Madiwani Muleba walia na watendaji kufuja mapato, mwenzao awalipua

Jamii Africa

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera wamketaka kushughulikiwa haraka kwa watendaji wanaoiba mapato ya halmashauri hiyo,  ambao wanakwamisha mpango ya kubuni njia mpya za mapato.

 

Picha Diwani wa Kata ya Gwanseli Julius Rwakyendera

Katika mjadala mkali uliojitokeza wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani baadhi ya madiwani walisema hawako tayari kupendekeza uanzishwaji wa vyanzo vipya vya mapato kwani hata vilivyopo havisimamiwi vizuri na watendaji.

“Halmashauri ina vyanzo vingi vya mapato tatizo ni uadilifu miongoni mwa watumishi, hatuwezi kubuni vyanzo vipya na kuleta kero kwa wananchi huku mapato yakiingia mifukoni mwa watumishi wachache,” alisema Julius Rwakyendera Diwani wa Kata ya Gwanseli.

Katika kikao hicho,  madiwani walilalamikia mbinu chafu zenye harufu ya rushwa wakati wa utoaji wa zabuni kwa mawakala wa ukusanyaji ushuru katika mialo na kuwa kiasi kinachopelekwa halmashauri ni kidogo ikilinganishwa na hali halisi.

Baadhi ya madiwani wanaotoka katika kata za visiwani ambao walidai kuwa na uzoefu katika biashara ya samaki, walisema tenda hutolewa kwa upendeleo ambapo baadhi ya makusanyo huingia mifukoni mwa watendaji.

Diwani wa Kata ya Nshamba Jones Kabelinde alitaka ushindani wa kupata tenda za kukusanya ushuru wa mialo uwe wazi na kuwa anajua ‘utamu na faida’ kubwa iliyopo tofauti na kiwango kidogo inachopata halmashauri.

Akithibitisha hila za watendaji wa halmashauri kuikosesha wilaya hiyo mapato Diwani wa Kata ya Kerebe iliyoko kisiwani, Projest Paul alidai katika eneo lake aliyepewa tenda ni yule aliyeonyesha kukusanya Shilingi milioni 1.7 badala ya yule aliyeonyesha kukusanya Shilingi milioni mbili jambo alilolihusisha na ufisadi.

Aidha, Diwani wa Kata ya Muleba mjini Hassan Milanga alibadili mwelekeo wa kikao hicho ambaye pamoja na kupinga uanzishaji wa vyanzo vipya vya mapato pia aliwashutumu madiwani tisa waliokuwa katika ziara nchini Uganda hivi karibuni kuwa haikuwa na tija.

Mbali na kudai kuwa waliondoka kinyemela bila baraka za madiwani wenzao baada ya kupata mwaliko wa ujumbe mfupi wa maandishi (sms) katika simu zao,  alisema ziara hiyo haikulenga kuisaidia halmashauri bali malengo ya baadhi ya wanasiasa, akimtaja Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini Profesa Anna Tibaijuka.

Aidha katika kuthibitisha kuwa madiwani hao waliondoka kinyemela,  Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,  Olver Vavunge aliwaruka mbele ya baraza hilo kuwa hakujua kuondoka kwao na ndiyo sababu aliwanyima posho ambazo walidai baada ya kurudi katika ziara hiyo.

Habari hii imeandikwa na Phinias Bashaya-Mwandishi,  Kagera

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *