JIJI la Dar es Salaam linalokadiriwa kuwa na idadi ya wakazi wanaokaribia milioni sita kwa sasa na linaongoza kwa watu wake kula nyama. Linaongoza kwa kula nyama ya ng’ombe na hata wanyama wengine wanaofugwa.
Hata hivyo, Dar es Salaam sensa ya mwaka 2012, ilionesha kuwa jiji hilo lilikuwa na takribani watu milioni 3.4, huku kukiwa na asilimia 2.7 ya ongezeko la watu kila mwaka. Katika jiji hilo, zaidi ya ng’ombe 1,200 huchinjwa kila siku na kusambazwa kwa walaji. Maeneo mengi yanauza kilo moja ya nyama ya ng’ombe kwa shilingi 6,000 hadi 7,000.
Uchunguzi uliofanywa na FikraPevu kwa wiki mbili sasa unaonesha kuwa wanaume ndiyo wanaoongoza ‘kutafuna’ nyama kuliko wanawake wala watoto.
Imedhihirika kuwa wanaume wanakula zaidi nyama wanapokuwa matembezini; hasa sehemu za starehe(baa), ambako hupendelea kula nyamachoma na mishkaki, huku wakisukumizia na vinywaji.
“Ni dhahiri kwamba wanaume wanakula sana nyama wanapokuwa baa na maeneo mengine ya starehe, hii ni tofauti na wanawake na hata watoto,” anasema Castico Ismail, mmoja wa wapenzi wa Tamasha la Nyamachoma.
Castico anasema wanaume wengi wanapenda tamasha hilo kwa kuwa ni wapenzi wa nyama na zaidi sana hujitokeza kwa wingi kwa kuwa kuna burudani na michezo mbalimbali kila linapoandaliwa. Tamasha hili sasa hufanyika nchi nzima kwa vipindi tofauti.
Pamoja na kwamba haijawa rahisi kufahamu kiasi halisi cha nyama kinacholiwa na wanaohudhuria tamasha hilo, lakini taarifa zinaeleza kuwa nyama ya ng’ombe kilo 440 au zaidi hutafunwa na walaji. Pia nyama ya mbuzi na kuku huchomwa na kutumika siku hiyohiyo.
Kameloi ole Kilepai, Mmasai na moran wa kabila hilo anasema; “kwamba wanaume ni walaji wa nyama na wanatakiwa kula nyama zaidi kuliko vyakula vingine vya wanga wala mazao mengine. Masai hula nyama kama chakula na siyo kitoweo kama ilivyo kawaida kwa Watanzania wengi.
Kilepai anasifia nyama na kueleza kuwa ni chakula kitamu, chenye lishe bora na virutubisho muhimu kwa kujenga mwili na kwa uelewa wake, “nyama huimarisha kinga ya mwili.”
Mtaalamu wa lishe kwa binadamu na afya ya mwili, Kalengamye Mlongo akizungumza na FikraPevu anasema pamoja na uzuri wa nyama kwa afya ya mwili, lakini ni chakula chenye madhara makubwa kwa binadamu. Anasema binadamu anatakiwa, kitaalamu, kula nusu kilo tu ya nyama kwa wiki na siyo zaidi, lakini Watanzania wanakula zaidi.
“Kila mtu, kuanzia miaka 18, anatakiwa kula nusu kilo tu ya nyama kwa wiki na kuzidisha ni kujitakia matatizo ya afya, ambayo mengine siyo rahisi kupona,” anaeleza mtaalamu huyo wa lishe.
Mlongo ambaye sasa anajiendelea kielimu katika Chuo Kikuu cha Kampala, akisomea udaktari, anaeleza kuwa kila chakula kinapoliwa kwa ziada, kinaweza kabisa kuwa chanzo cha magonjwa na kushauri kutumika kiasi, ili kulinda afya na kuepuka kujaza tumbo.
Daktari Mayoel Kisai anasema ulaji wa nusu kilo ya nyama kwa binadamu huufanya mwili kupata kiasi cha protini kinachotakiwa na mwili, lakini ziada ya kiasi hicho ni uharibifu wa nyama na kuvuruga mfumo wa mwili kufanya kazi zake.
Anasema mwili unahitaji protini ambayo inapatikana kwenye nyama, lakini isiwe kiasi kikubwa kwa kila siku. “Unaweza kula nyama leo; iwe ya kuchoma au kuchemsha, ili kupata protini gramu 10 mpaka 15, na jumla yake ifikie gramu 110 kwa wiki, ikizidi hapo ni upotevu tu unaofanyika na kujaza tumbo,” anasema mtaalamu huyo wa afya ambaye anafanya kazi hospitali ya Iweko, Dar es Salaam.
Anashauri Watanzania wapende kula nyama ya kuchemsha zaidi, badala ile ya kuchomwa kwa kuwa kupika husaidia kuua baadhi ya vimelea vinavyopatikana katika nyama.
“Nyama ya kuchoma, pamoja na kuwa tamu na inayovutia, lakini usalama wake hauko sawa na nyama ya kupika, hii husaidia kumaliza vimelea na wadudu wadogo wanaopatikana katika nyama na hatari iko sana kwa wale wanaokula nyama mbichi,” anaongeza na kushauri watu kupunguza matumizi ya nyama.
Anasema, “Mnyama yeyote huishi akiwa na baadhi ya vimelea rafiki kwa uhai wale na hata anapochinjwa, vingine havifi haraka kwa kuwa huendelea kuishi hadi damu na majimaji ya nyama yanapokauka, sasa ukila nyama mbichi, mtumiaji humeza vimelea hivyo, hata kama havina madhara makubwa, lakini kitaalamu haishauriwi kuingia kwa binadamu vikiwa hai.”
Daktari huyo anasema kula nyama ya mnyama aliyechinjwa siku hiyohiyo hakushauriwi sana, kwa kuwa nyama nzuri ni ile inayokaa ndani ya majokofu kwa siku saba au zaidi.
“Nyama ikihifadhiwa kwa zaidi ya siku saba, huwa laini na kiafya ni nzuri mno kwa kuwa wale wadudu na vimelea rafiki nao wanakuwa wamekufa, hivyo kuiacha nyama ikiwa salama,” anasema daktari Kisai.
Je, wasiokuwa na majokofu wafanyeje? Daktari huyo anasema hawa ni vyema wakaikausha nyama hiyo kwa moto na kuila siku zinazofuata.
Ni kutokana na wingi wa wanaume kuwa walaji wa nyama wakubwa kuliko wanawake na watoto, idadi yao pia ndiyo inaongoza kwa kunyemelewa ama kukumbwa na magonjwa yatokanayo na matumizi ya nyama. Daktari Kisai anasema wanaume wengi wanakumbwa na saratani ya utumbo, kisukari na magonjwa ya moyo kwa kuwa mengi husababishwa na ulaji wa hovyo wa nyama.
Akizungumzia magonjwa hayo kwa kirefu, Mlongo anasema utafiti unaonesha ulaji wa nyama nyekundu – hasa ng’ombe una madhara makubwa kwa mwili na afya ya binadamu. Anasema ulaji wa nyama huchochea kupatikana kwa magonjwa ya moyo kwa kuwa nyama ina lehemu, hii hukaa kwenye mishipa ya damu ya binadamu na kusababisha damu kushindwa kupita vizuri.
“Ulaji wa nyama kwa kuwa huchochea kuwepo kwa lehemu kwenye mishipa, husababisha viungo muhimu vya mwili kama moyo, kushindwa kupitisha damu ya kutosha baada ya mishipa mingi kujaa mafuta yanayokwamisha usafiri wa damu kuwa rahisi,” anasema.
Anasema pamoja na umuhimu wa lehemu katika mwili, lakini inayotengenezwa na mwili wenyewe, inatosha kulainisha safari ya damu kwenye mishipa, lakini inapozidi, mishipa inaweza kuziba na kusababisha kifo cha ghafla.
Mlongo anataja ugonjwa mwingine unaotokana na ulaji wa ziada wa nyama ni kansa ya utumbo mkubwa. Anasema nyama nyekundu ikiliwa inakaa saa kuanzia 13 hadi 72 kwenye mfumo wa chakula wa binadamu, tofauti na vyakula vingine.
Utafiti unaonesha limbikizo hilo linaambatana na hatari ya kupata ugonjwa wa kansa ya utumbo mkubwa kwa kuwa nyama “kuishi” muda mrefu kwenye joto la matumbo, inaweza kubadilika na kujijengea mgando ambao unaweza kuleta madhara kwenye kuta za ukumbo mpana na hatimaye kidonda ambacho hugeuka kuwa kansa.
Utumbo mpana wa binadamu una urefu wa futi tatu hadi tano na urefu huo ukichanganywa na ule wa utumbo mwembamba wa futi 18 hadi 23, hufanya urefu wa utumbo wote wa mtu mzima kuwa futi zaidi ya 27.
Ulaji wa ziada wa nyama pia unatajwa na Daktari Kisai kuwa unaweza kusababisha ugonjwa wa kisukari. Anasema hatari nyingine ya ulaji wa nyama kupindukia ni kupata ugonjwa wa Alzheimer; huu ni ugonjwa wa akili ambao huwapata watu wengi uzeeni na dalili yake ikiwa ni kupoteza kumbukumbu kabisa.
Wanasayansi wanaamini protini inayopatikana kwenye nyama uharibu mishipa ya fahamu ya kwenye ubongo na kuchangia kwa ugonjwa huu.
Wataalamu hawa wa afya na lishe wanautaja ugonjwa mwingine kuwa ni ugonjwa wa kifafa; minyoo inyopatikana kwenye baadhi ya maeneo ya nyama ya ng’ombe huweza kupaka kwenye ubongo na kuharibu mishipa ya fahamu ya ubongo hali ambayo husababisha kifafa kwa watu ambao hawakuzaliwa nacho kabisa.
“Ili kuzuia baadhi ya magonjwa haya ni kuhakikisha watumiaji wa nyama wanachemsha kwa muda mrefu – hadi iive, nyama ambayo imepatikana muda mfupi baada ya mnyama kuchinjwa,” anasema Daktari Kesai. Pamoja na magonjwa hayo, utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Adelide, Marekani kimegundua kuwa ulaji wa nyama kupita kiasi kumefanya idadi kubwa ya watu duniani kuwa na uzito mkubwa ambao unaweza kuwa chanzo cha magonjwa mengine.
Unene uliopitiliza unaotokana na kula nyama nyekundu ina kiwango kikubwa cha mafuta ambacho hakihitajiki mwilini.
“Kitambi, ambacho ni matokeo ya ulaji wa nyama nyekundu, ni hatari sana kwani husababisha matatizo mengi ya kiafya na kisaikolojia, vifo vya ghafla na kushindwa kufanya kazi vyema kwa baadhi ya viungo vya mwili, jambo ambalo ni hatari sana kwa maisha ya watu,” inasomeka sehemu ya matokeo ya utafiti huo uliofanyika Texas, Marekani, mwaka 2014 ukihusisha watu 1000.
Akizungumza na FikraPevu, Waziri mwenye dhamana ya afya na rika, Ummy Mwalimu amewataka Watanzania kula vyakula vyote kwa kiasi, huku akiwahimiza kufanya mazoezi.
“Kula au kunywa kwa kiasi kwa kila kitu ni jambo muhimu sana, ni vyema sasa Watanzania wakajifunza hili na pia kutenga muda wao kufanya mazoezi ili kujiepusha na magonjwa mengi yanayotokana na ulaji wa ziada,” anasema.
Hivi karibuni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alizindua kampeni iliyoasisiwa na Waziri Ummy ya kufanya mazoezi kwa kila Mtanzania ili kujiepusha na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza, yakiwamo hasa yanayotokana na mfumo wa maisha na ulaji.