MCHUNGAJI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri(KKKT) katika Usharika wa Inuka lililoko kata ya Mkuyuni Jijini hapa, Jackob Kituu ameshauri Wakristo nchini waache kula angalau kwa siku kadhaa, ili pamoja na mabo mengine wapate fursa nzuri ya kuliombea taifa dhidi ya vitendo vya ufisadi pamoja na ushoga.
Mchungaji Kituu alitoa rai hiyo wakati akihubiri waumini wa kanisa hilo kwenye maadhimisho ya siku kuu ya Krismas, Jijini hapa.
Vilevile, mchungaji huyo aliwataka waumini wa kanisa hilo ambao pia wamedhaminiwa nafasi za viongozi pamoja na watumishi katika ofisi za umma waache tabia ya kuomba ama kupokea rushwa kwa sababu vitendo hivyo vinamchukiza Mungu.
“ Kusema kweli taifa limefikia hatua mbaya sana katika vitendo vya ufisadi; na sasa Watanzania tunashauriwa na mataifa ya kigeni eti tukubaliane na ushoga. Ama kweli uovu unaofanyika sasa hivi duniani unazidi hata uliokuwa ukifanyika nyakati za Sodoma na Gomola na kuliko hata katika siku za Nuhu” alisema Mchungaji Kituu .
Alisema kwamba ni vema taifa likubali hata kufa kutokana na umaskini, kuliko kukubaliana na masharti ambayo yanayokiuka uumbaji pamoja na sheria za Mungu.
“ Mimi nasema ni afadhali kufa maskini kulikoWatanzaia kukubaliana na ushoga; na nisema pia kwamba waumini tusikualiane na yeyote anayetaka kutuingiza majaribuni juu ya ushoga” alisema.
Kwa mujibu wa mchungaji Kituu, ushoga ni hatua ya juu kabisa ya uovu duniani; uovu ambao umepewa jina la utandawazi kwa kisingizio cha haki za binadamu.
“ Huwa inanishangaza sana kwamba kila ninaposoma magazeti , kusiliza redio ama TV hukutana na majina ya wakristo. Kwa kweli watu kama hao wanalitia doa kanisa la Mungu na wanapaswa watubu!” alisema mchungaji huyo.
Mchungaji Kituu alisema ufisadi ni dhambi kama zilivyo dhambi zingine ambazo zimchukiza Mungu.
Alitumia fursa hiyo kuwataka waumini wa kanisa hilo kuchukia ufisadi ambao alisema umeenea hata katika baadhi ya nyumba za ibada nchini.
“ …ni aibu kwa kiongozi au mtumishi wa umma kushiriki katika kuomba na kupokea rushwa huku akijua kuwa analipwa mshahara. Hivi ni kwa nini uombe rushwa; kwa nini uandike matumizi hewa ofisini kwako! “ alihoji Kituu.
Aliwataka waumini wa kanisa hilo wawe mfano wa kuigwa katika jamii na serikali kwa kutenda mema siku zote; badala ya kusubiri nyakati za siku kuu pekee.
mwisho.
Na. Juma Ng’oko – Mwanza