WAKILI maarufu nchini, Tundu Lisu jana aligeuka kuwa mbogo katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, inayosikiliza kesi ya kupinga matokeo ya ushindi wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Jijini Mwanza, Highness Kiwia (Chadema), ambapo katika kesi hiyo alimbana maswali magumu shahidi wa kwanza na mlalamikaji wa tatu wa kesi hiyo ya madai.
Katika kesi hiyo namba 12/2010 iliyofikia hatua ya mashahidi, iliyosikilizwa na Jaji Mjemas kutoka Bukoba Mkoani Kagera, Lisu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kampi rasmi ya upinzani Bungeni, alitumia hati ya mashtaka ya walalamikaji kumbana shahidi huyo, Beatus Martin Madenge kuhusu maelezo ya hati hiyo, ambayo aliyakubali na baadaye akayakana mbele ya mahakama hiyo.
Katika mahojiano mbele ya mahakama hiyo, Wakili Lisu anayemtetea Mbunge Kiwia, alimtaka shahidi na mlalamikaji wa kesi hiyo ya madai, Madenge kuithibitishia mahakama Kuu iwapo maelezo na saini yake iliyomo kwenye hati ya mashtaka ni sahihi ama si sahihi, ambapo alikiri mbele ya mahakama kwamba maelezo yote yaliyomo kwenye hati hiyo ni sahihi na hakuna hata neno moja la uongo.
Baada ya shahidi huyo kukiri kupiga kura kihalali siku hiyo ya Oktoba 31 mwaka 2010, Lisu alimtaka pia shahidi huyo aieleze mahakama sababu za kutoa maelezo mahakamani hapo kwamba yeye alizuiliwa kupiga kura katika kituo alichopangiwa cha Mihama Shule ya Msingi Ilemela, baada ya kukamatwa na kundi la vijana waliokuwa wakiwazuia wafuasi wa CCM kwenda kupiga kura katika kituoni hicho.
Kufuatia maswali hayo magumu, shahidi huyo baadaye alikana mbele ya mahakama kwamba yeye siku hiyo ya uchaguzi hakufanikiwa kupiga kura, kwani alikamatwa majira ya saa 4 asubuhi wakati akienda kupiga kura, na kwamba walalamikaji wenzake ndiyo waliopiga kura siku hiyo, jambo ambalo lilisababisha watu waliokuwa wamejaa kusikiliza kesi hiyo kuangua kicheko cha chinichini.
“Mheshimiwa Jaji, yaliyoandikwa na kuyasaini mimi kwenye hati hii ni ya kabisa. Lakini mimi nasema sikupiga kura siku hiyo nilikamatwa. Sikupiga kura ila wenzangu ndiyo waliopiga kura”, alisema shahidi huyo mbele ya mahakama, akikana maelezo yaliyomo kwenye hati yake ya mashtaka yanayoeleza kwamba siku hiyo ya uchaguzi yeye alipiga kura kihalali.
Kesi hiyo ya madai namba 12 ya mwaka 2010, imefunguliwa na walalamikaji watatu, ambapo wanaiomba mahakama Kuu Kanda ya Mwanza itengue ushindi wa Mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Highness Kiwia (Chadema), kwa madai kwamba mbunge huyo hakushinda kihalali kwenye uchaguzi huo Mkuu wa mwaka 2010, na wanaoshtakiwa kwenye kesi hiyo ya madai ni Mbunge Kiwia, Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Ilemela pamoja na mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mbali na hayo, wakili Lisu alimhoji shahidi huyo akitaka aieleze mahakama ni kwa nini aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM jimbo la Ilemela, Anthony Diallo hajafungua kesi mahakamani, isipokuwa hao walalamikaji, na alimtaka pia shahidi huyo kueleza iwapo amepewa fedha au alikuwa mgombea mwenza wa Diallo katika uchaguzi huo Mkuu.
“Umeiambia mahakama kwamba Diallo ndiye aliyekuwa mgombea wa CCM Jimbo la Ilemela, sawasawa. Ni kwa nini Diallo hajalalamika popote wala kuleta kesi mahakamani?. Je wewe ulikuwa mgombea mwenza wa Diallo, au nani amekutuma kufungua kesi?”, alihoji Lisu huku Jaji Mjemas akimsisitiza shahidi huyo kujibu maswali ya wakili huyo wa upande wa utetezi.
Kufuatia maswali na majibu hayo, wakili Lisu ambaye alikuwa akizungumza kwa kujiamini huku akizunguka huku na kule mahakamani hapo, alimhoji shahidi huyo kwamba: “Kama Diallo hajalalamika mahala popote juu ya kushindwa kwake, wala hajaleta kesi mahakamani, unaufahamu usemi wa kwamba pilipili aile mwingine wewe ikuwashie nini?”.
Akijibu swali hilo, shahidi Madenge alisema yeye hajatumwa na mtu wala hakuwa mgombea mwenza wa Diallo, na kwamba yeye na wenzake wamepata machungu baada ya mgombea wa CCM kuonekana ameshindwa pasipo kihalali na mbunge wa sasa wa jimbo hilo.
Katika kesi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi, iliyopangwa leo Alhamisi kuendelea tena, walalamikaji wanadai kwamba watu ambao hawakupiga kura Ilemela siku hiyo ya Uchaguzi ni 114,085, kati ya watu 175,978 waliojiandikisha ambapo waliopiga kura ni 61,893 pekee, na kwamba anaamini idadi ya watu ambao hawakupiga kura ilitokana na kuzuiwa na vijana 200 anaoamini ni wafuasi wa Chadema.
Habari hii imeandaliwa na Sitta Tumma – Mwanza
kutokana na mazingira ya kujikanyaga mashahidi mm naona kwa maendeleo ya democrasia ya kweli wamuache mbunge awafanyie kazi wananchi ila tu watu wa mwanza wajipange kiupya kwa kipindi kijacho
Naona kesi imekwisha wakili amefanya kazi yake vema