Ripoti mpya iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB) imesema urahisi wa kuanzisha biashara nchini Tanzania uko chini ya wastani unaotakiwa na nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, sababu inayokwamisha ukuaji wa sekta binafsi na uchumi wa wananchi.
Ripoti hiyo ambayo imetolewa mapema mwaka huu ni matokeo ya utafiti kupitia mradi wa ‘Doing Business’ katika nchi 190 duniani kwa mwaka 2017 na kuchambua takwimu za sheria na sera zinazosimamia sekta ya biashara ambapo imeielezea Tanzania kama nchi ambayo inayokabiliwa na changamoto mbalimbali za kimchakato katika uanzishaji wa biashara.
Tanzania iko nafasi ya 162 sawa na asilimia 73.03 kati ya nchi 190 duniani ambapo kiwango hicho kiko chini ya wastani wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara cha asilimia 76.82. Tanzania inaungana na nchi za Malawi na Botswana ambazo ziko kwenye kundi moja la nchi zilizo chini ya mstari wa ‘frontier score’
Kwa mujibu wa ripoti hiyo asilimia 100 ni sawa na ‘Frontier score’ alama inayotambulisha nchi zenye utendaji mzuri zaidi kwenye uchumi hasa urahisi wa kufanya biashara. Upangaji wa kuupa nafasi uchumi wa nchi katika urahisi wa kuanzisha biashara unapatikana kwa kuangalia umbali wake kufikia ‘Frontier scores’ambapo ni kiwango bora cha kuanzisha biashara.
URAHISI WA KUANZISHA BIASHARA KWA NCHI ZA AFRIKA
Frontier scores hutofautiana kulingana na kanda na kiwango cha ukuaji wa uchumi na hali ya kisiasa ya nchi husika.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa katika nchi 5 za Afrika Mashariki, Tanzania bado haina mwelekeo mzuri wa urahisi wa kuanzisha biashara ambapo imeshika nafasi 4 kwa kupata asilimia 73.03 ikifuatiwa na Uganda. Burundi ndio nchi yenye mazingira rahisi ya kiuchumi ya kuanzisha biashara ikiwa na 91.94% ikifuatiwa na Rwanda (87.62%) pamoja na Kenya (83.20).
Wastani wa nchi za Afrika Mashariki kwa mazingira rahisi ya kiuchumi ya kuanzisha biashara ni 81.62%. kwa muktadha huo Tanzania na Uganda ziko chini ya wastani unaohitajika huku Kenya, Burundi na Rwanda zikiwa juu ya wastani unaotakiwa.
Utafiti ulitumia njia mbalimbali kupata matokeo ambapo uliweka viashiria vya urahisi wa kuanzisha biashara vikiwemo; muda, gharama, mtaji na mchakato wa kupata vibali vya biashara.
Kulingana na vigezo hivyo, Tanzania imeangushwa na ongezeko la ada ya usajili inayotozwa kwenye ardhi na makazi ambako biashara mpya zinafunguliwa. Pia ukiritimba wa upatikanaji wa leseni na mlundikano wa kodi kwa wafanyabiashara na kodi mpya inayokatwa kwenye mishahara ya wafanyakazi.
Ili kutimiza malengo ya mradi huo, utafiti huo uliangazia mambo mengine muhimu ikiwemo mtaji wa kuanzisha biashara, vibali vya ujenzi, kupata umeme, hati ya ardhi na nyumba, mikopo, ulinzi kwa wawekezaji, ulipaji kodi, biashara nje ya mipaka, utekelezaji wa mikataba na ufilisi wa mali.
Kwa upande wa dunia, New Zeland imekuwa nchi ya kwanza miongoni mwa nchi 10 zenye urahisi wa kufanya biashara, ikufuatiwa na Singapore pamoja na Denmark.
URAHISI WA KUANZISHA BIASHARA KWA NCHI ZA AFRIKA YA MASHARIKI
Lakini nchi za Somalia, Congo DRC, Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Libya, Yemen, Sudan ya Kusini, Venezuela na Eritrea zimewekwa kwenye kundi la nchi 10 za mwisho ambazo sio rahisi kufanya biashara. Sababu kubwa ni vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyochochewa na makundi ya waasi wasioridhishwa na mwenendo wa siasa za nchi husika.
Mapendekezo ya ripoti hiyo kwa Tanzania ni kuboresha mfumo wa upatikanaji wa hati za ardhi na majengo ya kufanyia biashara ili kuvutia wawekezaji wengi kwa muda mfupi na kupunguza gharama na mchakato wa kupata vibali vya biashara. Pia kulegeza masharti ya ulipaji kodi kwa sekta binafsi.