Mwekezaji atoweka na kuacha shimo, hema

Kulwa Magwa

TAKRIBAN miaka mitatu imepita tangu kampuni ya Kastan iliyotaka kuchimba dhahabu katika kijiji cha Sambaru, wilayani Ikungu, mkoa wa Singida, ilipoondoka bila kuaga.

Kampuni hiyo ilipokwenda sehemu hiyo, ilifanikiwa kupata leseni kadhaa za wachimbaji wadogo ambao iliingia nao mikataba ya kuuziana maeneo na kushirikiana katika uchimbaji.

Hata hivyo, tangu ilipofika na kuondoka, mwaka 2010, hakuna mwakilishi wake aliyerejea sehemu hiyo ambako imeacha hema na shimo refu ililokuwa imeandaa kwa ajili ya shughuli zake.

shimo

Shimo liliachwa na Kastan Limited, katika kijiji cha Sambaru, wilaya ya Ikungi, mkoani Singida

Herbert Bisanga ambaye ni mmoja wa wachimbaji wadogo wanaoishi Londoni, wilayani Manyoni, anasema kwenda na kutoweka kwa kampuni hiyo ni mambo yaliyoacha maswali miongoni mwao.

Bisanga anasema maswali waliyo nayo ni jinsi Kastan Limited ilivyoingia katika kijiji hicho na kuanza kununua maeneo kwa wachimbaji huku wengine ikiwakopa, na baadhi yao kukabidhi leseni za umilikiwa migodi kwa mmoja wa wawakilishi wa kampuni hiyo.

kastan-ltd

Bango linaloonyesha barabara iliyokuwa ikitumiwa na kampuni hiyo

Anasema, waliokopwa waliambiwa wangelipwa baada ya kukamilika kwa baadhi ya taratibu na tangu wakati huo hakuna malipo waliyopelekewa.

Suala la pili, Bisanga, analitaja kuwa ni kutokamilika kwa malipo ya waliokopwa na kutoweka ghafla kwa mawasiliano kati yao na mwakilishi wa kampuni hiyo.

Hata hivyo, suala lingine ni jinsi ilivyoondoka baada ya kutokea ‘sintofahamu’ kati ya mwakilishi wa kampuni hiyo, wananchi na wachimbaji wadogo ambao walifika mahali wakavamia ilipokuwa ikifanyia shughuli zake na kumtimua mtu huyo. Tangu wakati huo, mahali hapo limebaki hema na shimo hilo.   

hema

Hema lililoachwa sehemu hiyo

Katibu wa Kamati ya Wachimbaji Wadogo wa Sambaru na Londoni, Ayoub Magoa, anasema wamiliki wengi wa leseni walioingia makubaliano na kampuni hiyo wameachwa solemba kwa kuwa hakuna walichoambulia.

“Huo ulishakuwa kama msiba – hao watu wameachwa bila chochote – sio pesa wala leseni; vyote viliondoka na juhudi za kufuatilia kujua ilipo kampuni hiyo hazijazaa matunda,“anasema Magoa.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Watafiti na Wachimbaji Madini Wadogo mkoa wa Singida (SIREMA), Robert Malando, anasema tangu ilipopokelewa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Singida, kampuni hiyo haikuwa wazi katika mambo yake.

“Unajua hata walipokuja walifikia kwa RAS (katibu tawala wa mkoa) ambaye alitualika kwenye kikao – tukakutana nao, tukazungumza lakini baada ya hapo tukaanza kusikia malalamiko kutoka kwa watu mara hawalipwi kulingana na makubaliano, mara leseni zimeondoka zitarudishwa. Tulifika mahali tukaomba msaada tena kwa RAS lakini hakutusaidia,” anasema Malando.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *