Mkurugenzi Magu akiri kulipa mishahara marehemu

Jamii Africa

HATIMAYE Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, imekiri kuwepo kwa ufisadi mkubwa wa kulipa mishahara hewa, ikiwemo ya watumishi wake waliostaafu na wale waliofariki dunia.

Kutokana na ukweli huo, halmashauri hiyo tayari imemsimamisha kazi mtumishi wake aliyekuwa anahusika na ulipaji wa mishahara watumishi, Anjelina Kamugisha, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo nzito za ufisadi.

Imeelezwa kwamba, baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo ya Magu ambao kwa sasa ni marehemu pamoja na watumishi waliostaafu kazi, kwa muda mwingi wamekuwa wakiingiziwa malipo ya mishahara yao kwenye benki ya NMB tawi la Magu, kisha fedha hizo kutolewa na baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wa benki hiyo wasio waaminifu.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo ya Magu, Cornel Ngudungi (DED), aliyathibitisha hayo jana jioni, wakati alipokuwa akitoa taarifa ya  tuhuma za ubadhilifu huo, katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani, kilichoketi chini ya mwenyekiti wake, Boniventure Kiswaga mjini humo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza, Boniventure Kiswaga

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza, Boniventure Kiswaga (katikati aliyesimama), akituliza munkari ya madiwani kuhusu marehemu kulipwa mishahara na halmashauri hiyo. Kulia kwake Mwenyekiti ni Mkurugenzi mwenyewe (aliyevaa tai)

“Mheshimiwa mwenyekiti, taarifa za halmashauri kulipa mishahara kwa marehemu na wastaafu, ni kweli zipo. Nimelazimika kuzifuatilia hadi kwa uongozi wa NMB.

“Mishahara hii ilikuwa ikiingizwa benki ya NMB tawi la hapa Magu. Baada ya kuingizwa ilikuwa ikitolewa na baadhi ya watumishi wetu kwa kushirikiana na wale wa benki wasiowaaminifu.

“Kwa hiyo, nimeamua kumsimamisha kazi Anjelina Kamugisha ambaye ndiye aliyekuwa anasimamia ulipwaji wa mishahara. Tuhuma hizi za mishahara hewa zipo na tunazifanyia kazi”, alisema Mkurugenzi Ngudungi bila kutaja idadi ya fedha za mishahara hewa zilizolipwa.

Madiwani wa Halmashauri ya Magu wakifuatilia mjadala

Madiwani wa Halmashauri ya Magu wakifuatilia mjadala mkali wa halmashauri hiyo kulipa mishahara kwa watumishi wa halmashauri hiyo ambao walishafariki dunia na wale waliostaafu kazi

Inasadikiwa kwamba, halmashauri hiyo imetumia mamilioni ya fedha kulipa mishahara hewa kwa wastaafu na watumishi wake waliotangulia mbele ya haki, na FikraPevu itaendelea kuchokonoa kiundani zaidi ili kubaini idadi halisi ya fedha hizo zilizotumika vibaya.

Aidha alieleza kwamba, ili kubaini ukweli wa mambo, yeye alilazimika kuonana na uongozi wa NMB tawi hilo la Magu, kwa lengo jema la kupata usahihi wa taarifa hizo, lakini aliombwa aende jijini Mwanza akaonane na Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa.

Alisema, baada ya kuonana na meneja huyo aliyemtaja kwa jina la Chilongola, alielezwa kwamba, benki hiyo haiwezi kutoa fedha hizo mpaka vyombo vya dola, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), na jeshi la polisi waamue kutolewa kwa fedha hizo na si vinginevyo.

“Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Bwana Chilongola aliniambia hawawezi kuzungumzia suala hilo hadi wapeleke barua.

“Na tulipopeleka barua alitujibu benki yake haiwezi kutoa fedha hizo mpaka TAKUKURU au polisi waamuru kutolewa kwa fedha hizo”, alifafanua Mkurugenzi huyo wa halmashauri ya wilaya hiyo ya Magu, huku akimuonesha mwenyekiti Kiswaga majibu ya barua ya NMB.

Alisema, tayari alishamwandikia barua Mkuu wa kituo cha Polisi wilaya hiyo ya Magu, akimuomba asaidie kupata taarifa ya ripoti ya ukaguzi wa NMB, na kwamba amemuagiza Mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo aanze mara moja ukaguzi wa wizi huo, pamoja na kutoa ushirikiano zikiwemo nyaraka zote kwa Mkaguzi.

Awali, kulikuwepo na taarifa za halmashauri hiyo kulipa mishahara hewa, ikiwemo ya watu waliofariki dunia na wale waliostaafu kazi katika halmashauri hiyo, lakini ukweli wake ulikuwa haujabainika.

Taarifa hiyo, imekuja kufuatia kikao kilichopita cha baraza la madiwani wa Magu, ambacho kilitoa maazimio ya kuitaka ofisi ya Mkurugenzi kufuatilia tuhuma hizo, na kikao cha juzi atoe taarifa ya tuhuma hizo za ubadhilifu wa mali ya umma.

Licha ya Mkurugenzi Ngudungi kutoa taarifa hiyo ya utekelezaji wa baraza la madiwani, lakini madiwani wenyewe walichachamaa na kumtaka Mkurugenzi huyo aeleze kwa nini nani aliyekuwa anaidhinisha mishahara ya watumishi, ikiwemo mishahara hiyo hewa.

Diwani wa Kata ya Lubugu, Julius Ngongoseke (UDP), alisimama na kumtaka Mkurugenzi Ngudungi alieleze baraza hilo kama kuna mtu tofauti na Mkurugenzi anayeidhinisha kulipwa kwa mishahara hiyo.

Kufuatia hali hiyo ya vuta ni kuvute, mwenyekiti wa halmashauri hiyoanayesifiwa kwa umakini katika kazi zake, alilazimika kuvunja kanuni kisha kusimama kikaoni na kuwaomba madiwani wasiendelee kulijadili suala hilo, kwani kufanya hivyo wanaweza kutoa fursa ya mtuhumiwa kulalamika kwamba amejadiliwa mapema, hivyo liachwe lishughulikiwe kisheria zaidi.

Habari/Picha na Sitta Tumma – FikraPevu, Mwanza

7 Comments
  • Huyu DED ana matatizo siyo tu mishahara, hata mikataba ya wakandrasi na malipo yao. Amekuwa akivuruga na kuvunja mikataba na kukwamisha maendeleo ya wana Magu.

    • Duh! Ama kweli kwa hali hii nawambieni ya kwmb hakika tumeshaishaga Watanzania kitambo sana,Ila ingekuwa leo ni Mi ndio mwenye usemaji ktk hili,nawaambia ya kwmb ningekuwa na kauli pevu ya kutoa!
      Na kwa kuwa hili litawalenga mafisadi bila shaka litapotelea mikononi mwao bila hata ya kusikika.

      Ni Tanzania zaidi ya tuijuavyo!

  • Rais wao alisema ni upepo – utapita tu,
    Sasa kitakuwa kimbunga cha kuwapepesua wateule wa Rais kwani ubadhilifu wa mali zetu umepitiliza

  • Hatua nzuri lakini mkurugenzi kwani yeye hajui watumishi wake kama wapo hai au wamekufa?? Tuseme kwani huwa hakutani nao au ye anaishi Marekani na watumishi wako Magu? Nafikiri na yeye anatakiwa kusimamishwa ili kupisha uchunguzi na hatua za kisheria zichukuliwe.

  • Mheshimiwa Rais Kikwete alipokuwa anawaacha mawaziri waliotajwa kwenye hoja za ukaguzi za mkaguzi mkuu Ludovick Utoh alisema hata watendaji walio chini ya mawaziri hao watawajibika.

    Hiyo ni kwa ajili ya serikali kuu sasa je wale waliotajwa kwenye tume ya Agustino Mrema Je watabaki madarakani.

    Sijui kama mkurugenzi huyu wa Magu alitajwa kwenye ripoti ya ukaguzi ya mheshimiwa Lyatonga, lakini kama alivyosema msemaji aliyepita

    Kazi ya kwanza ya mkurugenzi ni kuwafahamu kwa majina wafanyakazi wake,

    Pili kufahamu familia za wafanyakazi hao maana yake msiba au tatizo lolote linapotokea kwani Mkurugenzi ndiye anayetangaza hata misiba ya wafanyakazi wake ni wajibu wake ndiye mtendaji mkuu

    Ikiwezekana ataje jina la mtoto mfano John amemaliza shule , sasa swali ikitokea msiba nani wa kuutangaza kama siyo mkurugenzi

    Hakuna chochote kitakachofanyika kwenye kurugenzi bila ridhaa ya mkurugenzi au kaimu wake kwa kibali cha mkurugenzi.

    Mishahara yote lazima hundi iidhinishwe na mkurugenzi ndiye anayejua idadi ya wafanyakazi wake maeneo walipo kazi wanazofanya tarehe za ajira nk chukua mfano mfanyakazi amekufa yeye mkurugenzi ndiye wa kuandika dokezo la kumfuta kwenye payroll

    Kama sivyo basi kuna namna labda kushirikiana na Mhasibu na labda fedha hizo zinatumika kama petty cash au mikopo nafuu nk

    Kumfukuza mhasibu ni kumwonea kwasababu lazima mkurugenzi anajua kama hajui ni mzembe na hafai kuwa mkurugenzi na naomba mheshimiwa Kikwete aanze naye ili kuwa kama mfano kwa wengine kwani kama kuna majina mengi ya marehemu wengi kwenye payroll ni hasara kubwa kwa taifa na hizi ni fedha za walipa kodi

    ili Mheshimiwa Rais aweze kurudisha imani kwa wananchi wale wote wanaotajwa kwenye taarifa hizi za ukaguzi ,ufisadi, wizi wa mali za umma kwa ujumla wake lazima waajibishwe na ikiwezekana kushtakiwa .

    Mheshimiwa Kikwete chukua fagio la chuma kama alivyochukua Rais Mwinyi na kulinda heshima yake hadi leo

    Mungu ibariki Tanzania

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *