisi kwa raia wa China. Kwa mujibu wa Kampuni ya usafiri ya ForwardKeys, baada ya Morocco na Tunisia kurahisisha upatikanaji wa visa, kumekuwa na ongezeko la asilimia 240 na 378%  wasafiri wa China walioingia katika nchi hizo.

Travelzoo wanaeleza kuwa bara la Afrika litaendelea kushuhudia ongezeko la watalii hasa kutoka China ambao wanavutiwa na mandhari nzuri na utamaduni.

Watalii kutoka China ni mafano mzuri wa jitihada za China kuchangia ukuaji wa uchumi wa Afrika. Afrika hasa Tanzania imekuwa mshirika muhimu wa maendeleo wa China hasa katika sekta za ujenzi, elimu, afya, miundombinu ambazo zimetengeneza ajira na kukuza ujuzi na teknolojia kwa wananchi.

                     Fukwe za Ngonga zilizopo kwenye ziwa Nyasa wilaya ya Kyela

Hata hivyo, China inatumia fursa hiyo kujiimarisha kijeshi katika nchi za Afrika ili kushindana na Marekani. China imekuwa ikiwachukua vijana wengi wa Afrika na kuwapa mafunzo ya program mbalimbali zinazolenga kuimarisha utamaduni wa China katika bara hilo.

Kitendo hicho kimeufanya utawala wa Donald Trump wa Marekani, kuongeza vikwazo kwa watalii kuingia nchini mwake akihofia kupoteza uungwaji wa mataifa ya Afrika.

Kulingana na shirika la biashara la Umoja wa Mataifa (2014) limeeleza kuwa utalii ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi, ikizingatiwa kuwa mwaka 2014 pekee ulichangia asilimia 8.5 ya pato la ndani la Afrika na kutengeneza asilimia 7.1 ya ajira zote.

Aliyewahi kuwa Waziri  Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo mwaka 2017/2017 alisema sekta ya Utalii ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi hasa katika sekta za kilimo, mawasiliano, miundombinu, usafirishaji, burudani na uzalishaji wa bidhaa na huduma kwa watalii.

“Aidha katika mwaka 2016/2017 watu laki tano waliajiriwa katika sekta ya Utalii na wengine milioni moja walijiajiri wenyewe katika sekta hiyo. Vilevile sekta ilichangia asilimia 17 ya Pato la Taifa na kulipatia Taifa asilimia 25 ya fedha za kigeni”, alinukuliwa  Prof. Maghembe.

 

Nini kifanyike kukuza utalii Tanzania

Baadhi ya tafiti zinakadiria mchango wa pato la taifa kupitia sekta ya utalii unaweza kuongezeka kwa asilimi sita tu ndani ya mwaka 2015-2025,iwapo tu serikali ya Tanzania itaweza kukabiliana na vikwazo ndani ya sekta hii kwa kupunguza utozaji wa ushuru usio na mpangilio kwa wawekezaji na kuthibiti watoza kodi wasio rasmi yaani vishoka ambapo kunaweza kuwa na ongezeko la zaidi ya asilimia 20.

Ili kuboresha sekta ya utalii nchini Tanzania elimu ya darasani na katika sekta hii ni muhimu  ili kuwa na kizazi kitakacho linda hifadhi ya utalii wa taifa.

Hata hivyo, uboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege ni muhimu ili kuongeza wigo wa watalii wa kimataifa kutembelea vivutio vilivyomo nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *