Ukame, Ukosefu wa Chakula, vinavyoleta changamoto ya afya kwa waathirika wa UKIMWI huko Mwadui – Lohumbo

Belinda Habibu

Ukame wa muda mrefu uliyoikumba vijiji vya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ni mwiba kwa waathirika wa virusi vya UKIMWI.

Mzee Doto Masese (60) ambaye ameathirika kwa virusi vya UKIMWI, alisema wengi wetu tunashindia mlo mmoja ama hakuna kabisa hata unga wa kupikia uji, wakati huo huo tunatakiwa tunywe dawa za kurefusha maisha (ARV).

“Naweza kukaa na njaa kutwa nzima sina chochote ila siwezi kuacha kunywa  dawa hizi za ARV, sipendi kufa mapema, ila zina nguvu sana kama huli chakula cha kutosha” alisema mzee Masese.

kushuka-cd4

Moja ya faili la muathirika wa UKIMWI ikionyesha kushuka kwa CD4 kutokana na kukosa lishe

Ameongeza changamoto yetu kubwa sisi tulioathirika ni lishe, tumeshauriwa na daktari kula milo mitano kwa siku,hapa kijijini Lohumbo kuna njaa ya kutisha, mazao yanakauka kwa waliolima na hata ukiomba msaada kwa watu wengine wakazi wa hapa  hawana akiba ya chakula.

Pamoja na umri wake kuwa mkubwa mzee Masese alisimulia mwaka 2012, jinsi alivyovamia mgodi wa mwekezaji wa Williamson wa almasi katika udongo wa jalalani ilia apate walau madini akauze anunue chakula.

“Mwanangu nilifanya hivyo baada ya kufikiria sana, nikaona nivamie tu mgodi huo,nilikamatwa nikawekwa kituo cha polisi pale mgodini Mwadui, ila niliwaambia askari,mimi ni mwathirika wa virusi vya UKIMWI, nikawaonyesha cheti na niliwaambia nina njaa natakiwa ninywe dawa pia, wakaniachia”alisema mzee Masese.

Mwathirika mwingine wa ugonjwa wa UKIMWI anayejulikana kwa jina la Gamaya Simba alisema alijiunga na kikundi cha Upendo ili asaidiwe kwa kupata dawa za kuongeza maisha (ARV) aendapo zahanati ama hospital  na chakula kwa kuwa mwaka wa nne sasa hakuna mvua ya kutosha.

Ameongeza nilikuwa mpweke na mawazo mengi na afya yangu ilizorota,lakini sasa naweza kunywa uji hata kwa mwenzangu ingawa ukame umetuathiri sana hapa kijijini,hasa  sisi tunaoishi kwa matumaini.

Mjumbe wa kikundi hicho bibi Halima Juma Nkwabi alisema wengi wetu CD4 zimeshuka kutokana na lishe kuwa ya wasiwasi ama isiwepo kabisa.

“Tunapambana na ugonjwa,chakula na hata dawa wakati mwingine,na umbali wa kutoka hapa hadi hospital ya Mwadui ni zaidi ya km 3.kama hujala vizuri unaweza kuanguka njiani  unapokwenda kuchukua dawa”alisema bibi Nkwabi

Mwenyekiti wa kikundi cha waathirika wa ugonjwa wa UKIMWI kinachojulikana kwa jina la Upendo, bibi Elisifa Michael alisema usione mtama huu hapa uliopandwa karibu na serikali ya kijiji, mwaka huu tuna njaa hapa kijijini Mwadui  Lohumbo,familia nyingi zinashindia mlo mmoja na sisi waathirika wa ugonjwa wa UKIMWI ndio tunapata shida sana.

“Kwa mfano nikiumwa malaria sasa hivi,natakiwa ninywe dawa za mseto,ARV, wakati huohuo sina chakula tumboni nitakuwa katika hali gani ndugu mwandishi? Ni mateso makubwa kwetu.” Alisema mwenyekiti  huyo.

Ameongeza toka tuanzishe kikundi hiki mwaka 2008,tumeshapoteza wenzetu wana kikundi wanne,aliyekuwa mwenyekiti wa kwanza wa kikundi hiki bwana Joseph Ngunila (62) alifariki kwa kukosa lishe nzuri na magonjwa nyemelezi yalimwandama basi tukampoteza.

Alisema wengine ni Sai Sande (60), Bunonu Nhugulu (70) na Sara Kija (57) nao tatizo lao halitofautiani na mwenyekiti wetu, ukichanganya na uzee walionao walipoteza maisha.

Bibi Michael alisema ingawa tunachangishana sh.2500 kwa wiki,kwa wanachama wote wa kikundi cha Upendo wapatao 20,na hela iliyopatikana kukopeshana miongoni mwetu, bado haikidhi haja ya kumaliza ukali wa ukame na ukosefu wa chakula hapa kijijini.

“Tumesitisha kwa sasa kupokea marejesho kutoka kwa wanachama, kwa kuwa hali ni ngumu ya kiuchumi miongoni mwetu,tunaomba msaada kwa serikali hatuna jinsi kwa sasa”alisema mwenyekiti huyo akionyesha kuhuzunika.

Kwa upande wake katibu wa kikundi hicho, bwana Boaz Masunga, alisema kwa kuwa wana changamoto nyingi, ikiwemo ya chakula,walibuni mradi wa kufuga kuku wa kienyeji kama walivyoshauriwa na ofisi ya TASAF wilaya ya Kishapu,ili waweze kuuza mayai na hata nyama.

“Tunashangaa mradi wetu mpaka leo hauna majibu, wanachama wanahitaji chakula,tunashindwa kununua maana kulima ni shida kwa kipindi hiki cha ukame” alisema Masunga.

Alisema wakati sisi tunapeleka mardi wetu tulioubuni  na serikali ya kijiji nayo wakabuni mradi wa lambo,pamoja na kufungua akaunti  mpaka leo hatupewi jibu la uhakika tunapoiuliza serikali ya kijiji ili hali wao wameshapata fedha za mradi wao.

Akizungumzia suala hilo afisa mtendji wa kijiji hicho, Musiba Atanasi alisema ni kweli wanachokisema lakini sijui mpaka sasa kwa nini hela hizo zimechelewa na hawajawekewa, kwa upande wa mradi wa lambo, ofisi ya kijiji kweli imeshawekewa hela kiasi cha sh.milioni 47 katika akaunti yake ili  kuanza mradi huo.

“Kwa nini umeanza mradi wetu mimi sijui, ila kwa uzowefu wangu kwa miradi mingi ya TASAF, wazo mlilobuni likikubalika huchukua wiki ama wiki mbili, ila mimi ninavyojua mambo ya serikali, unaweza ukaahidiwa leo utekelezaji ukafanyika baada ya miaka mitano.” aliongeza bwana Atanasi.

Aidha Kutokana na hali hiyo,afisa huyo amesema  mradi wa lambo na ule wa kuku wa kienyeji walituma maombi yao toka mwezi wanne mwaka 2012,na kupata jibu la kufungua akaunti mwezi wa tisa mwaka huo huo,hivyo kikundi cha upendo kiwe na subira.

Mratibu wa TASAF wilaya ya Kishapu bibi Rehema Edison amekiri kuwa kikundi hicho hakijaingiziwa fedha katika akaunti yao sh.milioni 15 za mradi wao wa kuku wa kienyeji, kwa sababu ofisi kuu ya Dar es salaam haijaweka kwa kuwa wanaanda bajeti ya mwaka wa pili wa mradi ila muda wowote itaingia.

“Mwezi wa kwanza 2013, nilikuwa Dar es salaam, kwaajili ya bajeti ,nafikiri wanamambo mengi na wako bize na maandalizi ya TASAF 3 inayoanza mwezi wa 7 mwaka huu”, aliongeza mratibu huyo.

Ameongeza nimetoa taarifa kwa serikali ya kijiji nini kinaendelea  kwa upande wa TASAF makao makuu,ili wawaambie wanakikundi wote.

Akizungumzia suala la lambo na ufugaji wa kuku, bwana shamba na mifugo wa wilaya ya Kishapu Dr. Alphonce Bamagashi alisema kutokana na mazingira ya sasa ya ukame katika wilaya hii ni mazingira mazuri ya  kuchimba lambo.

Aliongeza mradi wa lambo kupewa kipaombele cha kwanza kwa kupewa  hela kuliko vikundi vingine, haina picha mbaya kwa kuwa malambo yanachimbwa wakati wa ukame kama huu,ili msimu wa mvua ukifika tuwe na hifadhi ya maji, tunaomba kikundi hiki (Upendo) kiwe na ustahimilivu watapata hela ya mradi wao kwa kuwa umekubaliwa.

Kikundi cha Upendo kinajumuisha watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI wapatao 20 wa rika tofauti vijana kwa wazee, waliojiunga waweze kutambulika na jamii, wanatoa elimu ya UKIMWI kwa wanajamii na wamekuwa mashujaa wa kujitangaza kwa hali yao kijijini Mwadui Lohumbo.

UPENDO-group

Baadhi ya wanachama wa Kikundi cha Upendo

Aidha kijijini hapo pia  kipo kikundi kama hicho kinachojulikana kwa jina la Amani,chenye wanachama 24 wanaoishi kwa virusi vya UKIMWI na wao wako wazi wanajitangaza na kuelimisha wanajamii juu ya athari za ugonjwa wa UKIMWI.

Kijiji cha Mwadui Lohumbo ni miongoni mwa vijiji 8 vinavyozunguka mgodi wa mwekezaji wa madini ya almas ya Willianson Diamond,ambapo wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula kutokana na ukame wa zaidi ya miaka minne.

Kwa mujibu wa barua ya muktasari wa mkutano wa upembuzi shirikishi jamii ya tarehe 24.4.2012,kwenda kwa mkurugenzi wa halmashauri ya kishapu,inaonyesha kijiji hiki kina kaya 194,wakazi 854(wanaume 417 na wanawake 437).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *