TANZANIA ina upungufu mkubwa vitabu vya elimu kwa ajili ya kufundishia (kiada) na kujifunzia (ziada) jambo ambalo limechangia ongezeko la waandishi wengi.
Kuibuka kwa wimbi la waandishi wengi Watanzania kumefanya kuwepo na baadhi ya vitabu ambavyo vina muundo unaomfanya mwanafunzi kukariri badala ya kuelewa, huku vingine vikiwa na vitu vichache kiasi kwamba inakuwa haina tofauti na notisi za mwalimu.
FikraPevu inafahamu kwamba, vitabu ni sehemu ya kuongeza uelewa na ujuzi wa vitu kwa mwanafunzi, lakini kwa mwalimu pia ni sehemu ya kufanyia maandalio ya mamsomo kwa kuchukua baadhi ya vitu ambavyo anaweza kwenda kufundishia darasani.
Kwa maana nyingine, vitabu hivyo vinatarajiwa kuwa na vitu vingi vya ziada kwa mwanafunzi na hata mwalimu, ambaye mambo anayofundisha darasani yanatakiwa kuwa kama mwongozo ili mwanafunzi anaporejea kwenye kitabu ajifunze zaidi.
Lakini vitabu vingi vinapoandikwa katika mtindo wa ufupisho (summary) kwa kutoa maana ya maneno tu au baadhi ya vitu hii huwafanya wanafunzi kukariri na walio wengi huishia kusoma notisi ambazo wamepewa na walimu wa shule au katika masomo ya ziada (tuition) kwa kuona hakuna tofauti kati ya vitabu na kile ambacho wamepata kutoka kwa walimu hao.
FikraPevu ilizungumza na Aloyce Makopa, mwalimu taraji wa hisabati na kompyuta aishiye jijini Mwanza, ili kujua wakati anafundisha huwa anapendelea kutumia vitabu gani.
Mwalimu Makopa, kwanza alikiri kuwa vitabu vingi vya waandishi wa Tanzania havina vitu vingi, hivyo humlazimu kuchanganya vitabu hasa kilichoandikwa na S. Wakamoga na Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE).
“Bila kuchanganya vitabu huwezi kupata notisi zilizokamilika ikiwa tu utategemea kitabu kimoja ambacho ni ‘chepesi’, kwa maana hakina mambo mengi yanayopaswa kufundishwa,” anasema.
Kitendo cha mwalimu kuchanganya vitabu ili kupata notisi kinafanya mwanafunzi aishie kusoma vitu alivyopewa kwa sababu maudhui yanakuwa na uzito mkubwa kuliko yale yanayopatikana kwenye vitabu, jambo ambalo halipaswi kuwa hivyo kwa sababu mwalimu anapofundisha huwa hatoi kila kitu, bali hutoa mwongozo na mifano ili kumfanya mwanafunzi aongeze juhudi kwa kujifunza yaliyomo kwenye vitabu hivyo.
Ni kwa mtindo huo ambapo mwanafunzi hupanua uelewa wake wa kuyatanzua mambo, hivyo huweza kuelewa na siyo kukariri.
Kuna miundo ya uandishi wa vitabu ambayo mwanafunzi akiiona inamfanya kuanza kufikiria ni kwa namna gani kitu fulani kiwe hivyo, mwanafunzi anakuwa na uwezo wa kujenga hoja na kutamani kupata majibu huku akiongozwa na mifano iliyotolewa na walimu, ukiongezea na namna mwandishi wa kitabu alivyoandika na kuweka vitu vingi vya muhimu ambavyo vipo humo.
Lakini kwa hali iliyopo, vitabu vya sasa vina namna ya maandishi ambayo yanashawishi kufanya mtu awaze kukariri kwa ajili ya kujibu mtihani na siyo kuelewa kama inavyopasa, hii ikiwa na tafsiri kwamba, vitabu vvya sasa vimeandikwa ili mwanafunzi aweze kujibu mtihani.
Ushahidi wa hili unaweza ukaonekana kwa kulinganisha vitabu ambavyo vimeandikwa na waandishi kutoka nchi tofauti na Tanzania hasa kutoka Ulaya.
Kwa mfano, ukiangalia kitabu kilichoandikwa na John Avison kiitwacho The World Of Physics kinachotumika kwa ajili ya elimu ya sekondari (GCSE) Uingereza na kile cha Physics for Secondary Schools Form 4 kinachomilikiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi kitumikacho kwa ajili ya wanafunzi wa sekondari Tanzania, tena wa kidato cha nne, utanona kuna tofauti kubwa.
Mada ya Electromagnetism (Sumaku) katika kitabu cha Avison mada hii inapatikana katika ukurasa wa 192 na ni mada ya 15 wakati kitabu cha Wizara ya Elimu mada hiyo inapatikana ukurasa wa 36 na ni topiki ya pili.
Ipo tofauti kubwa sana ya kiuandishi na vitu vilivyomo katika vitabu hivyo. Katika kitabu cha kidato cha nne Tanzania, kutoka ukurasa wa 36 hadi wa 37 ambapo kuna utangulizi wa mada husika hakuna picha hata moja kuonyesha uhalisia wa magnetism (Sumaku) sehemu ambayo ujuzi wake unatumika, badala yake kuna maandishi mengi na michoro mitano.
Hili ni tofauti kabisa katika kitabu cha Avison katika kurasa mbili kuna picha tatu na michoro mitatu, picha hizo zinaonyesha sehemu ama mazingira ambayo sumaku inaweza kutumika na ufafanuzi wake unaonyeshwa kwa michoro.
Kwa hali hii inamshawishi mwanafunzi kufikiri zaidi kwa kuona uhalisia na kumuepusha kukariri maandishi pekee bali anajengewa kumbukumbu kwa kutumia vitu halisi.
Endapo utachukua wanafunzi wawili ambao wamesoma vitabu hivyo viwili, yaani mmoja aliyesoma kitabu cha mwandishi wa Tanzania na mwingine akasoma kitabu cha mwandishi wa Ungereza, kisha ukawapa sumaku na ukawaambia waitumie kwenye uhalisia, mwanafunzi aliyetumia kitabu toka Tanzania anaweza akashindwa.
Kwenye mitihani mingi Tanzania kuna aina ya maswali ya kuelezea maana ya neno fulani, kwa mfano, “Ielezee Sumaku” (Define Electromagnetism). Uandishi wa kitabu cha Fizikia kidato cha nne upo katika mtindo wa kumfanya mwanafunzi kujibu swali hilo na kutoa maana moja kwa moja kutoka kwenye kitabu, kwa sababu ukurasa 36 baada ya kichwa cha mada “Electromagnetism” mwandishi ameanza na kutaja maana ya neno huku maana hiyo ikiwa imekolezewa boksi la rangi nyekundu kumuonyesha mwanafunzi sehemu hiyo kuwa ya muhimu kuliko nyingine.
Kwenye kitabu cha Avison, mada inaanza kwa kumjengea mwanafunzi uelewa (concept) na kumpa mwanafunzi picha ya jumla jinsi “sumaku” ilivyo kiasi cha kwamba inampa changamoto ya mwanafunzi kufikiri zaidi na hata kujiuliza ama kuuliza maswali mengi.
Kama sera ya viwanda inataka ifanikiwe ni lazima waandishi hasa wa vitabu vya sayansi wazingatie uandishi wa vitabu kwa namna ambayo inaweza kumfanya mwanafunzi kuwa mbunifu na kuweza kutumia kile ambacho anakisoma katika mazingira yanayomzunguka na hivyo kuhamasisha wanafunzi na watu wengi kupenda kujisomea vitabu.