Madiwani wa Muleba wapinga mkopo wa baiskeli

Jamii Africa

KILIO cha madiwani kuboreshewa maslahi yao kimegeuka wimbo wa kawaida takribani katika wilaya zote nchini. Wanadai wanachopata hakilingani na thamani ya uwakilishi wao wa miaka mitano.

Hivi karibuni halmashauri ya wilaya ya Muleba katika kikao cha baraza hilo imeibuka na majibu ya malalamiko ya madiwani kwa kutoa barua inayoelekeza utaratibu wa kuwadhamini kukopa vyombo vya usafiri.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Oliver Vavunge alikuwa katika wakati mgumu wa kuwathibitishia madiwani kama kweli mkopo huo ulilenga kuwasaidia kutokana na kuambatana na masharti magumu ya dhamana.

Kwa mujibu wa mkurugenzi utaratibu huo ulikuwa umetolewa kwa halmashauri zote nchini na kwamba ulilenga kuleta unafuu kwa madiwani ili wajipatie vyombo vya usafiri.

Moja ya masharti hayo ni diwani kuchangia makato ya theluthi moja katika posho yake ya kila mwezi na kulazimika kuweka dhamana ya hati ya nyumba au shamba ambapo idadi kubwa ya madiwani wanatoka katika maeneo yenye ardhi isiyopimwa.

Utaratibu huo uliongeza kilio zaidi kwa madiwani wakiufananisha na mkopo wa baiskeli kwani kwa kiwango cha posho ya diwani wa halmashauri hiyo baada ya kukamilisha masharti angeweza kupewa mkopo sio zaidi ya shilingi laki tisa.

Kiwango hicho cha fedha kiliwashangaza madiwani huku wakijitapa kuwa hiyo hatua ya kuwadhalilisha kwani tayari walikuwa wanamiliki usafiri binafsi uliokuwa unazidi hata kiwango cha mkopo unaokusudiwa kutolewa.

Diwani wa kata ya Gwanseli Julius Lwakyendera alisema kupitia barua hiyo haoni juhudi zozote za kuwasaidia na kuwa huo ulikuwa ni ujanja wa serikali kuvuta muda ili ionekane kilio chao kinazingatiwa.

Pia alisema Wizara husika haina nia ya kuwasaidia na kupendekeza kuanzishwa aina nyingine ya umoja miongoni mwa madiwani utakaowaunganisha na kudai maslahi yao na kuwa umoja uliopo hivi sasa umeshindwa kuwasaidia.

“Wizara haina nia ya kutusaidia huu ni wakati wa kuamka na kuanzisha aina nyingine ya umoja wa kutuunganisha ili kutetea masrahi yetu hatuwezi kukubali mkopo unaolingana na thamani ya baiskeli”alisema diwani huyo.

Baadhi yao walisema hakuna njia nyingine ya kumsaidia diwani hapa nchini zaidi ya kuunganisha nguvu kuliko kukubaliana na masharti ya mkopo ambao hauwezi kuwasaidia kuongeza kipato na kukidhi mahitaji yao mbalimbali.

Wakati wa mjadala madiwani wa kambi zote waliungana na wengine wakidai wakati wa uchaguzi mkuu ujao wasitambuliwe kama miongoni mwa mafiga matatu kwani baada ya uchaguzi mafiga mawili huungana na moja kuwekwa kando.

Madiwani hao walilalamikia kubebeshwa majukumu makubwa katika kata zao bila masrahi yao kupewa umuhimu huku wakiwatuhumu wabunge kwa kutetea masrahi yao na kulisahau kundi la madiwani.

Diwani wa kata ya Bumbile Sweetbert Mutembei alisema maendeleo hayawezi kupata kasi ya kutosha endapo kundi lao litaendelea kupuuzwa katika uboreshaji wa masrahi yao.

Alisema tofauti na wabunge madiwani ni kundi lililopo karibu zaidi na wananchi na wajibu wao ni mkubwa katika kuchochea maendeleo ya maeneo yao.

Walisema dhamana ya udiwani ni kubwa na anasitahili kupata nafuu ya mkopo na kikiona kama kichekesho ikilinganishwa na wabunge ambao hupewa mashangingi na hivi karibuni kuongezewa posho ya vikao kinyemela kutoka 70,000 hadi 200,000.

Baadhi yao walitaka mjadala huo ufutiliwe mbali kwani pamoja na kuwa usingeleta majibu tofauti pia ulikuwa unachelewesha kujadili mambo waliyodai ni muhimu zaidi kuliko hiyo danganya toto ya mkopo.

Diwani wa Kata ya Muhutwe Justus Magongo aliwataka madiwani kujielekeza zaidi kujadili mipango ya maendeleo ya wilaya hiyo kwani barua hiyo ilikuwa inawaweka katika kundi la watu wasioweza kukopesheka.

Baada ya kukubaliana kuwa mashariti yalegezwe na kiwango cha mkopo kuongezwa hatimaye walijadili kero zinazowakabili wananchi wa wilaya hiyo ikiwemo kukithiri kwa migogoro ya ardhi katika maeneo yaliyonunuliwa na wawekezaji.

Mgogoro wa ardhi Rutoro katika lanchi ya Kagoma ulichukua sehemu kubwa ya mjadala huku madiwani wakiitahadharisha serikali athari kubwa zitakazojitokeza kwa kushindwa kupata ufumbuzi kati ya wananchi na mwekezaji.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Muleba Oliver Vavunge alisema mahitaji ya madiwani ni makubwa ikilinganisha na mapato madogo yanayotegemewa kwa kiasi kikubwa katika uendeshaji wa halmashauri hiyo.

Alisema hapingani na madiwani waliokosoa utaratibu wa kupatiwa mkopo wa usafiri na kushauri mawazo hayo yapelekwe kwenye umoja wao ambapo yanaweza kujengewa hoja zaidi.

Habari hii imeandikwa na Mwandishi wa Fikrapevu (Mkoani Kagera) – Phinias Bashaya

2 Comments
  • udiwani kwa mujibu wa sheria si kazi bali ni nafasi ya kujitolea ambayo mtu hupewa kwa njia ya kidemokrasia kutokana na wenzake kuamini kuwa huyo mtu ni maarufu na ana uwezo zaidi (maarufu). na kwa msingi huo hata akisha chaguliwa halmashauri humtegeme mtu huyu kwa misaada mbalimbali. sheria inatamka wazi kuwa diwani ni mtu mwenye kazi yake, na kazi hiyo inampa kipato halali. hayupo kwenye payroll ya serikali, na kwa kusema hayo hakopesheki in any how.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *